Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zainab Mndolwa Amir
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ZAINAB M. AMIR aliuliza:- Wananchi wengi wamejenga makazi yao bila kuzingatia mipangomiji na matokeo yake kuvunjwa nyumba zao bila kupata fidia pindi Serikali inapoanza ujenzi unaozingatia mipangomiji:-. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wananchi elimu stahiki ili waepukane na adha hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina maswali madogo ya nyongeza; kuna baadhi ya watu wanajenga katika mabonde na wengine wanajenga katika hifadhi za barabara na pia karibu kabisa na njia za reli lakini Serikali yetu kupitia halmashauri zetu kila mwaka hukusanya kodi za majengo na kodi za ardhi katika maeneo hayo. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kadhia hii?
Mheshimiwa Spika, Swali langu la pili ili mwananchi aweze kujenga katika eneo husika ni lazima apate kibali kutoka katika mamlaka na sasa nauliza swali langu. Je, ni nini adhabu ambazo wanapewa watendaji ambao wanatoa vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi? Ahsante sana. (Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli wako watu ambao wamejenga katika hifadhi za barabara, hifadhi za miundombinu mbalimbali na mabondeni lakini wamefanya hivyo kinyume cha sheria na Serikali hairuhusu na hata zoezi la urasimishaji na utoaji wa leseni za makazi hautafanyika wala hatutarasimisha makazi kwa watu ambao wamejenga katika maeneo hatarishi na maeneo ambayo yamepangwa na wapangamiji kama maeneo ya hifadhi ya barabara au maeneo ya miundombinu. Kwa hilo nakiri ni kosa wako watu wamefanya namna hiyo na sheria lazima ichukue mkondo wake kwa sababu ya kuwasaidia wao lakini kusaidia maendeleo ya miji yetu.
Mheshimiwa Spika, pia ni kweli kwamba kodi inakusanywa kwa sababu hawa watu lazima walipe kodi, kuishi kwao kule wanatumia rasilimali za Halmashauri husika, kwa hiyo halmashauri zile zinapaswa kuwatoza kodi katika maeneo yale kwa sababu na wenyewe wanatumia rasilimali na infrastructure zilizoko kule lazima wachangie, Hilo linafanyika na ni kweli lazima watoe kodi, lakini ujenzi katika maeneo hayo hairuhusiwi. Kwa hiyo huwezi kujenga tu eti kwa sababu unataka kukaa mabondeni halafu usitozwe kodi kama wanavyotozwa Watanzania wengine. Ni kweli kodi za majengo zitatozwa na kodi mbalimbali za halmashauri wanazotoza raia wengine zitazozwa, lakini hiyo haihalalishi kwamba wewe hapo umekaa kihalali. Lolote likitokea linaweza likatokea kama wapangaji na halmashauri husika wakiamua kuchukua hatua za kisheria.
Mheshimiwa Spika, la pili vibali vya ujenzi zamani vilikuwa vinatolewa zamani vilikuwa vinatolewa na Kamati ya Mipangomiji ya Madiwani lakini sasa utaratibu Serikali ya Awamu ya Tano imebadilisha kwa sababu ilikuwa inachelewesha sana na ilikuwa inachukua gharama kubwa sana, inamaliza hela nyingi kwa ajili ya posho ya vikao na kila kitu. Sasa hivi iko timu ya wataalam tu wa Serikali ambao ndiyo wanatoa vibali vya ujenzi na tumesema vibali visichukue zaidi ya siku tatu viwe vimeshatoka, kwa sababu watu wako pale wana uwezo wa kwenda kufanya ukaguzi na ni wataalam waliobobea katika kazi hiyo na vibali vya ujenzi lazima zitolewe. Kwa hiyo vibali sasa vinatolewa kwa kasi na hii imesababisha kupunguza hata gharama kwa wananchi za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba siku za nyuma ilionekana kwamba watu waliweza kutoa vibali hata kwa watu ambao wametakiwa kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa. Serikali kwa wakati tofauti imechukua hatua kali na wengine wameachishwa kazi kwa wale ambao wametoa vibali katika maeneo ambayo hayastahili. Kwa hiyo Serikali imekuwa inachukua hatua za kinidhamu mara kwa mara, lakini nataka kumhakikishia katika Awamu hii ya Tano hilo halifanyiki. Awamu ya Tano imejenga nidhamu tofauti, watu ni wale wale lakini nidhamu yao imekuwa tofauti, hawatoi vibali tena hovyo hovyo na hawatatoa tena vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi.
