Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vedastus Mathayo Manyinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Primary Question
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Ikiwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inawahudumia na kutatua kero za wananchi, kero hizo zisipotatuliwa katika ngazi za Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa wananchi hao hulazimika kuandika na kushika mabango kila Mheshimiwa Rais anapofika majimboni ili kupaza sauti zao:- (a) Je, ni kwa nini Viongozi wa Wilaya na Mkoa huzuia mabango hayo yasionekane na kusomwa na Mheshimiwa Rais? (b) Je, wananchi watumie njia gani kufikisha ujumbe wao kwa Mheshimiwa Rais pale matatizo yanaposhindwa kutatuliwa katika ngazi ya chini?
Supplementary Question 1
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kwa nini sasa hawa viongozi ambao mara kwa mara maana huwa tunashuhudia, kiongozi akifika mahali wanawapiga wakinyanyua mabango yao, wanapigwa, wanafukuzwa na kwa tamko hilo sasa ni kwa nini hawa viongozi wanaofanya mambo haya ya kunyanyasa wananchi wasichukuliwe hatua za kinidhamu?
Mhshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mara nyingi huu utaratibu wa kutatua kero za wananchi, unakuta hata leo mfano Waziri wa TAMISEMI akifika pale ziko kero nyingi za wananchi yeye ndio anazitatua, au Waziri wa Ardhi akifika pale zinaonekana ziko wazi ambazo labda Mkurugenzi angeweza kuzitatua, lakini ameshindwa kuzitatua mpaka kiongozi afike pale. Hali hii sasa inaonesha dhahiri kwamba, leo baadhi ya kero nyingi zinaweza kutatuliwa tu pale ambapo viongozi wa Kiserikali au viongozi wakuu wanaenda pale. Serikali inao mpango gani wa kuhakikisha kwamba, hayo matatizo yanaisha na matatizo ya wananchi yanatatuliwa kule kwenye ngazi za wilaya?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge wa Musoma Mjini, ndugu yangu, kaka yangu Vedastus Mathayo Manyinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua ni kwa nini kuna baadhi ya watu wanazuia wananchi kutoa kero zao au kuonesha mabango ambayo yamejaa hisia za changamoto zao katika maeneo yao na amesema kwamba, wanapigwa. Tunachojua ni kwamba, Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakifanya ziara wamekuwa wakiruhusu maswali kujibiwa na wananchi kutoa kero zao. Tukumbushane kwamba, pia kwenye mikutano ile ambayo kiongozi hasa Mheshimiwa Rais anapokuwepo ni mkusanyiko mkubwa sana. Sasa wakati mwingine ni watu wa usalama wanaangalia mazingira yalivyo, bahati mbaya sana yale mabango hayaratibiwi, kwa hiyo, wao wanachukua tahadhari kwanza ya kiusalama halafu wakigundua kwamba, ni ya hoja genuine, wana lengo la kupeleka kero, inaruhusiwa na wamekuwa wakifanya mara kadhaa tumeshuhudia sisi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nitoe wito kwamba, viongozi wetu hawa kwenye maeneo yetu ya mikoa na wilaya, tunao ugatuzi wa madaraka katika nchi hii kutoka ngazi ya kitongoji mpaka ngazi ya kitaifa na hii itaenda sambamba na kujibu swali lake la msingi, kimsingi Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo, tumeeleza kwamba, viongozi wetu watoke ofisini, kama ni Mkuu wa Mkoa awe na utaratibnu wa kusikiliza wananchi wake katika eneo lake husika. Kwanza akutane na Wakuu wa Wilaya kwenye mkoa wake husika na watendaji wake, anapokea changamoto katika mkoa wake, wanaweka mikakati namna ya kutatua zile changamoto, halafu badae anafanya ziara kwenda kusaidia yale ambayo yameshindikana ngazi ya wilaya wasaidiane kama mkoa kuyamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi maana yake ni kwamba, jambo ambalo lipo kwenye ngazi ya kitongoji limalizwe na viongozi wa kitongoji kwa tatizo husika. Jambo likitoka kwenye kitongoji kuja kwenye kijiji au mtaa liwe na uwezo huo walimalize, kwenye kata vivyo hivyo na kwenye ngazi ya wilaya na mkoa. Tukifanya kazi kwa pamoja kila mtu akaenda site, watu wasikilizwe, kero zitatuliwe, hakuna sababu ambayo itakuwepo tena Mheshimiwa Rais au Viongozi wa Kitaifa Mawaziri kwenda mahali mbalimbali kutatua kero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitoe wito kwa viongozi wetu kimsingi ni kuonesha kwamba, mtu huyo kwenye mkoa au kwenye kata ameshindwa kufanya kazi. Kama kuna changamoto inatolewa mbele kiongozi wa Kitaifa akiwa kwenye ziara wakati pale kuna mtu ambaye ni wa kisiasa mwakilishi, lakini pia kuna mtu ambaye ni mteuliwa wa Rais au mamlaka nyingine halafu kuna watendaji wa Serikali. Tukifanya kazi kila mtu kwa ngazi yake hii habari ya kupeana mabango wakati viongozi wamekuja haitakuwepo, tutakutana na viongozi watafanya mambo ya jumla makubwa ya Kitaifa na tutaenda na maendeleo yetu kama kawaida. Ahsante.
Name
Maryam Salum Msabaha
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Ikiwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inawahudumia na kutatua kero za wananchi, kero hizo zisipotatuliwa katika ngazi za Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa wananchi hao hulazimika kuandika na kushika mabango kila Mheshimiwa Rais anapofika majimboni ili kupaza sauti zao:- (a) Je, ni kwa nini Viongozi wa Wilaya na Mkoa huzuia mabango hayo yasionekane na kusomwa na Mheshimiwa Rais? (b) Je, wananchi watumie njia gani kufikisha ujumbe wao kwa Mheshimiwa Rais pale matatizo yanaposhindwa kutatuliwa katika ngazi ya chini?
Supplementary Question 2
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa ma-DAS na Wakuu wa Mikoa na wateuliwa wa Rais wengi wao wengine hawataki kufuata taratibu kusikiliza kero za wananchi na hata pale wananchi wengine wanapodhulumiwa haki zao hawatatui kwa wakati, mpaka wanasubiri msafara wa Rais na kwenda kulalamika mbele ya Rais wale wananchi ambao wamedhulumiwa haki zao. Je, Serikali ina mkakati gani hawa ma-DAS na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wasiowajibika katika nafasi mbalimbali walizoteuliwa ili kuwahakiki na kuchukuliwa hatua za kisheria?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na malalamiko, lakini Mheshimiwa Rais alipokuwa anahutubia katika eneo la Mbarali, Mkoani Mbeya alitoa maelekezo mahususi kwamba, kila Mkuu wa Mkoa, kila Mkuu wa Wilaya, kila mteule wa Serikali na mamlaka yake mpaka ngazi ya chini waweke ratiba ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Zile ambazo zitakuwa zimeshindikana kwenye ngazi yao wapeleke ngazi ya juu, lakini tumeenda hatua mbele zaidi tunafuatilia, Mheshimiwa Maryam na Wabunge wengine kama kuna maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ataenda au viongozi wengine watu wananyanyua mabango kulalamikia kero ambazo zipo ndani ya uwezo wa viongozi wale, hao watu ndio wanapaswa kimsingi kuondolewa katika nafasi hiyo kwa sababu, wameshindwa kutimiza wajibu wao. Ahsante.