Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stanslaus Shing'oma Mabula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Serikali imeruhusu urasimishaji wa makazi katika maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo Jiji la Mwanza isipokuwa maeneo ya Kata ya Isamilo, Mbugani, Mabatini na Igogo. Je, ni lini Serikali itawamilikisha wananchi hawa maeneo yao kwa kuwa wameishi katika maeneo haya kwa muda mrefu?
Supplementary Question 1
MHE. STANSLAUS S. MABULA:Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Naibu Waziri pamoja na Waziri kupitia Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli katika suala zima la urasimishaji makazi wamejitahidi.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu kubwa ilikuwa ni namna gani wakazi hawa walioko kwenye maeneo ya milima watapatiwa nafuu kubwa hasa angalau kwa kutambulika. Sasa niishukuru Serikali kwasababu imeliona hili na kulifanyiakazi; ni jambo jema sana na mimi nawashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaendelea na utaratibu wa urasimishaji wa makazi, na tunafahamu kwamba ili urasimishe makazi yako maeneo ambayo yalikuwa na michoro ambayo ilikuwa na maeneo mbalimbali. Kwa mfano, maeneo kwa ajili ya maziko, kwa maana ya Makaburi; Serikali ina mpango gani sasa? Maana kumekuwa na mgogoro mkubwa, kwamba eneo lilitengwa kwa ajili ya makaburi lakini linakuta wananchi wameshajenga sana kwasababu halikulindwa na badala yake wanalazimika aidha sasa tuamue wananchi waondoke tubakishe eneo kwa ajili ya makuburi au wananchi wabaki ili tutafute eneo lingine la makaburi. Maeneo ya kule Sawa, Mwalukila pamoja na Igwambiti liko tatizo la namna hii; na namshukuru Waziri amefanya jitihada kubwa amefika kule.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili; ili uweze kupima na kupanga unahitaji fedha na Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwenye halmashauri zetu kama mkopo. Sisi kama Wilaya ya Nyamagana, Jiji la Mwanza tulishaomba fedha na mikataba yote ikafungwa kwa ajili ya kupata fedha bahati mbaya sana hatujapata fedha hizi mpaka leo ni nini kauli ya Mheshimiwa Waziri? Ni lini tutapata fedha hizi hizi ili tupime na kupanga maeneo ambayo tunadhani yanaweza kuiingizia Serikali na Halmashauri mapato?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili uweze kupima na kupanga unahitaji fedha na Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwenye Halmashauri zetu kama mkopo.
Sisi kama Wilaya ya Nyamagana, Jiji la Mwanza tulishaomba fedha na mikataba yote ikafungwa kwa ajili ya kupata fedha bahati mbaya sana hatujapata fedha hizi mpaka leo. Ni nini kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba lini tutapata fedha hizi ili tupime na kupanga maeneo ambayo tunadhani yanaweza kuiingizia Serikali na Halmashauri mapato? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mabula kwa namna ambavyo amekuwa akipigania watu wake kwa ajili ya kurasimishiwa maeneo. Wote kama mnavyojua, Mji wa Mwanza umezungukwa na milima usipokuwa makini unaweza ukapata ajali kwa ajili ya watu pengine kuporomekewa mawe na kadhalika lakini amekuwa mvumilivu, amefuatilia na kuhakikisha kwamba taratibu zilizopangwa na Serikali zinafuatwa, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anazungumzia habari ya maeneo ya maziko ambayo tayari yameshavamiwa na ni kweli nilitembelea katika eneo lile nikakuta sehemu kubwa ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya maziko limevamiwa na watu. Nitoe rai kwa Halmashauri zote kusimamia maeneo haya kwa sababu tunapanga maeneo hatuyasimamii matokeo yake watu wanavamia halafu kuwatoa inakuwa ni kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo alilolisema kwenye Kata ya Sawa, kuna maeneo ambayo yako wazi kidogo ambayo hayajavamiwa na kama wako watu hawazidi watano, bado tunaweza tukafanya mabadiliko katika ramani ya eneo lile ili watu wakapangwa kwenye maeneo yale wakaendelea na maisha yao halafu sehemu ya maziko nayo ikapatikana kwa sababu huduma zote tunazihitaji. Kwa hiyo, hilo ni suala la kumuelekeza Mkurugenzi wa Mipango Miji aweze kusimamia shughuli hiyo ili upangaji ufanyike upya katika eneo lile tupate eneo la maziko na watu warasimishiwe maeneo yale waweze kuishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia suala la Halmashauri kuwezeshwa ili waweze kupata pesa za upimaji. Napenda tu nitoe taarifa kwenye Bunge lako, Wizara ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 6.2 katika Halmashauri zipatazo 24 kwa ajili ya kuwapa mkopo usio na riba ili waweze kupima na kurejesha na wengine waweze kupewa. Nasikitika kusema kati ya Halmashauri 24, ni Halmashauri tatu tu ambazo zimeanza kurejesha mikopo yake. Kati ya hizo shilingi bilioni 6.2 ni shilingi milioni 906 ndiyo zimerejeshwa ambapo Halmashauri ya Ilemela imerejesha shilingi milioni 800 kati ya shilingi bilioni 1.5 iliyopewa; Halmashauri ya Ukerewe imerejesha shilingi milioni 20 kati ya shilingi milioni 73 na Halmashauri nyingine ambazo zimepelekewa bado hazijarejesha mpaka leo.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai ili na wengine waweze kufaidika na pesa hiyo tunaomba sana Halmashauri hizi waweze kurejesha pesa hizo ili wale wengine waweze kupata. Sifa ni moja tu, ni kuandika andiko ambapo utaonesha mchanganuo mzuri namna utakavyofanya upimaji wako, utakavyolipa fidia na utakavyorejesha mkopo. Kwa hiyo, ni kitu kidogo tu watu wanafahamu wafanye kazi hiyo na Wizara itapokea lakini kwa kusubiri pesa zirejeshwe.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved