Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:- Kituo cha Polisi Lukumbule kiliungua moto miaka iliyopita na mpaka sasa kituo hicho hakina Askari kimefungwa:- (a) Je, ni lini Serikali itakirejesha kituo hicho hasa ikizingatiwa kuwa kipo mpakani mwa nchi ya Msumbiji? (b) Je, ni lini Serikali itaweka kituo cha Uhamiaji katika kituo hicho cha Lukumbule? (c) Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Lukumbule ambacho kimeishia kwenye lenta baada ya Halmashauri kushindwa kumalizia ujenzi huo?

Supplementary Question 1

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini chanzo cha kituo kile kuchomwa ni mgogoro wa ugomvi wa usalama barabarani kati ya Askari pamoja na bodaboda, hii ndiyo imekuwa tabia ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na tabia hiyo ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji likiwa na Tarafa tatu. Tarafa ya Namasakata tangu imeundwa haijawahi kuwa na Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka Kituo cha Polisi Misechela na Namasakate yenyewe kwa kituo cha polisi ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini na Tarafa ya Namasakata kwa ujumla.

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hatuwezi kuhalalisha jambo lolote na vitendo vya uchomaji vituo vya Polisi, kwa hiyo hata kama kulikuwa kuna matatizo kati ya bodaboda iwe na Askari wa Usalama barabarani ama awe Askari yeyote basi haihalalishi uchomaji wa kituo cha polisi, hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake kwamba kuna watu ambao siyo Askari wa Usalama Barabarani wanawapiga bodaboda. Niliwahi kujibu swali hili siku chache zilizopita na nilieleza kwamba hatujapata taarifa ya kuona Askari Polisi wakipiga bodaboda na kama kuna taarifa hizo basi ni vema tukapatiwa ili tuzifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba wanaofanya hivyo siyo Askari wa Usalama Barabarani, kwa sababu tunaamini askari wa usalama barabarani wamepata mafunzo na weledi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao, Askari wa aina nyingine yoyote ama watu wa aina nyingine yoyote ambao wanafanya vitendo kama hivyo kama wapo kauli ya Serikali ni kwamba ni kinyume na utaratibu hivyo watumie weledi katika kuhakikisha kwamba wanawakamata wanaovunja sheria ikiwemo hawa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu maeneo hayo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ambapo anataka kujua ni lini tutajenga kituo cha polisi. Jibu ni kwamba katika maeneo yote nchini tutajenga kuanzia kwenye wilaya hata ngazi ya kata ikiwemo maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu.