Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Gimbi Dotto Masaba
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:- Wananchi wa Wilaya ya Itilima, Mkoani Simiyu huvamiwa na kuharibiwu mazao yao na wanyama aina ya tembo na Serikali hutoa fidia kidogo na wakati mwingine kutowafidia kabisa:- Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wakulima juu ya fidia kwa waathirika wa uvamizi huo?
Supplementary Question 1
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ifahamike kuwa gharama za kukodisha mashamba zinapanda kila siku, unakuta kukodisha hekari moja ni Sh.200,000, uandaaji wa shamba ni kama Sh.300,000 bado ushuru wa Serikali. Je, Serikali haioni kwamba sasa inatakiwa kuweka mkakati wa lazima kuhakikisha wananchi hawa wanapata kifuta machozi ambacho kinastahili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana na utafiti umeonyesha kuwa miti ya pareto, pilipili, mizinga ya nyuki inasaidia kuwafukuza wanyama hawa. Je, Serikali ina mpango gani kuanzisha kampeni mahsusi kuhakikisha kwamba wanapanda hiyo miti kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi?
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nikiri kwamba swali hili limeulizwa mara nyingi sana hapa Bungeni na matukio ya wanyama kama tembo kuendelea kuharibu mashamba yanaendelea katika maeneo mengi na hivi karibuni Kalambo, Same yameendelea kusumbua. Kwa hiyo, tunakiri kwamba tunahitaji kuwa na mkakati kama nchi wa kuangalia namna tunavyoweza kuendelea kulinda mali za wananchi pia na maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana na swali lake la pili kwamba kama Serikali tunahitaji mkakati na tumewaelekeza watu wa TFS kuhakikisha kwamba wanatoa elimu na kusaidia kusambaza mizinga ya nyuki katika maeneo yote ambayo yamekuwa yakipata athari za wanyama hawa mara kwa mara. Pia katika mikutano yote ya hadhara tumekuwa tukihamasisha upandaji wa pilipili. Katika maeneo mengi zao za pareto siyo maarufu lakini limeaminika kwamba linapokuwa limepandwa kwenye mipaka ya mashamba linasaidia kuzuia tembo wasisambae. Kwa hiyo, tunachukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu kifuta machozi, ni kweli kwamba hata lugha inayotumika kwenye majibu yetu ni kifuta jasho na kifuta machozi sio fidia na gharama za kuandaa shamba heka moja zinakadiriwa kuwa takribani Sh.300,000 mpaka Sh.350,000 ambapo sisi kwenye taratibu zetu tumekuwa tukilipa pesa isiyozodi Sh.100,000. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge moja ya maeneo ambayo tunayarejea sasa kuyaangalia vizuri ni kuangalia gharama kutokana na hali halisi ya sasa zikiwemo gharama za uandaaji wa mashamba pamoja na mbegu na mambo mengine. Kwa hiyo, tumemaliza hatua ya wadau wa ndani na tunajielekeza sasa kupata maoni ya wadau wa nje na mara taratibu hizo zitakapokamilika tutakuwa tumefikia kwenye kiwango ambacho kinaweza kikawa angalau ni cha kuridhisha.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved