Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa ni chanzo cha migogoro badala ya kutatua migogoro. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kumudu majukumu yao kwa ufanisi?

Supplementary Question 1

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la kuingiliwa katika maamuzi ya kesi na wanasiasa hasa kwenye maeneo ya vijijini na hivyo kuathiri yale maamuzi.

Je, Serikali inatoa maelekezo gani kwa maeneo hayo ya vijijini ambako kumekuwa na mwingiliano wa viongozi wa kisiasa hasa Madiwani?

Lakini pili kumekuwa na tatizo kubwa la Mabaraza haya kutokuwa na vifaa vya kufanyia kazi, lakini kutokuwa na ofisi, posho za kuweza kujilipa na mwisho wa siku imekuwa wakiona yule anayedaiwa au anayehukumiwa ndiyo mwenye uwezo, wanaangalia nani mwenye uwezo basi wanamu-award ili waweze kupata hizo fedha na mwisho wa siku waweze kujilipa au kuweza kununua hivyo vifaa?

Je, ni nani mwenye wajibu wa kutoa hivi vifaa na kutoa hizi posho lakini pia na ofisi? Ahsante sana.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya wanasiasa ambao wanaingilia mambo hayo ya uendeshaji wa Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza kwenye jibu langu la msingi, haya mambo ni mambo ya kisheria ya tangu mwaka 1985 na yamefanyiwa marejeo mwaka 2002 wale Wajumbe wa Mabaraza ya Kata ni Wajumbe ambao wanatoka kwenye Kata husika kwa hiyo lazima uwe mkazi wa Kata husika kama siyo mkazi hupaswi kuingia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili la kuangalia wakati unapata Wajumbe wa Uendeshaji wa Mabaraza ya Kata, ni lazima hao watu wasiwe na tuhuma zozote za jinai na makosa mbalimbali kwa lugha nyingine lazima wawe ni waadilifu katika eneo lile, lakini majina haya ambayo yanaombwa yanapaswa kubandikwa kwenye notice za matangazo ili kama kuna mwananchi ana pingamizi dhidi ya mtu yeyote mjumbe aliyeomba aondolewe, lakini hakuna nafasi kabisa ya kiongozi wa kisiasa kuingilia kwa sababu kuna Kamati ya Ward DC inapendekeza majina kwa maana ya maoni, lakini uteuzi wa mwisho wa wajumbe hawa unafanywa na Halmashauri akiwepo Mwanasheria wa Halmashauri na Mkurugenzi na viongozi wengine, na ikiwezekana Mkuu wa Wilaya anaingia katika eneo hilo kwa maana ya kufanya consultation.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mujibu wa sheria hakuna namna ya kuingilia, lakini kama kuna eneo ambalo viongozi wa kisiasa wanaingilia hayo ndiyo maeneo tunayohitaji kupata taarifa ili tuweze kuchukua hatua na kutoa maelekezo na kuendesha vizuri katika maeneo hayo bila kuingiza siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni vitendea kazi ambayo inapelekea pia maamuzi ambayo yameyumbishwa kulingana labda na vipato na kuangalia nani amepeleka kesi katika eneo hili. Ni kweli kwamba tumepata pia maneno maeneo mbalimbali wanakosa vitendea kazi, lakini haya Mabaraza yanasimamiwa na Wakurugenzi wa Utendaji wa Halmashauri na Wanasheria wa Halmashauri na ndiyo maana baada ya kuchaguliwa wanapaswa waende watoe semina na mafunzo, lakini Bajeti za Halmashauri lazima ziwe na kipengele ambacho kinasaidia uendeshaji wa Mabaraza haya ya Kata na hata fedha ambazo wanapanga kwa mfano kesi imeamuliwa kutoka eneo moja ofisini kwenda kuangalia mahali ambapo kuna malalamiko inabidi gharama ile iwe ni gharama iwe ni gharama ya kawaida kabisa ndogo ambayo mtu wa kawaida ataifanya, na lengo la Mabaraza haya ni kupunguza umbali wa kuwafanya wananchi kutoka kwenye Kata yake kwenda kwenye Mahakama za mwanzo na Wilaya, lakini vilevile kuwasaidia watu wa kawaida kabisa ngazi ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nielekeze Wakurugenzi Watendaji na Wanasheria katika Halmashauri zetu kama kuna maeneo kuna malalamiko makubwa na watu wanakuwa charged gharama kubwa, naomba wachukue hatua ili tuweze kusimamia, tuweke viwango vya kawaida kabisa ambavyo mtu wa kawaida anaweza kufanya, lakini mwisho isije ikatokea hata siku moja kwa sababu kuna mtu ana malalamiko yake na kwa sababu hana uwezo wa kifedha asisikilizwe hili litakuwa ni kosa kwa viongozi wetu ambao wanasimamia katika eneo lile na itakuwa inaenda kinyume kabisa na maelekezo ya Baraza na Uanzishwaji wa Baraza la Usuluhishi wa Kata, nakushukuru sana.

Name

Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa ni chanzo cha migogoro badala ya kutatua migogoro. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kumudu majukumu yao kwa ufanisi?

Supplementary Question 2

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba unisikilize vizuri.

Kwa kuwa ni-declare interest kwamba niliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya kwa hiyo najua matatizo ya Mabaraza ya Kata. Mara nyingi wanaolalamika ni wale ambao hawana uwezo, ndiyo wanadhulumiwa ardhi na mashamba yao, wanaowadhulumu ni watu wenye uwezo na kwa sababu Halmashauri hazina uwezo wa kifedha wanaotoa gharama ya kuendeshea kesi hizo mahakama hiyo ni wale waliolalamikiwa wenye fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri haki itapatikana? Mimi nafikiri naomba unijibu. (Kicheko)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, haki inapaswa kupatikana hata kama hauna pesa, maelekezo ni kwamba zile bei ni kweli wanakubaliana, kwanza bahati nzuri viwango vya kutoza ni viwango ambavyo kwenye ngazi ya Kata ya Diwani na Ward DC yake wanaweza ku-moderate, Halmashauri zinaweza kusimamia, Mkuu wa Wilaya anaweza kuingilia, Mkuu wa Mkoa anaweza kuingilia, kwa hiyo, kuna flexibility kubwa sana ambayo unaweza ukaangalia hapo, lakini mahali pengine ilipotokea tumetoa maelekezo isitokee mtu ambaye hana uwezo asitendewe haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapanga viwango vya kawaida na maeneo mengine tumetoa maelekezo unakuta kwamba kwa mfano hata hukumu imetoka, lakini ile gharama ya kwenda kuchapisha ni kubwa anatozwa mwenye kesi, ikikosa anapeleka mtu mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nitoe maelekezo ni kwamba hili jambo ni jambo muhimu, jambo la kisheria na lililenga kimsingi kusaidia watu wa ngazi ya chini au maskini ndiyo Mabaraza ya Kata lililenga naomba viongozi wetu wakiwemo na Waheshimiwa Wabunge tuwasiliane, kama kuna mahali Mheshimiwa Mwamoto kuna mwananchi amedhulumiwa au hakusikilizwa kwa sababu hana fedha nipo tayari twende sasa hivi tukamsikilize na apate haki yake, ahsante.