Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:- Magari mengi ya Serikali yanafanyiwa service kwenye gereji kubwa hapa nchini hii imekuwa tofauti kwa magari yanayomilikiwa na Jeshi la Polisi:- Je, Serikali haioni kuwa upo umuhimu wa kuwa na maeneo ya kutengeneza na kurekebisha magari ya Polisi ili kuliimarishia vitendea kazi.

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa dhati kabisa nitambue kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini, lakini majibu haya haya hayaakisi hali halisi iliyopo kwenye maeneo yetu kule. Magari mengi ya Polisi yanapoharibika hutegemea zaidi hisani ya wadau mbalimbali hasa Wabunge kuweza kuyatengeneza. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa Jeshi letu la Polisi.

Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha utaratibu huu unatekelezwa na magari ya Polisi yanatengenezwa katika mazingira mazuri kama utaratibu ulivyoelekezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri?

Swali la pili; kama ilivyo kwa tatizo la magari vituo vyetu vya Polisi vinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa vitendea kazi vya kila siku kama mafuta ya magari, karatasi, wino na kadhalika. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa kila siku wa Jeshi letu la Polisi lakini hata kuchelewesha haki za wananchi wa kawaida kule kwenye vituo vyetu vya Polisi.

Nini sasa Mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inawezesha Jeshi letu kupata vifaa vya utendaji kazi vya kila siku kama hivi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kila siku?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo inagusa maeneo yote mawili aliyozungumza ni ufinyu wa bajeti. Uwezo wa Jeshi letu la Polisi kutengeneza magari kwa maana ya kiutalam tunao lakini wakati mwingine magari haya wanapohitaji kutengeneza yanahitaji ununuzi wa vipuli na matengenezo makubwa ambayo yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wadau wote mbalilmbali ikiwemo Waheshimiwa Wabunge ambao wameona changamoto hii na wameona umuhimu wa kusaidiana na Serikali kukabiliana na changamoto ya ubovu wa magari yetu katika Jeshi la Polisi. Ninawatia moyo waendelee hivyo nasi Serikali pamoja na Jeshi la Polisi mbali ya kuwa na Serikali inaendelea kuongeza bajeti la Jeshi la Polisi kadri ya hali inavyoruhusu lakini tumekuwa tukibuni mbinu mbalimbali za kuweza kuyarekebisha magari haya yaweze kuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna magari katika Mikoa mbalimbali ambayo tumefanya matengenezo kwa njia hii za ushirikishaji wa wadau. Hii inakwenda sambamba na hoja yake ya pili ambayo inahusu vitendea kazi kwa ajili ya Jeshi la Polisi nami nikuhakikishie kwamba kama ambavyo sote tunatambua jinsi ambavyo uchumi wetu unavyoendelea kukua vizuri hivyo Serikali kuongeza uwezo wa kuhudumia taasisi zake ni imani yangu kwamba changamoto hizi zitaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. (Makofi)