Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amb. Adadi Mohamed Rajabu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Primary Question
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Serikali ilituma wataalam wa madini, mazingira na maji katika Kijiji cha Sakale, Tarafa ya Amani kuangalia uwezekano kama uchimbaji wa dhahabu unawezekana katika maeneo hayo. Je, Serikali imefikia uamuzi gani kuhusu suala hilo?
Supplementary Question 1
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu suala hili, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru sana Waziri wa Madini, Mheshimiwa Doto ambaye alifika kabisa Sakale kwenye kijiji hiki na kujionea hali halisi ya pale na pili, nawashukuru sana Wizara ya Madini pamoja Mazingira, kwa kuweza kupeleka wataalam kwa haraka sana kwenda kuangalia mazingira ya eneo lile na nawashukuru sana wananchi wa Sakale na Mbomole kwa nidhamu ambayo wanaionesha kuweza kutunza chazo cha maji cha Mto Zigi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la kwanza, ni ukweli kwamba pale dhahabu ipo kwenye Milima ya Sakale ambayo ipo karibu na Mto Zigi na dhahabu ambayo ipo pale ni ya kiwango cha juu. Sasa dhahabu ipo ndani ya mto na kwenye Milima ya Sakale. Sasa Serikali itakubaliana na mimi kwamba kuna umuhimu wa kutuma wataalam wa juu waliobobea kuweza kwenda kuangalia tena namna gani dhahabu ile inaweza kuchimbwa kutoka kwenye milima ambayo iko karibu na Mto Zigi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba kila wananchi wa Sakale, Mbomole wakitembea kwenye ardhi ile, wanahisia wanakanyaga dhahabu sasa na wanasikitika kwamba wanakanyaga mali ambayo ipo chini ya ardhi lakini Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kutoa ile mali pale nje.
Sasa Serikali inaona umuhimu gani wa kuchukua hatua za haraka kupeleka wale wataalam na kuhakikisha kwamba wananchi wa Sakale, Mbomole na Muheza wanafaidika na dhahabu hiyo ambayo iko kwenye Milima ya Sakale? Nakushukuru. (Makofi)
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika milima hiyo kuna dhahabu nyingi na milima hiyo kwenda hadi kwenye Mto Zigi kuna dhahabu nyingi tu ya kutosha, lakini kwa uchimbaji mdogo kwa sababu wachimbaji wadogo wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu, Wizara pamoja na wataalam wameshauri kwamba uchimbaji mdogo usifanyike pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa uchimbaji wa kati na uchimbaji mkubwa hilo linawezekana, lakini cha msingi tu ni kwamba ni lazima tupate mwekezaji ambaye anaweza akafanya utafiti wa kina kuweza kujua mashapo yamekaa vipi katika milima hiyo hadi kwenye mto na vilevile aweze kuchimba na uchimbaji wa maeneo hayo inabidi uchimbe katika style ya underground badala ya open cast mining. Ni kwamba wachimbe kwa kwenda chini na wahakikishe kwamba uchimbaji ule hautaathiri vyanzo vya maji kwa sababu vyanzo vya maji vya Mto Zigi vinategemewa katika Jiji la Tanga, Wilaya ya Korogwe na Wilaya ya Muheza yenyewe. Kwa hiyo, vyanzo hivi ni muhimu sana, ukiweka uchimbaji pale, ukawa unatiririsha kemikali kwenye vyanzo vya maji, ni hatari kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama uchimbaji wa kati au wa hali ya juu kwa sababu wale wanaweza wakachimba kwenda underground na vilevile ile processing plant inabidi iwekwe mbali na eneo hilo. Kwa hiyo, kusafirisha zile rocks za dhahabu kupeleka maeneo ambayo ni ya processing plant inabidi iwe ni distance kubwa, kwa hiyo, ni lazima uwekezaji uwe ni wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana, tutafute wawekezaji ambao wanaweza wakafanya detailed exploration kwa maana ya kujua mashapo yamekaa vipi na wakaweza kuja na plan nzuri ya uchimbaji ambao hautaathiri mazingira, vyanzo vya maji, hilo linawezekana. Kwa hiyo, tushirikiane tu na Mheshimiwa Mbunge kwa hilo nadhani tunaweza tukafikia pazuri. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Serikali ilituma wataalam wa madini, mazingira na maji katika Kijiji cha Sakale, Tarafa ya Amani kuangalia uwezekano kama uchimbaji wa dhahabu unawezekana katika maeneo hayo. Je, Serikali imefikia uamuzi gani kuhusu suala hilo?
