Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuyagawa kwa wananchi mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji katika Kata za Daa na Oldeani, Wilayani Karatu ambayo hayaendelezwi huku wananchi wakikosa ardhi kwa ajili ya makazi?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika kata husika nilizozitaja katika swali langu la msingi kuna baadhi ya mashamba wawekezaji wamehifadhi mapori ambayo hawayaendelezi. Mapori hayo yanahifadhi pia wanyama ambao ni hatarishi kwa wakati katika maeneo hayo.
Je, Serikali sasa wako tayari kwa kushirikiana na halmashauri kwa sababu, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuhakikisha wanayatambua haya maeneo na kufanya partial revocation na yale maeneo yarudi kwa wananchi ili wananchi wanaozunguka maeneo hayo pamoja na wanafunzi wanaoenda shule waishi katika maeneo salama bila kuathiriwa na maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika mashamba hayo hayo niliyoyataja, kuna shamba mojawapo linaitwa Shamba la Benduu, mwekezaji alishafariki, nitamwandikia Mheshimiwa vizuri kwa karatasi; mwekezaji alishafariki, lile shamba wafanyakazi wake hawajalipwa takribani miezi nane na hawaruhusiwi kwenda kufanya kibarua kwenye mashamba mengine, hawajui hatima ya haya maslahi yao na hawajui hatima ya nini wafanye kwa sababu, wakitoka kwenda kufanya kazi kwenye shamba lingine anafukuzwa asirudi kwenye lile shamba. Je, sasa Serikali wako tayari kwenda kutatua mgogoro uliopo katika shamba hilo, ili wananchi wanaofanya kazi na vibarua wanaofanya kazi katika eneo hilo wapate haki zao na pia waruhusiwe kufanya kazi katika maeneo mengine, ili waendelee kujipatia kipato? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameongelea kwamba, baadhi ya mashamba yamefanywa mapori na yanafuga wanyama kule ambao pengine ni hatarishi kwa watu na anaomba pengine yaweze kufanyiwa partial revocation kwa maana ya kwamba, ile sehemu ambayo pengine haitumiki basi iweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kutoa jibu la moja kwa moja kwa sababu, ni mpaka anachokisema hicho kiwe na uhakika kwa sababu, unapopewa shamba kuna muda wake wa kuweza kuliendeleza, ndani ya miaka mitano unatakiwa kuwa umeendeleza angalau moja ya nane ya hilo shamba. Sasa kama mashamba hayo hayajaendelezwa kwa kiwango hicho kwa sababu, tumeshasema uhakiki unaendelea kufanyika basi, tutapita pia kuona hilo shamba likoje, lakini kama nilivyosema mwanzo mashamba yote 25 ya Wilaya ya Karatu yamefanyiwa uhakiki na kwa sehemu kubwa yameendelezwa zaidi ya asilimia 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaongelea Shamba la Benduu, nadhani atanipa karatasi, kwamba, mwekezaji alikwishafariki na watumishi wale wanadai hawana malipo. Nadhani hili ni suala la kisheria zaidi kwa sababu, kama mtu amefariki kuna mtu ambaye anatakiwa kuwa administrator wa mali ya yule aliyefariki. Kama atakuwa ameteuliwa msimamizi wa mirathi katika eneo lile basi, huyo atabeba dhamana pia ya kuweza kulipa wafanyakazi ambao wanadai, wanayemdai alishafariki na tayari kuna mtu ambaye anasimamia mirathi ile atashughulikanao katika suala zima la kuweza kupata haki zao.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved