Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stanslaus Shing'oma Mabula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KITETO Z. KOSHUMA) aliuliza:- Bodi ya Utalii pamoja na mambo mengine ina jukumu la kutunza utalii wa ndani ya nchi:- Je, Serikali inasimamiaje Bodi hiyo ili kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unatangazwa kama Mji wa Kitalii?
Supplementary Question 1
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kuonesha wazi kwamba kama Wizara wanatambua namna ambavyo Mji wa Mwanza una vivutio vingi na unaweza kuwa sehemu ya utalii kwenye nchi hii. Sasa nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa spika, moja ni kwamba pamoja na mazingira na vivutio vingi vilivyopo ni nini sasa mkakati wa Wizara kuhakikisha kwamba ili watalii waje ni lazima wapatikane watu wanaosababisha watalii kuja. Tunatambua ili watalii hawa waje wanatakiwa wawe na watu wenye weledi ambao vijana wamefundishwa kwa kuona maeneo ambayo tunaweza kuwa na ma-tour guide wazuri ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha vijana wengi waliopo Mwanza wanapatiwa mafunzo haya na kufanya kazi hii vizuri.
Mheshimiwa spika, la pili; tunatambua kwamba TTB tayari kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na St. Augustine University wameanzisha Mwanza Tourism na kupitia mkakati huo tayari Wizara kwa maana ya halmashauri pamoja na Ubalozi wa Ujerumani wameanza ukarabati wa ile Gunzeki House ambayo iko pale Makoroboi itakayokuwa ni moja ya majumba ya maonesho ya historia pamoja na ile Gallostream Nini mkakati wa Wizara kuhakikisha maeneo haya yanapewa kipaumbele na kuwa moja ya vivutio katika Mji wa Mwanza, nakushukuru sana. (Makofi)
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mabula kwa namna ambavyo tumekuwa tukishiriki kwa pamoja katika juhudi hizi za kuifanya Mwanza kuwa hub ya utalii wa Mikoa ya Kaskazini Magharibi. Tulikuwa nae kwenye kongamano hilo ambalo nimelisema na alishiriki kwenye kuchangia mambo mazuri sana ambayo Wizara inayafanyia kazi, kwa hiyo nampongeza sana.
Mheshimiwa Spika, ameuliza ni mkakati upi wa Wizara katika kuhakikisha kwamba tunapata washiriki wengi katika shughuli za utalii katika mikoa hiyo. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Wizara katika nyakati mbalimbali imefanya mikutano na wadau katika Mkoa wa Mwanza na tumeendelea kufanya semina mbalimbali kupitia ofisi yetu ya idara ya utalii lakini pia kupitia TTB na hivi karibuni tutafanya mkutano mwingine kutathmini kikao tulichokifanya pale awali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu tu ni kwamba naomba kuwakaribisha wadau wote wa utalii wa Mkoa wa Mwanza na watu walio na interest ya kufanya biashara ya utalii kama alivyosema mwenyewe, watalii wanaletwa na watu na watalii wanatafutwa lazima wawepo wapo Mkoani Mwanza wanaotafuta watalii. Sisi tutakuwa tayari kufadhili mafunzo hayo ili kuhakikisha kwamba tunapata watu wengi wanaoshirikiana na jambo hili.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili amezungumzia kuhusu ukarabati wa jengo lililopo Makoroboi na kwamba ni upi mkakati wa Wizara. Wizara yetu imeendelea kutoa utaalam katika maeneo haya na katika maeneo mengine kwa mfano pale Mkoani Iringa lilikuwepo pia jengo la mkoloni ambalo zamani ilikuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya lilikarabatiwa na kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha RUCO sasa hivi jengo hilo ndilo ambalo linaonesha makumbusho na historia mbalimbali ya Mkoa ywa Iringa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawapongeza sana Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kwa kuandaa kila mwaka Mwanza Tourism ambapo wamekuwa wakipeleka watu mbalimbali katika Kisiwa cha Saa Nane na kuwazungusha katika Jiji la Mwanza. Juhudi hizi tunaziunga mkono tutaendelea kushirikiana na Mkoa wa Mwanza.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa, lakini kwa kuwa circuit ya Kaskazini Magharibi ni circuit ya Kimkakati kwenye Serikali ya Awamu ya Tano hususan kwenye Sekta ya Kiutalii, napenda niongeze mambo yafuatayo ambayo tunayafanya na tunakusudia kuyafanya katika circuit hii ya Kaskazini Magharibi.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye miundombinu (hard infrastructure) kama vile Reli ya SGR ambayo itafika mpaka Mwanza, viwanja vya ndege; Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kitakuwa cha Kimataifa na sasa hivi ujenzi unaendelea pale. Vile vile ukiunganisha na mtandao wa Viwanja vya Ndege vilivyopo katika circuit hii, Kiwanja cha Ndege cha Chato, Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Kigoma, Tabora pamoja na cha Musoma vyote vinafanyiwa first lifting ili kuhakikisha kuna ndege zinatua regularly katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, hiyo ni sambamba na mtandao wa lami. Pia tunawekeza katika softly infrastructures ambapo sasa hivi tumewaelekeza Chuo cha Taifa cha Utalii wafungue Tawi kwa ajili ya kuongeza idadi ya vijana ambao wanasomea mambo ya utalii, tour guiding, upishi na vitu vingine katika Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Spika, mbali na hayo yote, circuit hii ya Magharibi ina bahati ya kuwa na maziwa na mito na tumeona kwamba hii ni unique feature ambayo kama tukiitumia vizuri itaifungua kwa kasi sana circuit ya Kaskazini Magharibi ambapo kwa kuanzia, tumewaelekeza TANAPA na tayari wameshafanya manunuzi ya boti ambayo itakuwa ni luxury kwa ajili ya utalii, itakuwa inachukua watu 50 na itakuwa inazunguka kutoka spix gulf kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, inakwenda, ina-dock Mwanza, itakuwa ina-dock pale Kisiwa cha Saa Nane, Kisiwa cha Rubondo lakini pia kwenye eneo la Katete ambapo Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato inaanzia. Hii boti itakuwa ni luxury na itakuwa inatumia masaa takribani matatu na nusu mpaka manne kutoka Serengeti kufanya huo mzunguko wote.
Mheshimiwa Spika, tunakusudia boti hiyo itakuwa ni ya business class lakini tumewaelekeza pia TANAPA wawekeze kwenye manunuzi ya boti nyingine ambayo itakuwa economy class ambayo itachukua watu 300 kwa ajili ya kuwazungusha kwenye Ziwa Victoria ili kuvinjari katika Ziwa, lakini pia Visiwa vilivyoko pale na maeneo ya Hifadhi ambayo yanaungana moja kwa moja na Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipenda kuongezea hayo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved