Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Frank George Mwakajoka
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:- Je, ni upi mpango wa sasa wa kutatua kero ya maji katika Jimbo la Momba?
Supplementary Question 1
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba vijiji vitano mpaka sasa hivi vimeshakamilika kupata maji katika Jimbo la Momba ambapo jumla ya vijiji vilivyopata maji sasa hivi vitakuwa ni saba (7) lakini jimbo hili lina vijiji 82 ina maana kati ya vijiji 82 ni vijiji saba (7) tu ndiyo vyenye maji ya bomba. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika bajeti hii ambayo imetengwa ya shilingi bilioni 1.7 inapelekwa kama ambavyo imetengwa ili kwenda kupunguza tatizo la maji kwenye Jimbo la Momba?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 1973 katika Mji wa Tunduma uliazishwa mradi wa maji wa mserereko katika Kata za Mpemba na Katete. Mradi ule sasa hivi umekuwa ukitoa maji kidogo sana kutokana na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu. Serikali ina mpango gani kukarabati mradi ule ili uwahudumie wananchi wa kata hizo mbili?
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Kikubwa ambacho nataka kusema ni kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatutaka itakapofika 2020 tuwe na 85% ya upatikanaji wa maji vijiji na 95% upatikanaji wa maji mijini.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, sisi kama Wizara ya Maji tukaona chanzo pekee ambacho kinaweza kutatua tatizo la maji katika Mji wa Momba ni kutumia Mto Momba. Sasa hivi tupo kwenye hatua ya usanifu, mradi ule utakapoanza utaweza kuhudumia zaidi ya vijiji 21. Kwa hiyo, tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutafanya usanifu ule kwa haraka kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuchukua maji Mto Momba na kuweza kuhudumia vijiji 21.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mradi wa ukarabati wa mradi wa maji kwa ajili ya kuhudumia Kata ya Mpemba, sisi kama Wizara ya Maji tutaongea na Wahandisi wetu Maji pale Tunduma kuhakikisha wanafanya ukarabati huo ili wananchi waweze kupata huduma hii maji. Maji ni uhai, sisi kama viongozi wa Wizara hatupo tayari kupoteza uhai wa wana Tunduma.
Name
Joseph Osmund Mbilinyi
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbeya Mjini
Primary Question
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:- Je, ni upi mpango wa sasa wa kutatua kero ya maji katika Jimbo la Momba?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kama lilivyo tatizo la maji katika Jimbo la
Momba kwenye Jiji la Mbeya sasa hivi tatizo la maji tunaweza tukasema ni janga. Bonde lote la Uyole maji ni tatizo, ni kukavu kabisa, wananchi wanyonge wananunua maji mpaka ndoo Sh.500, maisha haya yalivyokuwa magumu. Maeneo ya Mwakibete na Ilomba, kote maji ni tatizo. Tumeshauri ili kutatua tatizo la maji Mbeya tutoe maji Mto Kiwira iwe kama source.
Mheshimiwa Spika, cha ajabu akija Rais au Waziri Mkuu maji Mbeya yanatoka, hayakatiki, wakiondoka maji yanakatika. Tatizo nini hasa ambalo linafanya changamoto hii ya maji katika jiji la Mbeya lisitatulike wakati vyanzo vya maji tunavyo na miundombinu ipo?
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu kaka yangu Mheshimiwa Mbilinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo ambalo nataka kusema ni kwamba Jiji la Mbeya sasa hivi limekuwa na ongezeko kubwa sana la watu. Kwa hiyo, mahitaji na uzalishaji wetu umezidiwa kutoka na ongezeko kubwa la watu.
Mheshimiwa Spika, mimi kama Naibu Waziri wa Maji nilifika Mbeya na nimejionea hali halisi na kweli nimefika katika chanzo cha Mto Kiwira tumeona hiki ni chanzo pekee ambacho kinaweza kikatumika na kutatua tatizo la maji la Mbeya. Tumekubaliana sisi kama Wizara kuangalia namna ya kufanya usanifu ili sasa tuweze kutumia chanzo cha Mto Kiwira katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Jiji la Mbeya.
Mheshimiwa Spika, lakini haki ya mwananchi ni kupatiwa huduma ya maji. Niwaagize Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya Mbeya kuhakikisha inatoa huduma hii maji, kwa uchache wake, lakini kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma muhimu na bora si mpaka kiongozi aweze kufika. Cha msingi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara tumejipanga kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji katika Jiji la Mbeya.
Name
Aysharose Ndogholi Mattembe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA (K.n.y MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:- Je, ni upi mpango wa sasa wa kutatua kero ya maji katika Jimbo la Momba?
Supplementary Question 3
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Changamoto ya ukosefu wa maji iliyopo Momba inafanana kabisa na changamoto ya ukosefu wa maji iliyopo Manyoni Mashariki.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mradi wa Kintinku - Lusilile utekelezaji wake umekuwa ukisuasua, je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka fedha za kutosha ili kukamilisha mradi huo hasa ikizingatiwa kwamba kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha zaidi ya wakazi wa vijiji kumi? Nashukuru.
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda nijibu swali la dada yangu Mheshimiwa Aisharose, kwanza, ni miongoni mwa Wabunge akina mama wafuatiliaji suala zima la maji katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kikubwa nachotaka kusema utekelezaji miradi ya maji unategemea na fedha. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji tutawaangalia kwa namna ya kipekee katika kuhakikisha wakandarasi wanao-rise certificate ya utekelezaji wa mradi wa pale Manyoni Mshariki tunawalipa kwa wakati na utekelezaji wake uendelee na wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, pia nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Manyoni kuwa na changamoto ya maji lakini sisi kama serikali na tunamshukuru Mheshimiwa Rais zaidi ya dola milioni 500 tulizozipata kwa ajili ya kutatua tatizo la maji nchi zaidi ya miji 28 Tanzania Bara na mji mmoja Zanzibar, sasa hivi Mkoa wa Singida miji mitatu tunaenda kutatua tatizo la maji. Wahandisi Washauri wameshapatikana, nataka nimhakikishie itakapofika mwezi September wakandarasi watakuwa site katika kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji na sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga vizuri sana.