Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Shirika la Mzinga limekuwa likifanya kazi zake kwa weledi na uaminifu mkubwa lakini lina changamoto za vifaa kama vile mashine za ramani:- Je, kwa mwaka 2019/2020 Serikali ilitenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya Shirika hilo?

Supplementary Question 1

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, shirika limekuwa likipata tenda kutoka ndani ya Serikali na limekuwa likifanya kazi hizi kwa weledi mkubwa sana. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha shirika linalipwa kwa wakati ili hata zile changamoto ndogondogo wanapopata zile hela kwa wakati wapate kuzitatua wenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miundombinu ya haya mashirika, hiki Kikosi cha Mizinga kwenye makambi mengi ni chakavu na si rafiki sana na ni siku nyingi. Sasa Serikali ina mikakati gani ya kutenga fedha na kuangalia hiki kitengo kwa sababu hiki kitengo ni kwa kazi maalum na kinafanya kazi kwa ujasiri na kwa weledi mkubwa. Je, Serikali na Wizara ya Fedha ina mkakati gani kuhakikisha kwamba kile kinachotengwa kwa ajili ya kitengo hiki kinapelekwa ili kutoa hizi changamoto ambazo zipo katika Kikosi hiki cha Mizinga katika hili Shirika la Mzinga? Ahsante.

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu malipo kwa kazi ambazo shirika linafanya za Serikali naweza nikamueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba malipo hayo yanafanyika. Hivi karibuni Shirika la Ujenzi la Mzinga limepata kazi kadhaa ikiwemo ujenzi wa ofisi za Serikali hapa Dodoma, lakini katika baadhi ya halmashauri pia wamekuwa wakipata kazi. Kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba malipo yanafanyika na fedha hizo zinawasaidia kuboresha mambo madogomadogo katika shirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miundombinu ya shirika lenyewe; ni kweli kwamba kwa kiwango kikubwa miundombinu pale katika Shirika la Mzinga imechakaa, ni ya muda mrefu na ndiyo maana kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba sasa wametengeneza mpango mkakati ambao kwa kiwango kikubwa ukipata fedha utaweza kushughulikia yote haya ikiwemo kuboresha miundombinu, lakini kuleta wataalam waliobobea katika fani hizo na kuwa na mtaji wa kuweza kuendeleza shirika hili. Ni matumaini yetu kwamba mpango mkakati huo utapitishwa na Serikali ili shirika liweze kupata fedha na kuweza kuboresha miundombinu yake.