Name
Joram Ismael Hongoli
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. ZAINAB M. AMIR aliuliza:- Wananchi wengi wamejenga makazi yao bila kuzingatia mipangomiji na matokeo yake kuvunjwa nyumba zao bila kupata fidia pindi Serikali inapoanza ujenzi unaozingatia mipangomiji:-. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wananchi elimu stahiki ili waepukane na adha hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la makazi holela sehemu nyingi linasababishwa na kukosa wataalam wa kupanga, kupima na hatimaye kutoa hati. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe hatuna Afisa Ardhi wala hatuna Afisa Mpima, tuliyenaye pale ni afisa tu ni kama technician. Je ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Njombe itapata Afisa Ardhi ili aweze kutusaidia katika kupanga na kupima na baadaye kutoa hati? (Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mbunge wa Njombe la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maswali haya bila shaka yananipunguzia muda wa kujadili kesho pengine utapungua utakuwa siku moja, maana ni haya haya ambayo nitasema kesho.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama ulivyosema mwenye tunao upungufu wa Maafisa Ardhi na katika speech yangu nimetoa uwiano ikama inasema nini lakini tulionao ni wangapi. Nataka kukuhakikishia zoezi hili litapunguza makali kidogo mwezi wa Saba ambapo Wizara yangu sasa itaanza kupanga upya hawa maafisa, wanahamishwa na kupangwa na Wizara yangu, kwa sababu tumegundua siyo kwamba ikama ilikuwa inasababisha lakini upangaji ulikuwa hauzingatii mahitaji. Ukienda Mkoa wa Mwanza kwa mfano Wilaya za Nyamagana na Ilemela unakuta kuna Maafisa Ardhi themanini lakini Njombe hakuna hata mtu mmoja. Kwa sababu tatizo ni kwamba wale wapangaji pengine pale walipokuwa wanasimamiwa hawakuwa na fani zinazofanana nao, kwa hiyo walikuwa hawajui fani gani ipangwe namna gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka niwahakikishie Wabunge wote mwezi wa Saba tutawapanga hawa hawa wachache, lakini tutajitahidi angalau kila wilaya iwe na afisa angalau wa taaluma moja ya ardhi aweze kuwepo. Nazijua baadhi ya wilaya ambazo hazina hata mtu mmoja wa sekta nzima ya ardhi ambayo ina vitengo vitano, hawawezi kufanya shughuli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi lako tutalitekeleza mwezi wa Saba na la Waheshimiwa Wabunge, tutawapanga upya na Njombe, tatizo la Njombe Afisa Ardhi alikuwa mtendaji mzuri sana nimempandisha cheo amekuwa Kamishna Msaidizi. Kwa hiyo nitampelekea mtu mwingine baada ya hapo na Waheshimiwa Wabunge wote wenye swali kama hili watusubiri mwezi wa Saba Mungu akipenda tumeamua kuwapanga upya, nitawaita hapa kwanza niwaelekeze lakini tutawapanga upya ili angalau kila wilaya tuwe na afisa anayeweza kufanya kazi fulani.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ZAINAB M. AMIR aliuliza:- Wananchi wengi wamejenga makazi yao bila kuzingatia mipangomiji na matokeo yake kuvunjwa nyumba zao bila kupata fidia pindi Serikali inapoanza ujenzi unaozingatia mipangomiji:-. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wananchi elimu stahiki ili waepukane na adha hiyo?
Supplementary Question 3
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi tunajua moja ya Serikali kuwa na mikakati ya mipango bora ya ardhi ni pamoja na kuzuia watu kujenga mabondeni na pamoja kwenye mikondo ya mito na Serikali ilianzisha operesheni ya kubomoa nyumba za watu ambao wamejenga kwenye mikondo ya mito na hili ni tangu Bunge lililopita Mheshimiwa Lukuvi nadhani analijua na amebomoa nyumba nyingi tu kule Kawe lakini kuna nyumba ya kigogo mmoja tu ameiacha na wamekuwa wakitoa ahadi humu ndani hiyo nyumba itabomolewa. Nataka kujua ni lini ile nyumba itabomolewa?
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inachukua hatua za mara kwa mara na nikisema Serikali maana yake kwa umoja wetu na wasimamizi wa sheria zote za mipangomiji ni mamlaka ya upangaji ambayo ni halmashauri yenyewe. Ukisikia operesheni ya vunja vunja au kuondoa watu waliojenga kinyume cha sheria katika halmashauri fulani, ujue inaendeshwa na halmashauri ambayo ndiyo yenye mamlaka na hata ile enviction order ya kwenda kuwavunjia haitolewi na Wizara yangu, hapana inatolewa na Afisa Ujenzi wa Wilaya. Kwa hiyo mazoezi haya yamekuwa yanafanyika katika wilaya mbalimbali ili kuwaondoa watu ambao wamevunja sheria naamini ni kweli katika wilaya mbalimbali ikiwepo Dar es Salaam Kinondoni operesheni kama hizo zimeendeshwa kwenye bonde la Msimbazi kwa watu ambao wamevunja sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachoomba tu ni kwamba wananchi wazingatie sheria. Wasijenge bila vibali, wahakikishe kwamba kila wanapojenga wanajenga maeneo ambayo siyo hatarishi, wanafuata sheria ili angalau hatua kama hizi zinazozungumzwa na Mheshimiwa Mbunge zisiwapate. Hilo ndilo ombi langu.