Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Justin Joseph Monko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Primary Question

MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Inapotokea Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa/Kijiji amefariki au kupoteza sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji husika huongozwa na Kaimu Mwenyekiti:- Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuwepo uchaguzi mdogo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?

Supplementary Question 1

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba, sheria na taratibu zinaruhusu uchaguzi huo; na kwa kuwa, wanatambua kwamba, maeneo mengi yalikuwa pia yana makaimu na chaguzi hizo hazikufanyika. Je, Serikali sasa inatoa maelekezo gani kwa watendaji wanaohusika ili wawe wanachukua hatua zinazostahili kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sasa hivi tuko kwenye mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utaondoa kabisa makaimu hawa ambao wamekuwa ni kero kwa maeneo mengine na tumesikia chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, wametangaza kujitoa katika uchaguzi huu na kuwakosesha wananchi haki yao ya kimsingi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa Katiba yetu na Serikali ya Vyama Vingi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kadhia hii ambayo inaendelea nchini? Ahsante sana.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua kwa nini nafasi hizo zilikuwa hazijazwi kama ambavyo inatakiwa na kanuni. Ni kweli kwamba, kumekuwa na nafasi wazi mpaka tunaingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu na hii ilitokana na aidha, watendaji wetu katika ngazi zile kutokuwa na uelewa mkubwa wa kanuni zetu, lakini vilevile tumeshaelekeza sasa kwamba, tunacho chuo hapa cha Serikali za Mitaa cha Hombolo. Baada ya uchaguzi huu Wakurugenzi na sisi Wabunge tunaomba tushiriki kuhakikisha kwamba, viongozi wetu watakaopatikana wa vijiji, vitongoji na mitaa wapate mafunzo pamoja na watendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko sababu mbalimbali zimeainishwa ambazo Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji au Kitongoji anaweza kupoteza nafasi yake, mojawapo ni kwamba, kama Mwenyekiti kwenye Kijiji hajasoma mapato na matumizi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo inaweza ikamfanya akapoteza nafasi yake. Vilevile Mwenyekiti huyo kama atakuwa hajaitisha mikutano mara tatu mfululizo bila sababu za msingi, au inaweza ikaitishwa mikutano ya kisheria yeye Mwenyekiti asihudhurie katika hii mikutano, sababu nyingi ambazo zimetolewa ikiwepo kufukuzwa na chama au kufariki au kujiuzulu mwenyewe. Kwa hiyo, tunaomba tutoe wito kwamba, baada ya uchaguzi huu basi viongozi wetu ngazi husika hasa Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zetu na Miji watoe elimu, watoe maelekezo na Waheshimiwa Wabunge wakati wowote ikitokea nafasi wazi au ukahisi, tuwasiliane tutachukua hatua kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anazungumzia habari ya CHADEMA kujiondoa katika nafasi za kugombea. Ni kweli na sisi kama ofisi tumepata taarifa kwenye mitandao labda huenda wakatoa tamko rasmi, lakini Kauli ya Serikali ni kwamba, uchaguzi huu unaendelea kama kawaida kama ulivyopangwa kwenye ratiba. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika tarehe 24 Novemba, mwaka huu 2019, wananchi wote ambao wamejiandikisha na vyama vile ambavyo vipo kwenye mchakato waendelee na mchakato wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wametoa tamko jana kwenye mitandao, lakini itakumbukwa kwamba, kwenye taratibu zetu ni kwamba, wale ambao walikuwa na malalamiko wameandika mapingamizi yao na kesho ndio siku ya mwisho, wao jana ndio wametoa tamko. Kwa hiyo, kama wamejiondoa hawana sababu yoyote ya kulalamika kwamba, hawakutendewa haki, tulieleza tukarudia mara kadhaa kwamba, watu wenye sifa ya kutoa mapingamizi ni wale ambao ni wagombea. Wenzetu walitaka watoe kauli Bungeni, kwenye mitandao, mtaani na Serikali iamue, Serikali inafanya kazi kwa karatasi kwa mawasiliano, hatuna document mezani hatuwezi kujadili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito, yale maagizo ya kuhamasisha wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo bahati nzuri Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya kazi kubwa Watanzania wanamuunga mkono. Mwenye mamlaka ya kutoa maelekezo nchini Tanzania ni Rais wa Jamhuri ya Muungano pekee na sio kiongozi wa chama cha siasa. Kiongozi wa chama cha siasa atatoa maelekezo kwenye chama chake kwa wanachama wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, tumepata taarifa kwenye mitandao wanahamasisha watu, wanaharibu mazao ya watu na wanatishia watumishi wa umma. Wakuu wa Wilaya popote mlipo kama kuna mtu anahisi hakutendewa haki kwenye uchaguzi huu na anafanya fujo mtaani, sheria stahiki zichukue mkondo wake. Hatujawahi kutunga sheria katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema ukigombea ukinyimwa haki au ukahisi kunyimwa haki ukafanye fujo. Ukigombea ukinyimwa haki au ukahisi kunyimwa haki ziko taratibu za kisheria wazifuate, wasipofuata vyombo vya usalama vitashughulika nao na Watanzania wawe na amani, uchaguzi uko palepale, amani na tulivu, tunachapa kazi na hakuna ambaye atawaambia wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo, sisi TAMISEMI tupo pale kila mahali, ukishiriki kuhamasisha fujo na viongozi wetu wachukue taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, atakayebainika tusilaumiane mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Inapotokea Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa/Kijiji amefariki au kupoteza sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji husika huongozwa na Kaimu Mwenyekiti:- Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuwepo uchaguzi mdogo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?

Supplementary Question 2

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu Katiba inatambua uwepo wa Serikali za Mitaa na uwepo wa Serikali Kuu. Serikali za Mitaa kwa juu zinaanzia kwenye ngazi ya Halmashauri. Je, Serikali haioni kwamba, umefika wakati sasa wa kuunganisha uchaguzi wa Madiwani na uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa ili Serikali za Mitaa wafanye uchaguzi pamoja na Serikali Kuu kwa maana ya Bunge na Rais, uchaguzi wao uwe pamoja?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, hili jambo ni jambo la kisheria. Tunayo Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura Namba 287 na Sura Namba 288, lakini pia tuna uchaguzi wa Serikali Kuu, Wabunge na Madiwani na Mheshimiwa Rais; tupokee wazo hili tulifanyie kazi, ni jambo la mchakato, kama itawezekana kufanya hivyo ni jambo jema tutalifanyia kazi, lakini hili ni jambo la kisheria tunalipokea na kulifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu zetu. Ahsante.