Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza: - Upatikanaji wa maji katika Mji mdogo wa Same ni asilimia 34; na mradi mkubwa wa maji Same – Mwanga – Korogwe umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa: - (a) Je, ni kitu gani kilichochelewesha mradi huo na ni hatua gani zimechukuliwa kwa watu waliohusika na ucheleweshaji huo? (b) Je, ni lini sasa mradi utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawili ya nyongeza lakini kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka msukumo kwenye mradi huu. Pia niipongeze Serikali kwa maana ya Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kufanya kazi vizuri na kufuatilia vizuri mradi huu na kuondoa wakandarasi ambao ni wazembe ambao wanachelewesha huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la nyongeza, kwa kuwa Desemba ni mbali kwa mahitaji ya maji katika Mji Mdogo wa Same kata za Njoro, Kisima, Stesheni pamoja na Same Mjini; na kwa kuwa Serikali hivi sasa inachimba visima viwili virefu, je, visima hivi vitakamilika lini ikiwa ni pamoja na kuweka pump kusudi wananchi hawa waweze kupunguza makali ya ukosefu wa maji kabla ya Desemba kufika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili ili twende tukakague kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji kuhusiana na utekelezaji wa mradi huu?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tunafahamu kwamba Desemba ni mbali na maisha lazima yaendelee. Sisi Wizara ya Maji tuko imara kabisa kuhakikisha kwamba tatizo sugu la maji tunakwenda kulishughulikia kwa haraka sana. Wizara tumejipanga vyema chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Jumaa Aweso ambapo katika Mji wa Same kisima kipya kimeshachimbwa eneo la Stelingi chenye kina cha mita 200. Kazi hii ilianza Oktoba 2020 na itakamilika mwezi huu Februari 2021. Kama Quick-win program ya kuongeza uzalishaji wa maji katika Mji wa Same utahudumiwa na visima virefu viwili vilivyopo Stelingi na Kambambungu pamoja na chemichemi mbili za Mahuu na Same Beach.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la kuongozana na wewe Mheshimiwa Mbunge usiwe na hofu, hiyo ndiyo shughuli yangu. Mheshimiwa Mbunge nitampa upendeleo mara baada ya Bunge hili tutakwenda, tutahakikisha wananchi wa Same Magharibi wanapata maji ya kutosha na hilo tatizo litabaki kuwa historia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na napenda kumjulisha tu Mheshimiwa David kwamba timu kubwa ya club kubwa ya pale Msimbazi iko humu ndani basi na kesho tunakukaribisha. (Makofi/Kicheko)