Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Joseph Monko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Jimbo la Singida Kaskazini limepata Mradi wa Umeme Vijiji (REA na BTIP) ambapo utapeleka umeme katika vijiji 54 kati ya 84; katika baadhi ya maeneo ambayo mradi umepita umeacha nyumba za wananchi, taasisi za dini, taasisi za Serikali na pampu za maji pasipo kuziunganishia umeme. (a) Je, Serikali ina kauli gani kwa maeneo hayo yaliyorukwa na wananchi waliokwishafanya wiring kwa matarajio ya kuunanishiwa umeme? (b) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji 30 vilivyosalia? (c) Je, Serikali ipo tayari kusaidia njia mbadala ya umeme wa jua (solar power) katika maeneo ya huduma muhimu kama zahanati, sekondari na huduma za maji wakati tukisubiri usambazaji katika vijiji vilivyosalia?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, awali napenda tu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri aliyefanya ziara yake tarehe 16 Mei ambayo imesaidia sana hasa kwenye Mradi wa REA III.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mgori ambayo ina shule ya kidato cha tano na sita pamoja na Kituo cha Afya cha Mgori pamoja mgodi wa dhahabu pekee tulionao Jimboni wa Mpitipi katika Kata ya Mudida ambavyo vyote vipo katika umeme wa REA II havijapata umeme hadi sasa. Mgodi huu upo kilometa tatu tu kutoka ulipo umeme wa REA mpaka sasa.
Je, Waziri anawaambia nini wananchi kwamba maeneo haya yatapatiwa umeme lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili Kata ya Kinyeto yenye Kijiji cha Kinyeto, Mkimbii, Ntunduu na Minyaa pamoja na Kata ya Muhama yenye Kijiji cha Muhama na Msikii vipo katika umeme wa backbone. Vijiji hivi havijapata umeme mpaka sasa kwa sababu wanahitaji ku-upgrade kutoka umeme wa kilovolti 11 kwenda kwenye kilovolti 33.
Je, Mheshimiwa Waziri anatuahidi ni lini zoezi hili la upgrade litafanyika ili wananchi hawa waweze kupata umeme, ahsante sana. (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Monko na nimshukuru na yeye na kumpongeza sana kwa kazi nzuri na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Nishati alifanya ziara katika Mkoa wa Singida tarehe 16 Mei na kutoa msukumo mpya wa kasi ya miradi hii.
Mheshimiwa Spika, maswali yake mawili yalijielekeza kwanza kwenye Kata ya Mgori ambayo ipo chini ya REA II ambapo kwa kweli kulikuwa na changamoto katika Mkoa wa Singida na Kilimanjaro na ndiyo maana Serikali ilichukua hatua za haraka za kusitisha mkataba na kumpa mkandarasi mwingine na mpaka sasa hivi kazi zinazoendelea katika mradi wa REA II wa mkandarasi EMEC ni vijiji vinne vimeshawashwa kati ya 16.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo haya aliyoyataja yakiwemo na Mgori na kwenye mgodi huo kwa kuwa kazi inaendelea na kulikuwa na changamoto ya vifaa, Mheshimiwa Waziri aliielekeza REA iwasilishe vifaa mapema. Nimthibitishie tu kwa kipindi ambacho tunaelekea mpaka mwezi wa tisa, vijiji 12 vilivyosalia ikiwemo vya Kata ya Mgori vitapata umeme kutokana na jitihada zake za usimamizi na kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameulizia suala la Kata ya Kinyeto ambapo ipo katika mradi wa backbone na katika Jimbo hili, mradi huu unahusisha vijiji tisa na mpaka sasa hivi vijiji sita vimeshawashwa bado vijiji vitatu ambavyo Mheshimiwa Mbunge ndiyo ameviulizia hapa. Na kwa kuwa tatizo ni ku-upgrade tu kutoka KV 11 mpaka 33, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mara baada ya kutoka hapa tufanye mawasiliano na REA na kwa kuwa siyo changamoto kubwa na transfoma za aina hii zipo, ni kwamba ndani ya mwezi tu mmoja mpaka mwisho wa mwezi wa sita huu vijiji vilivyosalia ni vitatu na viwake. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Selemani Jumanne Zedi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Primary Question
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:- Jimbo la Singida Kaskazini limepata Mradi wa Umeme Vijiji (REA na BTIP) ambapo utapeleka umeme katika vijiji 54 kati ya 84; katika baadhi ya maeneo ambayo mradi umepita umeacha nyumba za wananchi, taasisi za dini, taasisi za Serikali na pampu za maji pasipo kuziunganishia umeme. (a) Je, Serikali ina kauli gani kwa maeneo hayo yaliyorukwa na wananchi waliokwishafanya wiring kwa matarajio ya kuunanishiwa umeme? (b) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji 30 vilivyosalia? (c) Je, Serikali ipo tayari kusaidia njia mbadala ya umeme wa jua (solar power) katika maeneo ya huduma muhimu kama zahanati, sekondari na huduma za maji wakati tukisubiri usambazaji katika vijiji vilivyosalia?
