Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Christopher Kajoro Chizza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Primary Question
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:- Kumekuwa na dalili za upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Kabingo, Ruhuru, Nyakayenzi, Nyamwilonge na Muhange Wilayani Kakonko na katika baadhi ya vijiji uchimbaji umeanza:- Je, Serikali inatoa ushauri gani kwa vijana ambao wapo tayari kujishughulisha na uchimbaji wa madini?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Kakonko na kuzungumza na wadau ambao wanataka kuchimba madini hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, Naibu Waziri alipokuja wadau walimwonesha nia ya kuchimba madini haya pamoja na madini ya chokaa, yanayopatikana kwa wingi katika Wilaya ya Kakonko na katika Mkoa wa Kigoma ambayo yanatumika sana kwa shughuli za ujenzi, shughuli za kulainisha ngozi na kazi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa kuwa sisi tumejiandaa katika Wilaya ya Kakonko, kujenga kiwanda cha kuchakata chokaa kuwasaidia vijana. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, sehemu ya tatu, Mheshimiwa Waziri ameshauri vijana wote wanaotaka kushughulika na uchimbaji wafike kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Kigoma. Kutoka Nyamwilonge mpaka Kigoma ni kilomita zaidi ya 300. Swali la kwanza, je, haoni kwamba ingekuwa busara sasa, badala ya vijana wote hawa kwenda Kigoma kilomita 300, amwagize Afisa Mkazi huyu wa Madini yeye ndiye awatembelee kuwapa ushauri kule waliko? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa madini ya chokaa yanapatikana kwa wingi katika Wilaya ya Kakono na katika Mkoa wa Kigoma, lakini katika Wilaya ya Kakonko, madini yote haya yapo katika Pori la Akiba la Moyowosi, ambalo Serikali inawazuia kuchimba au kufanya shughuli za uchimbaji katika pori la akiba. Je, Mheshimiwa Waziri, yuko tayari sasa kukaa na Wizara ya Maliasili ili kuangalia uwezekano wa Wizara hizi mbili kutoa kibali kwa wachimbaji hawa kufanya uchimbaji salama ili waweze kuchimba chokaa hii? (Makofi)
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze tu kumpongeza sana Mheshimiwa Chiza kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele sana kushughulika na suala la madini kwenye Wilaya ya Kakonko na kama utakumbuka tarehe 5 mwezi wa Aprili, aliuliza swali hapa hapa kwa ajili ya madini ya chokaa na leo ameuliza kwa ajili ya madini ya dhahabu, tunampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tu kwamba ni kweli, tumeweka Ofisi za Madini kila Mkoa ambazo kazi yake ni kutoa huduma kwa watu wanaotaka kujishughulisha na uchimbaji wa madini na sasa kutoka Kakonko kwenda Kigoma pana umbali mrefu sana. Nakubaliana naye, kwamba, Afisa Madini awatembelee aweze kutoa elimu hiyo. Pia nimwombe sana Mheshimiwa Mbunge, yeye pamoja na wale vijana wapange tarehe, tarehe fulani watakuwa tayari, Afisa Madini atakuja pale kuwapa elimu juu ya utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa madini haya yako kwenye hifadhi na kwamba wanataka wachimbe ndani ya hifadhi ya Kigosi. Naomba tu nimjulishe kwamba Mheshimiwa Mbunge, utaratibu uliopo ni kwamba, Wizara ya Madini wajibu wake ni kutoa leseni ya Madini (Mineral Right) na mwenye wajibu wa kutoa kibali kwa ajili ya mtu kupata access ya kuingia kwenye mapori hayo ni yule mwenye surface right ambaye kwa mujibu wa sheria ni Wizara ya Maliasili na Utalii. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge, yeye pamoja na wenzetu Wizara ya Maliasili na Utalii, wazungumze kuona namna gani bora wanaweza kupata kibali cha kuwea kufanya kazi kwenye maeneo hayo kama Sheria ya Maliasili itaruhusu. Nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved