Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Upendo Furaha Peneza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Wananchi wa Mtaa wa Mgusu wanaoishi ndani ya mipaka ya Mgodi wa Geita Gold Mine wanaathirika sana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka zinazomwagwa katika maeneo karibu na wananchi. Je, ni lini Serikali itatoa agizo kwa Geita Gold Mine kulipa wananchi fidia ili watoke katika eneo lililomilikishwa Mgodi?
Supplementary Question 1
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa bahati mbaya swali langu lilinukuliwa tofauti na nilivyowasilisha. Lakini kwa faida ya wananchi wa Nyakabale ninaomba kujua kwamba sehemu ya Nyakabale ni eneo limekuwa likipata shida kubwa kutokana na mgodi wa Geita Gold Mine kwa maana ya kimatatizo ya kimazingira lakini hata wananchi wenyewe kuzuia kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya kwamba itabidi wapishe shughuli za mgodi.
Mheshimiwa Spika, lakini ni miaka sasa hawawaondoi katika eneo hilo. Sasa ninaomba kujua tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Kalemani kwamba wale wananchi wangeondolewa lakini mpaka leo hawajaondolewa. Je, Serikali inatupa leo kauli gani wananchi wa Geita hasa wananchi wa Nyakabale kuhusu kulipwa fidia ama kuruhusiwa kwamba waendelee na shughuli zao za kimaendeleo katika eneo hilo la Nyakabale?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili linahusu katika upande huo wa ulipwaji fidia, sheria yetu imeruhusu haya makampuni kuweza kutumia wathamini binafsi kwenda kuhesabu mali za wananchi na hatimaye kuweza kulipwa na hili limeleta malalamiko kwa maana ya wananchi wengine kuona kwamba wanapunjwa na kampuni hizo kutetea maslahi zaidi za makampuni hayo ya uwekezaji. Sasa Je, Serikali leo inatoa kauli gani kuhakikisha ya kwamba maslahi ya wananchi katika maeneo husika yanalindwa ahsante? (Makofi)
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Nyakabale yako ndani ya leseni ya uchimbaji yaani leseni ambayo ni special mining license ya mgodi huu wa GGM ndani ya zile kilomita 290 za mgodi huo.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba sheria inasema kwamba ni lazima mtu ambaye anataka kuwekeza kuchimba maeneo yale watu wanaoishi maeneo yale ni lazima awalipe fidia waondoke ili aweze kufanya operation zake.
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la Nyakabale liko nyuma ya mgodi huo na kweli kuna wakati fulani mimi mwenyewe niliweza kutembelea pale nikakuta kuna maeneo mengine ambayo wananchi walizuiliwa wasiendeleze yale maeneo yao au wasiendelee kujenga kwa sababu wako ndani ya leseni na mimi niliweza kuwapa nilitoa tamko kwa mgodi kwamba wawalipe wananchi hao na kuondoka kama wananchi hao wanaathirika na uchimbaji huo. Lakini vilevile ni kwamba mgodi walisema wako tayari wataweza kuwaondoa wale wote ambao wanaonekana wanaathirika na shughuli za mgodi.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika swali la pili kuhusu fidia ya yale maeneo ambayo yanazunguka mgodi ambayo yapo karibu na Mji wa Geita hapa tunavyozungumza ni kwamba uthaminishaji ulikuwa unaendelea na uthaminishaji ule ulikuwa unafanywa na kampuni binafsi lakini chini ya usimamizi wa Chef Valuer wa Serikali ambapo mpaka sasa hivi tumekwishakuona kwamba ni watu wangapi ambao wanatakiwa walipwe uthaminishaji umeshakubaliana waliothaminiwa na wathaminishaji wote wameshakubaliana na toka Jumatatu tayari fidia hizo zimeanza kulipwa na kampuni ahsante sana. (Makofi)
Name
Goodluck Asaph Mlinga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulanga
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Wananchi wa Mtaa wa Mgusu wanaoishi ndani ya mipaka ya Mgodi wa Geita Gold Mine wanaathirika sana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka zinazomwagwa katika maeneo karibu na wananchi. Je, ni lini Serikali itatoa agizo kwa Geita Gold Mine kulipa wananchi fidia ili watoke katika eneo lililomilikishwa Mgodi?
