Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: - Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: - Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama lilivyo swali la msingi, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwenye Wilaya ya Kyerwa tuna kata 24 lakini tuna vituo vya afya vitatu; Serikali ina mpango gani wa kuongeza vituo vya afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya Nkwenda ni kituo ambacho tumeanzisha jengo la mama na mtoto ambalo bado halijakamilishwa. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Kituo cha Afya Nkwenda kwenye jengo la mama na mtoto?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Halmashauri ya Kyerwa kuwa na kata 24 na vituo vya afya vitatu tu na Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba halmashauri hiyo inapata vituo vya afya kadri ya maelekezo na sera. Kama ambavyo nimetangulia kusema kwenye jibu la msingi, Serikali imedhamiria kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuunga mkono ujenzi wa vituo vya afya katika kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa utekelezaji wa miradi hii ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata ni endelevu na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo 555. Pia katika mwaka wa fedha ujao tutatenga bajeti kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo hivyo. Halmashauri ya Kyerwa na kata zake ni sehemu ya halmashauri na kata ambazo zitanufaika katika mradi huu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili litafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kituo cha afya kuwa na jengo la wazazi na Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha jengo hilo linakamilika na kutoa huduma. Hilo ni jambo la muhimu sana katika kusogeza huduma kwa wananchi. Kwa sababu Serikali inatambua na ina dhamira ya dhati ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga, kipaumbele ni pamoja na kutenga fedha kadri zinavyopatikana kwa ajili ya kukamilisha majengo kama haya. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba pia jengo hilo litakuwa sehemu ya mpango huu ili liweze kukamilishwa na kutoa huduma zinazokusudiwa kwa wananchi.

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: - Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: - Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kijiji cha Migungumalo, Kata ya Usagari, Marehemu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alizindua zahanati ndogo na aliahidi kwamba pale patajengwa kituo cha afya ili iwe hospitali kubwa ambayo atakuja kuifungua tena. Nilipoingia madarakani tumeanzisha kujenga kituo kile na kwa uchungu sana nilikuwa nimepanga kwenda kumwambia Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwamba sasa ajiandae kuja kufungua kituo kile na bahati mbaya Mheshimiwa Mkapa amefariki, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Nimeshamwambia Mheshimiwa Rais juu ya suala hilo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maige, swali lako la nyongeza?

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, kwa vile kituo kile tunakijenga kwa nguvu za wananchi, je, Serikali ina mpango gani wa kukimalizia kituo hicho ili heshima ya Marehemu Benjamin Mkapa ihimidiwe?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini kwa kuchangia maendeleo na kuanza ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho lengo ni kupandisha hadhi ya zahanati kuwa kituo cha afya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maige kwamba katika bajeti ya Serikali ya kwenda kukamilisha majengo ya zahanati na vituo vya afya ambayo imetengwa katika mwaka huu wa fedha katika halmashauri yake na katika jimbo lake, jumla ya vituo vinne vimetengwa na jumla ya shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo eneo hilo la kituo hicho cha afya ambacho ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, basi tutakwenda pia kuona namna gani tunashirikiana katika bajeti hii, lakini pia katika bajeti zinazofuata, ili tuweze kukikamilisha kiweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Name

Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: - Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: - Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la vituo vya afya vilivyopo kwenye Jimbo la Tabora Kaskazini ni sawa na lililopo kwenye Jimbo la Igunga, Kata za Isakamaliwa, Kining’inila na Mtungulu. Ni kata ambazo hazina vituo vya afya vya kata na sisi kama wananchi tumeanza kutoa nguvu yetu kusaidia wananchi kujenga vituo vya kata. Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi kukamilisha vituo vya hizo kata husika ili tuweze kuwapatia wananchi huduma ya afya? Ahsante sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya katika kata. Katika bajeti ambayo imetengwa lengo ni kuhakikisha kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha nguvu za wananchi zitaendelea kuungwa mkono kwa Serikali kupeleka fedha ili kukamilisha vituo vya afya na zahanati zinazojengwa katika maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Igunga kwamba Igunga ni sehemu ya halmashauri na kata zake ni sehemu ya kata nchini kote ambazo zitanufaika na mpango huu wa umaliziaji na ujenzi wa vituo vya afya ili viweze kutoa huduma kwa wananchi.