Supplementary Question 2
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, tatizo la miradi hii ya REA ambapo unakuta mradi umefika kwenye eneo kama kijiji lakini unakuta nyumba, taasisi za kidini, taasisi kama shule, zahanati, pampu za maji zimeachwa bila kuunganishiwa umeme, ni tatizo ambalo lipo pia Jimboni kwangu Bukene na Wilaya ya Nzega yote.
Mheshimiwa Spika, sasa ninachotaka kujua ni kwamba pamoja na kwamba Waziri alifanya ziara na akatoa maelekezo maalum kwa Mkandarasi wa Wilaya ya Nzega ambaye ni POMI Engineering kuhakikisha maeneo yaliyoachwa yanaunganishwa, lakini mpaka sasa mkandarasi huyu inaonekana ameshindwa kabisa kupata vifaa vya kuunganishia maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka kujua je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo maalum au kumsaidia huyu mkandarasi ili aweze kupata hivi vifaa; waya, nguzo ambavyo inaelekea kabisa kumpata…
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI:...ili aweze kufanya kazi ya kuunganisha maeneo hayo yaliyoachwa. (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze pia Mheshimiwa Zedi kwa kazi nzuri ndani ya Jimbo lake, wiki moja iliyopita tulikuwa katika ziara ya Jimbo lake na nilifanya pia ziara katika Wilaya ya Nzega. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, umelisema kwa jumla pia suala hili la vifaa, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Zedi na Wabunge wote, kweli zipo changamoto za hapa na pale kuhusu vifaa, lakini tukitathmini mchango wa sekta ya nishati kwenye viwanda vya ndani, kwa sababu changamoto hii imejitokeza baada ya kutoa agizo vifaa vyote vinavyotumika katika mradi huu vizalishwe ndani ya nchi na agizo hili limesababisha kuwezesha viwanda zaidi ya tisa vipya vinavyozalisha nguzo, viwanda zaidi ya vinne vya mita na viwanda zaidi ya vitano vya waya havikuwepo nchini, vyote hivi vimetokana na agizo la kuhakikisha kwamba vifaa vyote vinavyotumika kwenye miradi hii vizalishwe ndani ya nchi ili vilete ajira lakini pia mapato kwa wananchi lakini pia mapato kwa wanaoajiriwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Zedi mimi nikuthibitishie tu sisi kama Wizara tunaendelea kusimamia kuhakikisha changamoto hii inapungua na kama nilivyosema katika majibu mbalimbali ndani ya Bunge lako tukufu, imeendelea kupungua na ndiyo maana leo tunajivunia zaidi ya vijiji 1,400 tumeshaviwasha kwenye REA III mzunguko wa kwanza ukiacha na awamu zingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa wakandarasi pamoja na ma-supplier kwa kuwa wanategemeana, wakae pamoja ili kuondoa vikwazo mbalimbali ambavyo vinaonesha kwamba vinachangia kutokuwepo kwa vifaa kwa wakati katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe tu Wabunge muendelee kutuunga mkono katika hili ili mradi huu unaotumia shilingi trilioni moja na bilioni 200 uchangie uchumi wa taifa kwa kutekeleza Sera ya Viwanda, asante sana. (Makofi)