Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Busanda
Primary Question
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 1
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais alipokuja Geita aliweza kunipatia Hospitali ya Wilaya itakayojengwa Kata ya Buseresere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, naipongeza Serikali kwamba imekusudia kuajiri watumishi 550 lakini kwa kuwa Halmashauri ya Geita tuna upungufu mkubwa sana tungependa kujua ni lini sasa hao watumishi wataletwa ili waweze kuanza kufanya kazi katika Halmashauri ya Geita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika Jimbo la Busanda kuna vituo vya kutolea huduma viwili ambavyo vimekamilika kabisa, vinatakiwa tu kufunguliwa, Buziba pamoja na Magenge. Napenda kupata kauli ya Serikali ni lini sasa watahakikisha vituo hivi vimefunguliwa kwa sababu vimekamilika kabisa?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali, naomba nipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anauliza ni lini watumishi watapelekwa ili kuweza kuziba pengo la upungufu huo mkubwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mchakato uko kwenye hatua za mwisho kabisa kwa sababu katika suala la kuajiri lazima taratibu zote zifuatwe. Namwondoa mashaka muda si mrefu watumishi wataweza kupelekwa huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea vituo vyake vya afya viwili ambavyo tayari vimeshakamilika, anachotaka kujua ni lini vituo hivyo vitafunguliwa. Kama azma ya Serikali ilivyo kwamba vituo vile vya afya vinajengwa ili vianze kutoa huduma, sina uhakika kama tayari kama vifaa vyote vilishapelekwa. Kama vifaa vilishapelekwa ni jambo jema kinachotakiwa ni kupeleka watumishi ili vituo hivyo vifunguliwe vianze kutoa huduma. Ndiyo makusudi ya Serikali na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na matatizo makubwa ya kijiografia yaliyoko katika Visiwa vya Ukerewe yanayoathiri utoaji wa huduma za afya lakini tuna madaktari 3 pekee kati ya 10 wanaotakiwa, tuna waganga wasaidizi 5 pekee kati ya 43 wanaotakiwa na tuna wauguzi 80 pekee kati ya 289 wanaotakiwa. Nini kauli ya Serikali wanayoweza kuwaambia wananchi wa Ukerewe juu ya kuboresha huduma za afya kwa kutoa wahudumu wa afya kiasi kinachotakiwa?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana upungufu mkubwa wa watumishi, wakati tunaajiri hao 550 tutazingatia. Naamini na Ukerewe nao hatutawasahau, ipo nia kubwa kuhakikisha kwamba tunapunguza hilo pengo la upungufu wa watumishi. Naomba nimhakikishie Mbunge tutazingatia katika mgao.
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki Serikali imefanya jitihada kubwa sana za kujenga hospitali, vituo vya afya, zahanati na kadhalika. Kwa hili kama Kambi Rasmi ya Upinzani tulivyosema jambo zuri lazima tulipongeze, kwa hiyo, napongeza sana jitihada hizi ambazo zimefanyika katika kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tumetatua tatizo moja tumekaribisha tatizo lingine. Watumishi katika sekta hii ya afya ni wachache sana. Katika jimbo langu kwa mfano kuna upungufu wa asilimia 52 ya madaktari na wahudumu wengine katika sekta mbalimbali za afya. Nataka Serikali itueleze mkakati ambao utakwenda sambamba na ongezeko hili la hospitali na vituo vya afya ili sasa wananchi wapate ile huduma ambayo Serikali imekusudia waipate na ambayo ni haki yao?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba kupokea pongezi kutoka kwa Kambi Rasmi, ni jambo ambalo limekuwa likifanyika mara chache sana. Sasa ikitokea ni wajibu na sisi tu-recognize hiki ambacho kimefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma za afya zinasogezwa jirani na wananchi. Ni ukweli usiopingika kwamba sasa hivi wananchi wengi wanavutiwa kwenda kupata huduma kwenye vituo vyetu vya Serikali tofauti na vile vya mashirika ya watu binafsi na dini. Naomba nimhikishie Mheshimiwa Mbunge hao watumishi 550 ambao tutakuwa tumewaajiri na kuwasambaza hivi karibuni ni mchakato wa kuendelea kuajiri na wengine kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu ili tupunguze adha ya mwananchi kupata huduma kwa urahisi ikiwepo ni pamoja na Rombo ambayo wana Mbunge ambaye ni makini ameweza ku-recognize kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved