Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia umeme vijiji 32 vya Jimbo la Lushoto ambavyo havina umeme?

Supplementary Question 1

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa mradi wa REA utaanza Februari hii ambapo leo ni tarehe 3 na katika Jimbo la Lushoto kuna vijiji vimerukwa kwa muda mrefu sana hasa katika Vijiji vya Kilole, Ngulu, Gale, Miegeyo, Handei, Magashai, Tambwe, Mazumbai, Ngwelo, Milungui na kata nzima ya Makanya. Je, Serikali haioni kwamba sasa vijiji hivi lazima vipewe kipaumbele kwa ajili ya kupata umeme kwa sababu wamesubiri kwa muda mrefu sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Jimbo la Lushoto lina vitongoji zaidi ya 32 na Mheshimiwa Waziri Kalemani yeye ni shahidi ametembelea Lushoto na akaona Wilaya nzima ya Lushoto hakuna nyumba ya nyasi hata moja na wananchi wote wameshafanya wiring wanasubiri umeme. Je, ni lini sasa vitongoji vile vya Wilaya ya Lushoto vitapata umeme kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki kama wenzao wanavyopata huduma?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, commitment ya Serikali ni kwamba, ifikapo tarehe 15 Februari, 2021 vijiji vyote vilivyobakia 2,150 ambavyo havikuwa vimepata umeme katika REA Awamu I, II na III mzunguko wa kwanza vitapelekewa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliofanyika sasa hivi ni kuhakikisha kwamba mkandarasi mmoja hapewi kazi kubwa sana. Kwa hiyo, tutaona maajabu makubwa katika kipindi hiki ambapo tutaanza kupeleka umeme katika maeneo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu mkandarasi mmoja pengine inaweza ikawa anapeleka umeme au jimbo moja. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Shekilindi, kwamba huduma anayotupatia ya dawa na sisi tutapeleka huduma ya umeme kwenye kwa kadri tulivyoelekeza katika kipindi hiki hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili la kupeleka umeme kwenye vitongoji, Wizara ya Nishati kwa maelekezo ya Serikali inatekeleza mradi unaoitwa densification na sasa tuko katika densification 2B ambao ni mradi jazilizi kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji na kufikia mwezi Mei tutakuwa tayari tumesaini mikataba kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vitongoji zaidi ya 2,800 katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, tunaamini katika upanuzi huo wa miradi jazilizi, basi Jimbo la Lushoto pia litapata maeneo kadhaa ya kuwekewa umeme katika maeneo ya vitongoji vyake. (Makofi)