Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mbarouk Salim Ali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wete

Primary Question

MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:- Je, ni mafanikio gani yameweza kupatikana katika kushirikisha jamii katika jitihada za usimamizi wa maliasili nchini?

Supplementary Question 1

MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, lakini mimi swali langu lilikuwa linajumuisha maliasili zote kwa ujumla ingawaje yeye amekwenda very specifically kwenye misitu, lakini hayo tuache.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, zoezi hili la ushirikishwaji wa jamii ni la muda mrefu kwa kweli, inasikitisha kwamba bado kuna malalamiko mengi ya migogoro na mambo mengine mengi. Nilitaka kujua ni kwa nini mpaka leo hii WMA’s nyingi hawapati gawio lao kwa wakati na kwa ukamilifu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na miradi mingi ambayo inafanywa na Serikali katika jamii hizi ambazo zimezungukwa na maliasili hizi ni sawa lakini jamii hizi ni maskini wa kutupwa na miradi mingi imeelekea zaidi kwenye miradi ya kijamii. Je, Serikali haioni kwamba sasa kuna haja au ulazima wa kubadilisha mwelekeo na kuelekeza nguvu zao zaidi kwenye miradi ya kiuchumi na kuwapatia taaluma wananchi ili waweze kujikimu? (Makofi)

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema swali lake lilikuwa linauliza maliasili kwa ujumla na ili kumjibu swali hilo labda pengine ningehitaji nusu saa nzima kwa sababu kama unavyofahamu maliasili kwa ujumla almost asilimia 50 ya nchi hii iko kwenye maliasili. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama ana swali la nyongeza tunaweza tukawasiliana ili kuweka vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kufahamu kwa nini WMA nyingi hazipati migao yake ya fedha kwa wakati na kwa kiwango cha thamani halisi. Naomba kwanza nitoe maelezo mazuri kwamba WMA ni jumuiya ambazo zinaanzishwa na vijiji kwa kutenga maeneo yao wanaanzisha jumuiya ambayo wanatafuta mwekezaji ambaye wanaingia naye mkataba kwa kutumia vikao mbalimbali wanakuwa na uongozi wao ambao unawajibika moja kwa moja kwenye kusimamia maslahi ya WMA. Hapa katikati tulirekebisha kanuni baada ya kuona tulikuwa na viongozi wengi ambao walikuwa wanapokwenda kwenye vikao hivi vya WMA wanazidiwa maarifa na wawekezaji tukarekebisha kanuni ili kuruhusu aina fulani ya elimu ili iweze kutumika lakini jumuiya ya WMA yenyewe imerudi na malalamiko kwamba inataka watu wote ili mradi anajua kusoma na kuandika waingie kwenye uongozi wa WMA. Kwa hiyo, hii ilikuwa ni changamoto lakini tumetoa maelekezo maalum kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhakikisha kwamba inatoa msaada wa kitaalamu na kitaaluma katika usimamizi wa WMA ili iweze kupata maslahi yake kwa mujibu wa mkataba walioingia na mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, jamii nyingi ambazo zinazunguka maeneo haya yenye maliasili ni maskini na kwa sababu Serikali labda imejielekeza zaidi katika miradi ya kijamii kama shule na kadhalika. Miradi yote inayofanywa na Mapori yetu ya Akiba na Hifadhi za Taifa na WMA ni miradi inayochaguliwa na vijiji vyenyewe. Vijiji vinakaa na kutenga miradi ya kipaumbele na vinapeleka muhtasari wa makubaliano haya kwenye mamlaka husika ya hifadhi, ndiyo inakwenda kujenga au kutoa msaada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeanza hivi karibuni sasa kuweka package ya kutoa elimu ya fursa mbalimbali ambazo zipo katika maeneo yanayopakana na hifadhi ili kuwaruhusu wananchi hawa kushiriki moja kwa moja kwenye mapato na biashara ya hifadhi na utalii yanayopakana na maeneo yao ya vijiji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tu nikushukuru kwamba maoni yako na ushauri wako tayari tumeanza kuufanyia kazi na tunashukuru kwa mtazamo huo na ndiyo mtazamo wa Wizara kuanzia sasa kuwashirikisha wananchi wote katika farsa ambazo zinapatikana katika maeneo yao.