Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustino Manyanda Masele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kata za Bujula, Nyamalimbe, Kamena, Nyalwanzaka, Nyakamwaga, Busanda Kaseme, Magenge, Butindwe na Nyaruyeye?

Supplementary Question 1

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kwamba, mkandarasi wa Awamu hii ya III wa REA katika Mkoa wa Geita anaonekana anaenda anasuasua katika utekelezaji wake. Sasa ni nini hatua zinazochukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, maeneo ya utekelezaji wa mradi huu REA III unakamilika kwa mujibu wa ratiba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Wilaya ya Mbogwe kuna vijiji vilivyoachwa kwenye Awamu hii ya REA Phase III ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, vijiji vyote vya Wilaya ya Mbogwe vinapatiwa nishati hii ya umeme? Ahsante.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Masele, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya mzingi:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Masele katika kuliza swali la msingi. Kwanza ni kweli Jimbo la Mbogwe lina vijiji 86 na kati ya vijiji hivyo ni vijiji 23 havijapata umeme, ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonze. Lakini pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Masele na ufuatiliaji wake Kata Mpya ya Nyabunigonza ambayo inapitia Kijiji cha Lunguya kwenda Kijiji cha Chibutwe, umbali wa kilomate mbili na iko katikati imeshaanza kushushiwa umeme tangu jana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba, kata nzima na vijiji vyake vitano itapelekewa umeme kuanzia mwezi huu hadi mwezi Septemba mwaka huu.

Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, nimefuatilia kazi hizi na kumpongeza sana kwenye wilaya yake itabakiza vijiji vitano ambavyo tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia mwezi ujao na vitakamilika mwezi Disemba mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini mkandarasi, White City, atamaliza kazi katika Mkoa mzima wa Geita:-

Mheshimiwa Spika, kwanza mkandarasi huyu ameshafikia average ya asilimia 52 na muda wake wa kumaliza kazi kimsingi ni mwezi Juni mwakani, lakini tunamtaka amalize kazi mwezi Disemba mwaka huu, ilibaki kazi ndogondogo za kuunga wateja, hasa ambao watachelewa kulipa. Kwa hiyo, nimpe taarifa na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maendeleo ya mkandarasi katika Mkoa mzima wa Geita, lakini nimhakikishie kwamba, utakamilika ndani ya muda. (Makofi)

Name

Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kata za Bujula, Nyamalimbe, Kamena, Nyalwanzaka, Nyakamwaga, Busanda Kaseme, Magenge, Butindwe na Nyaruyeye?

Supplementary Question 2

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nashukuru sana:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ile ya Awamu ya Pili ilipeleka umeme katika Mji Mdogo wa Laela, lakini haikushusha umeme katika sekondari ya Lusaka na Sekondari ya Kaengesa. Je, ni lini Serikali itashusha umeme katika sekondari hizo?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Malocha amejielekeza kwenye utekelezaji wa REA II ambapo Mji wa Raela nao ulifikiwa, lakini ameeleza Sekondari za Kaengesa kwamba, hazijapatiwa umeme. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri, tuliambatana kwenye ziara katika jimbo lake mpaka Kilyamatundu, lakini tulitoa maelekezo kwamba, Mradi wa Ujazilizi Awamu ya II ambao unaanza tarehe 01Julai, 2019 na tuko hatua za mwisho za kuwapata wakandarasi maeneo ya Raela na hususan vitongoji ambavyo havijafikiwa na hizi sekondari.

Mheshimiwa Spika, namuagiza Meneja TANESCO wa Mkoa ahakikishe maeneo haya yanaingizwa kwenye Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili, ili waendelee kusambaziwa umeme na maeneo menginebya taasisi za umma katika Mkoa wa Rukwa kwa kuwa upo katika orodha ya mikoa 26 ambayo itafikiwa na Mradi wa Ujazilizi Awamu ya II. Ahsante sana.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kata za Bujula, Nyamalimbe, Kamena, Nyalwanzaka, Nyakamwaga, Busanda Kaseme, Magenge, Butindwe na Nyaruyeye?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa jinsi Waziri na Naibu wake wanavyojibu haya maswali inaonekana kwamba, kazi yao ni nzuri, wanazunguka sana kwenye hii nchi na wana data za kutosha. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa katika Jimbo la Rombo kuna Kata za Reha, Nanjara, Kitirima, Mraokerio, Kwandele, ambazo vijiji kadhaa bado havijapata huduma ya umeme na mradi wa ujazilizi bado haujaanza kufanya kazi vizuri. Je, ni lini kata hizi na vijiji vyake sasa mradi wa kuwapelekea umeme utakamilika? Asante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana na yeye pia kwenye jimbo lake tumewahi kufanya ziara, lakini kwa kweli, nikiri katika Mkoa wa Kilimanjaro kulikuwa na changamoto ya utekelezaji wa mradi wa REA II na Serikali ilichukua hatua na ikaitangaza ile kazi tena na mkandarasi yuko site anaendelea. Katika maeneo aliyoyataja ikiwemo Kata ya Nachara na vijiji ambavyo havijapatiwa miundombinu ya umeme Mheshimiwa Mbunge ameulizia masuala ya mradi wa ujazilizi:-

Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa 9 ya ujazilizi ambayo itapata mradi wa ujazilizi Awamu ya II, mzunguko wa kwanza. Kwa hiyo, nataka nimtaarifu kwa kweli, vitongoji vyote vilivyosalia katika Mkoa wa Kilimanjaro vitapate umeme na huo mradi kama nilivyosema kwenye maswali ya awali kwamba, uko hatua za kuwapata wakandarasi. Ahsante sana.