Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Halima Abdallah Bulembo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU) aliuliza:- Mkoa wa Kagera una vijiji 134 ambavyo havijafikiwa na umeme wa REA; Biharamulo Vijiji 29, Bukoba Vijiji 9, Karagwe Vijiiji 8, Kyerwa Vijiji 31, Misenyi Vijiji 5, Muleba Vijiji 25 na Ngara Vijiji 27:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA katika Vijiji hivyo? (b) Umeme wa REA ulifika kwenye vijiji vingi lakini haukusambazwa: Je, mradi wa ujazilizi utaanza lini Mkoani Kagera ili wananchi waliorukwa wapatiwe umeme?
Supplementary Question 1
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri kabisa, lakini nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mkoa wa Kagera siyo vijiji peke yake ambavyo havijapata umeme wa REA. Kumekuwa na Taasisi kubwa kama shule na Vituo vya Afya ambavyo bado havijapata umeme wa REA na kupelekea kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa kwa wakati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taasisi hizi zinapata umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakikumbwa na kadhia ya kulipishwa nguzo za umeme. Serikali au Wizara inazungumziaje kadhia hii inayowakuta wananchi wa Mkoa wa Kagera? Nakushukuru. (Makofi)
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Halima Bulembo anapofuatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Kagera. Nampongeza sana na kweli kazi kubwa imeonekana kutokana na jitihada zake hasa kwa kupitia vijana. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika masuala yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza anataka kujua kuhusiana na upelekaji wa umeme katika taasisi za Umma. Naomba nitoe maelekezo kwa Halmashauri zetu na Waheshimiwa Madiwani wanaonisikiliza. Ni kweli Serikali imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo yote hasa vijijini lakini baadhi ya taasisi zimekuwa hazilipiwi na wamiliki wa taasisi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana wamiliki wanaohusika walipie gharama ya 27,000 ili taasisi zote zipelekewe umeme. Maelekezo na mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha taasisi zote zinapelekewa umeme. Nakupongeza Mheshimiwa Halima Bulembo kwa sababu katika Mkoa wa Kagera hadi sasa taasisi 897 zimepelekewa umeme na hii ni jitihada kubwa. Naomba maeneo mengine ambayo hayajapelekewa umeme, wanaohusika waendelee kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia taasisi tukiwa na maana ya shule, Vituo vya Afya, Zahanati, Misikiti, masoko na hata kama kungekuwa na maeneo madogo ya viwanda. Kwa hiyo, nitoe sana ombi kwa Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri tupeleke kwa kulipa shilingi 27,000/= katika Taasisi za Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili kuhusu kulipishwa nguzo; ni kweli zipo changamoto katika baadhi ya maeneo, yapo maeneo bado Wakandarasi na Mameneja wa TANESCO wanaendeleza kutoza nguzo wateja. Naomba nitoe tamko kali sana kupitia Bunge lako Tukufu kwamba ni marufuku kutoza nguzo kwa wateja wote; iwe Mkandarasi awe Meneja wa TANESCO, awe Injinia, awe Kibarua wake ni marufuku kulipiza mteja nguzo. Hii ni kwa sababu Serikali imegharamia kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved