Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Munira Mustafa Khatib
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuliza:- Kumekuwa na biashara haramu za mitandao maarufu kama pyramid schemes. Biashara ambazo zimeshamiri sana miji ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti biashara hizo ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa? (b) Je, ni kampuni ngapi za aina hiyo ambazo zimeingia nchini na kupata kibali cha kuendesha biashara za aina hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kudhibiti makampuni haya haramu kufanya biashara hii, ila yamekuepo baadhi ya makampuni haya yanayoendesha biashara hii kinyume na sheria. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia waathirika ambao fedha zao zimetapeliwa katika makampuni haya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; waathirika wakubwa wa biashara hii ni akina mama na vijana kutokana na mikopo yenye riba kubwa kwa mabenki, je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana na akinamama kuwapa mikopo yenye riba nafuu ili kuepukana na biashara hii haramu? (Makofi)
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kuwasaidia waathirika wa fedha hizi. Napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba washiriki wa biashara hii haramu wote, yule anayewashajihisha watu kufanya biashara hii na wale wanaoshiriki biashara hii wote wameshiriki kwenye biashara haramu kutokana na Sheria ya Makosa ya Jinai kama nilivyotaja kifungu 171A, B na C, wote wawili wanatenda kosa na wote wawili hawatakiwi kusaidiwa chochote zaidi ya kupata adhabu ya kushiriki katika biashara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; ni vipi Serikali inawasaidia vijana na akina mama; kwa dhamira njema kabisa Serikali yetu ilileta sheria hapa ya microfinance, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2018 ambapo kanuni zake zinakamilika na zitaanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 ili kuhakikisha vijana na akina mama wanapata mikopo kutoka kwenye taasisi halali ambazo zinatoza riba yenye kulipika, riba ambayo ni nafuu kabisa kwa vijana wetu na akina mama.
Lakini pili, Serikali yetu kupitia Bunge lako tukufu mwaka 2018 ilipitisha mabadiliko ya sheria kwenye Sheria ya Fedha kuhakikisha asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri inakuwa sasa ni lazima na ni sheria kwa Wakurugenzi wote wa halmashauri kutoa asilimia kumi hii na asilimia kumi hii ya mikopo inapotolewa haitozwi riba yoyote, riba yake ni sifuri ili akina mama na vijana wapate fedha hii waweze kufanya biashara zao bila kulipa riba yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia chini ya Wizara ya Fedha na Mipango tuna Taasisi ya Self Microfinance Bank ambayo inatoa mikopo katika riba nafuu sana kwa akina mama na vijana na imefanya vizuri katika mikoa mbalimbali. Naomba niwaombe na niwatake vijana wetu na akinamama wasijihusishe kwenye biashara haramu ila waende kwenye taasisi ambazo ni halali zenye dhamira njema ya kujenga uchumi wa taifa letu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved