Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:- (a) Je, ni lini Benki ya FBME italipa wateja amana zao zilizokuwepo kwenye Benki hiyo? (b) Je, Benki iko katika hali gani sasa? (c) Je, Benki Kuu ya Tanzania ina dhamana gani katika kulinda Mabenki?

Supplementary Question 1

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, haya ndiyo majibu ya muda mrefu, lakini anavyoanguka ndivyo anavyochinjwa. Nami nitakuja hivyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nakupongeza na miongoni mwa Manaibu Waziri wanaopigiwa simu wewe na Atashasta Nditiye mnapokea kwa wakati tofauti na Mawaziri wengine, hilo hongereni sana. (Makofi)

Mheshiniwa Naibu Waziri, swali hili limeulizwa karibu mara tano humu ndani nikiwemo mimi mwenyewe tarehe 6 Septemba, 2018 na leo ni tarehe 12 Septemba, 2019, ni mwaka mmoja na siku kidogo. Kama mwaka mmoja hivi tulifanyiwa semina hapa Ukumbi wa Msekwa, walikuja Ma-deputy governor karibu watano, Wakurugenzi na Watendaji na niliuliza swali hili, wakasema hizi fedha ziko Dutch Bank zitaletwa muda siyo mrefu. Sasa swali langu ni: Je, tokea muda huo zinaletwa kwa baiskeli ama kwa mguu? Maana ni muda mrefu hazijafika. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi juzi hawa jamaa walishinda kesi yao huko Uingereza: Je, ni kweli na kwamba waliambiwa waliofungua kesi hiyo walipe gharama za kesi? Ni kweli wameshinda kesi? Kama wameshinda, ni hatua gani zinazofuata? Wengine tukumbuke Mheshimiwa Naibu Waziri, cheo ni dhamana…

SPIKA: Maswali yasiwe mengi, nataka maswali mawili tu Mheshimiwa Jaku.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza, amekuwa mfuatiliaji mzuri sana tangu benki hii ilipofutiwa usajili wake hapa nchini akifuatilia amana za wateja ili waweze kulipwa. Kwa dhamira njema na nia njema ya Serikali yetu, ndiyo kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa shilingi milioni 1.5 wateja ambao walikuwa na amana hiyo ndani ya benki, yatari tumeshalipa zaidi ya asilimia 83 ya wateja wote. Asilimia 17 iliyobaki ni wateja ambao hawajajitokeza wao wenyewe kuja kuchukua amana zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba dhamira ya Serikali yetu ni njema na ndiyo maana tumeanza kulipa hawa wateja wote ambao walikuwa na fedha zao ambazo hazizidi shilingi milioni 1.5 kama sheria inavyotuelekeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza naomba niyajibu yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza fedha hizi hazitakuja kwa baiskeli, wala kwa gari, wala kwa meli, ila ni taratibu za kisheria zitakapokalimika. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha amana za wateja wetu wote ambao wako ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania zinabaki kuwa salama na wanazipata pale ambapo tumemaliza majadiliano na Benki Kuu ya Cyprus.

Mheshimiwa Spika, tayari mwezi wa Tisa baada ya Mahakama za nchini Cyprus kurejea na kuanza kufanyakazi yao, kesi zote zilizokuwa zimefunguliwa, tumekubaliana zitafutwa na tayari sasa fedha hizo zitafika ndani ya nchi yetu na watu wetu wote wataweza kulipwa fedha zao.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba tu nitoe majibu ya nyongeza kwa swali la nyongeza alilouliza Mheshimiwa Mbunge na hasa kuhusu ile kesi ya Uingereza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wamiliki wa iliyokuwa Benki ya FBME walifungua kesi Uingereza. Lakini lengo la kesi ile ilikuwa ni ku-challenge mwenendo wa mchunguzi aliyekuwa anachunguza masuala ya FBME kule Uingereza, ni kweli kwamba Mahakama kule imetoa hukumu yake lakini kwa namna yoyote hukumu au matokeo ya kesi ile haiathiri suala zima la liquidation ya ile benki huku. Kwa maneno mengine, hukumu ile haina athari yoyote wala haigusi jambo lolote katika mchakato unaoendelea kwa upande wa Tanzania na Cyprus.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:- (a) Je, ni lini Benki ya FBME italipa wateja amana zao zilizokuwepo kwenye Benki hiyo? (b) Je, Benki iko katika hali gani sasa? (c) Je, Benki Kuu ya Tanzania ina dhamana gani katika kulinda Mabenki?

Supplementary Question 2

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa benki hii ilikuwa na matawi Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, na kwa kuwa benki hii ilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 100 na familia hizo na wafanyakazi hao mpaka sasa hawajui hatma yao, familia hizo zinateseka kulipa ada, kulisha ndugu na kadhalika.

Je, ni lini sasa wafanyakazi hao watafahamishwa hatima yao kwa sababu pia hawawezi hata kwenda kuomba kazi mahali pengine popote?(Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye majibu ya msingi na majibu ya nyongeza ambayo nimemjibu Mheshimiwa Jaku Hashim, baada ya kuwa tumemaliza majadiliano na Benki Kuu ya Cyprus na kuingia sasa kwenye mchakato wa kuhakikisha kila mwenye haki yake anapata haki yake ni imani yangu na wafanyakazi hao wa iliyokuwa Benki ya FBME Limited watapata haki yao, nimesema wazi mwezi wa Septemba, baada ya Mahakama za nchini Cyprus kurejea kazini basi yote hayo yatajulikana na kila mmoja atapaa haki yake na kwa wafanyakazi kwa sababu waliajiriwa na Benki hii ambayo ilikuwa na Makao Mkuu hapa nchini, basi sheria zetu za kazi na ajira zitatumika ili kila mtumishi aweze kupata haki yake.(Makofi)