Supplementary Question 2
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante wananchi wangu wa Epanko tangu wafanyiwe tathimini ni miaka miwili mpaka sasa hivi hawajalipwa, na Mheshimiwa Waziri alishafika huko na anajua shida, sasa sheria inasema mtu akifanyiwa uthamini baada ya miezi sita anatakiwa alipwe na ikizidi hapo analipwa fidia na uthamini ukizidi miaka miwili unakuwa cancelled unafanywa upya, nataka kusikia kauli Serikali. Je, hawa wananchi waliofanyiwa uthamini wao lini watalipwa ni miaka miwili imeshapita?
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli uzuri kwenye sheria ya uthaminishaji na kulipa fidia iko wazi tunataka makampuni yote yakishafanya uthamini walipe ndani ya muda uliokubaliwa, mtu ambaye hatalipa ndani ya miezi sita sheria inasema atalipa lakini atalipa na interest yaani kwa maana ya usumbufu na asipolipa ndani ya miaka miwili, sheria inasema kwamba tayari ule uthaminishaji una- expire kwa mujibu wa sheria kwa hiyo ni lazima mrudi mfanye uthaminishaji upya.
Mheshimiwa Spika, nipende kutoa tu wito kwa makampuni yote walipe kwa muda ambao umepangwa wasipofanya hivyo inaleta mtafaruku, mfano mzuri uko kule Mara Tarime, kuna watu ambao hawakulipwa ndani ya muda matokeo yalivyokuja kuonekana ni kwamba sasa wale wenye zile nyumba waliona kwamba baadaye wataonekana watakuja kuondolewa wakawa wanajenga nyumba za kutegesha, nyumba za gharama nafuu ili waje walipwe fedha nyingi. Sasa hii imetokea maeneo mengi, kwa hiyo tunaomba sana makampuni yote tunawahasa mkishafanya uthaminishaji lipeni kadri ya sheria inavyosema usipofanya hivyo inaleta mtafaruku. Nashukuru sana. (Makofi)
Name
John Wegesa Heche
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Wananchi wa Mtaa wa Mgusu wanaoishi ndani ya mipaka ya Mgodi wa Geita Gold Mine wanaathirika sana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka zinazomwagwa katika maeneo karibu na wananchi. Je, ni lini Serikali itatoa agizo kwa Geita Gold Mine kulipa wananchi fidia ili watoke katika eneo lililomilikishwa Mgodi?
Supplementary Question 3
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge na awaambie Watanzania kwa mujibu wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 kampuni inatakiwa kulipa fidia ifanye relocation na ifanye resettlement kama inahamisha watu. Lakini hawajawahi kuhamisha mtu wala kumfanyia relocation na licha ya hivyo mpaka sasa kwa mfano wananchi wa Tarime waliofanyiwa uthamini maeneo ya Nyamongo kuanzia mwaka 2009 mpaka leo tunavyozungumza hawajawahi kulipwa. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Madini alikuwa pale ametoa kauli lakini mgodi unakiuka hausikilizi, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri ni lini hasa watu hawa wanaoendelea kuteseka kwa zaidi ya miaka 10 au 15 watalipwa sasa ahsante? (Makofi)
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Heche Mbunge wa Tarime kwa kifupi tu na kwa sababu leo ni bajeti yetu tutaeleza kwa kina hayo yote.
Mheshimiwa Spika, nieleze kwamba ni kweli kulikuwa na changamoto ya muda mrefu toka mwaka 2012 kwenye fidia za maeneo ya mgodi wa North Mara huko Nyamongo. Lakini kama Serikali tumechukua hatua kubwa sana kwa sababu kuna maeneo mengine ambapo kwa kweli tungekimbilia tu wananchi walipwe fidia walikuwa wamepunjwa sana, kwa mfano awamu ya 47 wananchi 66 ambao walikuwa wanadai fedha walithaminiwa kiasi cha shilingi milioni 224 peke yake, tumekwenda kule tumeangalia tumekuta wale wananchi walikuwa wamepunjwa sana tumeagiza uthamini huo ufanyike upya ili wananchi walipwe stahiki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Heche anafahamu Awamu ya 24 na Awamu ya 34 wananchi hawa walikwenda mahakamani na kwa kuwa wamekwenda mahakamani tuliwashauri kwamba wamalize shauri lao mahakamani wakishakumaliza sisi kama Serikali huku tutasimamia utaratibu wao wa kulipwa. Lakini Awamu ya 30, 32 (a) na (b) ambazo mgodi hauhitaji hayo maeneo Chief Valuer ameelekeza mgodi uwalipe kifuta jasho wananchi hao.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Heche kwamba jambo hili tumelifanya pamoja na kwenye bajeti tutalieleza kwa kina awe na subira tusiharakishe shughuli za Bunge ahsante. (Makofi)