Supplementary Question 2
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maonesho ya madini yaliyokuwa yanajulikana kama Arusha Gem Fair yalikuwa yanafanyika kuanzia mwaka 1992 na mwaka 2017 maonesho haya yalisimamishwa. Maonyesho haya yalikuwa muhimu kwa kuwa yalikuwa yanaitangaza Tanzania na kuonesha Tanzania ina madini yenye ubora wa hali ya juu ya kuweza kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa na kuingiza Tanzania katika ushindani wa soko la kimataifa. Je, ni lini Serikali itarudisha maonesho haya ya madini ya Arusha Gem Fair? (Makofi)
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwapigania wachimbaji wa madini wa Arusha, anafanya kazi kubwa sana na kwa kweli tunampongeza kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kusema kwamba baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini tuliyoifanya hapa Bungeni, ile Sheria ya Madini ya mwaka 2010, tukafanya mabadiliko mwaka 2017 ni kwamba tuliweza kuzuia utoaji wa madini ghafi (raw minerals) ni kwamba mpaka yaongezewe thamani ndiyo tuweze kuyatoa. Vilevile, ni kwamba maonesho haya mara nyingi yalikuwa yanafanyika pamoja na uuzaji wa madini hayo, kwa hiyo, wale organizer wa maonesho haya walikuwa wanatuomba kwamba kipindi cha maonesho haya waweze ku-export au kuweza kutoa nje madini ghafi na sheria ilikuwa inazuia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi tumekwenda vizuri, nadhani kufikia mwaka huu mwezi Julai mpaka wa Septemba tutakuwa tumefika sasa mahala pazuri tumekwisha kuelewana na hawa organizer wa haya maonesho na uzuri wa maonesho haya huwa yana kalenda ya kidunia.
Kwa hiyo, kalenda yetu ya mwaka ambao ukifika kwa maana ya Tanzania kupata zamu ya kuweza ku-organize maonesho haya, basi tunaweza tukaanza kukaribisha wawekezaji, waoneshaji na waoneshaji wakatoka katika maeneo/nchi zingine lakini vilevile kuweza kuonesha madini yetu ya Tanzanite ambayo kwa kweli sasa hivi wadau wengi wamekubali kuyaongezea thamani kwa maana ya kukata na sasa wapo tayari kwa ajili ya kuweza kupeleka kwenye maonesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari sasa kuyaridisha maonesho hayo wakati wowote ratiba ikishakuwa sawasawa, basi tutaweza kuyarudisha maonesho hayo na wananchi waweze kushiriki, ahsante sana.
Name
Lucy Thomas Mayenga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Serikali ilituma wataalam wa madini, mazingira na maji katika Kijiji cha Sakale, Tarafa ya Amani kuangalia uwezekano kama uchimbaji wa dhahabu unawezekana katika maeneo hayo. Je, Serikali imefikia uamuzi gani kuhusu suala hilo?
Supplementary Question 3
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali katika sekta hii ya madini kuhakikisha kwamba tunapata faida. Je, Serikali sasa iko tayari kukaa kwa Wizara nne; Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuweza kutoa kikwazo cha dola 300 za viza ya biashara kwa wafanyabiashara wa Congo ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha kusababisha nchi yetu kukosa dhahabu licha ya kufungua biashara ya dhahabu hapa nchini? (Makofi)
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika,ni kwamba sisi tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kweli hata sisi tunaona kwamba ni vizuri sasa kutoa viza kwa watu wanaotoka Congo. Vilevile tumeanzisha masoko katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na mikoa ambayo ipo mipakani mwa nchi yetu pamoja na Kigoma ambapo ni karibu na Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa tulipo sasa hivi ni kwamba tumetoa zile tozo ambazo zilikuwa zinakuwa charged katika Wizara yetu ya Madini kwamba mtu anapoingiza madini ni lazima alipe kiasi fulani, tumekwishakutoa hiyo ni moja ya hatua lakini vilevile tupo tayari kushirikiana na hizi Wizara kama alivyosema
Mheshimiwa Mbunge alivyotoa ushauri, basi tuangalie namna ya kuweza kurahisisha biashara kufanyika katika masoko haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi unaweza ukaleta madini katika masoko yetu na hatuulizi madini unayatoa wapi, wewe leta katika masoko yetu tutaangalia pale, tuta-charge sisi mrabaha wetu pamoja na clearance fee, utafanya biashara, wanunuzi utawakuta pale utaweza kufanya biashara yako vizuri na tumeweka mazingira mazuri.