Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?

Supplementary Question 1

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Nataka kufahamu pia kuhusiana na mgogoro wa wafanyakazi uliopo katika Hospitali ya Ndanda. Serikali iliahidi itaajiri wafanyakazi 85 na wale Wamisionari sasa hivi wameamua kupunguza wafanyakazi 59 kwa sababu Serikali haijatekeleza ahadi yake toka mwaka 2012 hali inayotishia kuifanya Hospitali ya Ndanda isiwe tena Hospitali ya Rufaa katika eneo la Kusini. Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kutekeleza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya wafanyakazi wa Ndanda Hospitali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu pia ni lini Serikali italipa pesa za fidia katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwa vile katika vitu vilivyoharibika ni pamoja na gari la wagonjwa la hospitali ya Chiwale ili waweze kujinunulia wenyewe tena lile gari liweze kusaidia baada ya kujenga wodi ya akinamama katika eneo lile? Ahsante

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la changamoto ya watumishi ni kwamba Serikali tumelichukua. Sasa hivi tuna mchakato wa kuajiri watumishi mbalimbali katika Halmashauri zetu na Wizara ya Afya ina-finalize stage hiyo. Nina imani kwamba siyo muda mrefu ndani ya mwezi huu wa Mei na Juni tutaenda kupunguza hii gape ya watumishi, lakini changamoto ya Ndanda tutakwenda kuifanyia kazi. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kulifanyia kazi kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ambulance zilizoungua, ni kweli na mimi mwenyewe nimefika pale. Pale kuna ambulance tatu zilichomwa moto na kwa njia moja au nyingine siyo kwamba Serikali ni ya kulaumiwa. Katika hili, naomba nitoe maelekezo kwa wananchi, inawezekana kwa jazba zetu tunaharibu vitu ambavyo vilikuwa kwa maslahi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi kile pale Mtwara watu walienda kuchoma ambulance ambazo zinabeba akinamama na watoto. Fikiria mtu anachukua kibiriti na petrol anakwenda kuchoma ambulance tatu mpya, unategemea nini katika mazingira hayo? Kwa kweli ni jambo lenye kuhuzunisha na ndiyo maana nilipofika pale Masasi nilienda kutembelea maeneo yake, kwa kweli ni jambo la kuhuzunisha, lakini Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa sababu mwisho wa siku ni wananchi na akinamama ndiyo wanaopata shida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalichukua hili kwa upana wake lakini kwa kweli kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumesikitika sana kwa sababu ile ni fursa ambapo wananchi walikuwa wanapata huduma kila siku. Naomba nitoe onyo kwa watu wote, tusichukue jazba zetu mbalimbali tukazielekeza katika vitu ambavyo vinawasaidia wana jamii kupata huduma bora katika maisha yao.

Name

Grace Sindato Kiwelu

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?

Supplementary Question 2

MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kuuliza ni lini wodi ya wazazi katika Hospitali yetu ya Mkoa ya Mawenzi itakamilika kwa sababu imejengwa kwa zaidi ya miaka mitano na inakuwa ni kero kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukamilika kwa wodi ya wazazi katika hospitali ya Mawenzi, Moshi ni suala la kipaumbele kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. Wiki takribani tatu zilizopita nilifika pale na kuona hatua ya ujenzi iliyofikiwa na tukashauriana na uongozi wa hospitali ile na kukubaliana kwamba kwa mwaka huu wa fedha waombe wapewe bajeti maalum kwa ajili ya kukamilisha sehemu ya jengo hilo ambayo itatoa huduma kwa akina mama wajawazito na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile watumie mikopo inayopatikana kwenye taasisi mbalimbali za kifedha ili wakamilishe ujenzi huo mara moja sasa hivi kuliko kusubiria huu utaratibu wa kutumia bajeti. Tayari wameanza mchakato huo kupitia Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Said Meck Sadick kwa kufanya mazungumzo na Benki ya TIB.

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?

Supplementary Question 3

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri zinatofautiana kimapato na Kituo cha Afya cha Nyambiti hakina gari, ni utaratibu gani sasa utumike ili kituo hiki kiweze kupata gari kwa sababu uwezo ni mdogo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la upatikanaji wa gari katika vituo vya afya, tulipokuwa tunapitia mchakato wa bajeti yetu ya mwaka huu 2016/2017, tulikuwa tukifanya analysis ya halmashauri mbalimbali katika suala zima la sekta ya afya, kila halmashauri iliweka kipaumbele chake. Kuna wengine waliweka kipaumbele cha ujenzi wa miundombinu, kwa mfano kwa ndugu yangu pale zahanati aliyosema ya Chiwale, wametenga karibuni milioni 287 kwa ajili ya kituo kile cha afya. Wengine kipaumbele chao walichoweka ni ununuzi wa gari la wagonjwa. Kwa hiyo, vipaumbele hivi vinatofautiana kati ya zahanati na zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Ndassa kwa sababu sijajua kipaumbele walichoweka katika eneo hili, sisi na wenzetu wa Wizara ya Afya tutaangalia katika bajeti ya mwaka huu tumegusa vipi katika eneo hilo. Mwisho wa siku ni kwamba, lazima kwa umoja wetu wote tuangalie jinsi gani tutafanya maeneo kama hayo ambayo wananchi wanapata shida waweze kupata fursa za kuwa na gari la wagonjwa ili mama akipata matatizo aweze kupelekwa hospitali ya karibu kupata huduma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndassa naomba tulichukue hili tujadiliane kwa pamoja na kuangalia bajeti yenu ya halmashauri mlipanga vipi kama vipaumbele vyenu vya awali.