Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI) aliuliza: - Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni Halmashauri mpya iliyotoka Wilaya ya Kilombero: - (a) Je, ni lini Serikali itaipa Mlimba hadhi ya kuwa Wilaya hasa ikizingatiwa umbali mrefu wa takriban Km 200 ambao Wananchi wanatembea kufuata huduma Makao Makuu ya Wilaya? (b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Halmashauri na kuboresha miundombinu ya barabara?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tunajua kwamba Serikali ilisitisha uongezaji wa maeneo ya utawala lakini Serikali ilitoa ahadi hapa Bungeni kwamba yale maeneo ambayo hayatakuwa na gharama za uanzishwaji wake na hasa maeneo ya kata, kwa sababu kata zetu hizi ni kubwa mno katika baadahi ya maeneo. Je, Serikali itaanza kutekeleza ahadi hii lini ili kusogeza huduma karibu na wananchi wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezizungumzia hapa zimekuwa zikiharibika mara kwa mara na hasa wakati huu wa kipindi cha mvua. Uwezo wa TARURA kuendelea kuzikarabati hizi barabara unaonekana unapungua siku hadi siku kwa sababu ya mgao mdogo ambao wanaupata kutoka kwenye fedha za Bodi ya Barabara. Je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kuanzisha chanzo maalum cha fedha kupelekwa kwenye TARURA badala ya kutegemea hisani kutoka kwenye Mfuko wa Barabara?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali ina mpango na dhamira ya dhati ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi kwa kuanzisha maeneo ya utawala ambayo hayatakuwa na gharama kubwa. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, naomba nimhakikishie kwamba dhamira hiyo ya Serikali ipo na utaratibu wa kuomba maeneo hayo unafahamika na nishauri kwamba pale ambapo tunaona kuna kila sababu ya kuanzisha maeneo hayo yanayofuata maelekezo ya Serikali ya kuzingatia kutokuongeza gharama, basi maombi yawasilishwe kwa mujibu wa taratibu Ofisi ya Rais TAMISEMI ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kadri ya taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye ni kuhusiana na barabara zinazohudumiwa na TARURA. Ni kweli Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini ina jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu ya barabara inapitika mwaka mzima. Wakala huyu ana mtandao wa barabara zipatazo kilometa 108,496 ambazo hufanyiwa matengenezo mara kwa mara na pale inapobidi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba bado bajeti ya TARURA haitoshelezi lakini Serikali imekuwa ikiongeza fedha mwaka hadi mwaka ili angalau kuendelea kuboresha utekelezaji wa wakala huyu. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bajeti ya TARURA ilikuwa shilingi bilioni 241, lakini kwa mwaka 2020/2021 bajeti ya TARURA ni shilingi bilioni 275 ikiwa ni ongezeko la takribani shilingi bilioni 34. Ni kweli Serikali inaona sababu ya kutafuta vyanzo vingine vya kuongezea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi na jambo hili linaendelea kufanyiwa kazi.

Name

Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI) aliuliza: - Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni Halmashauri mpya iliyotoka Wilaya ya Kilombero: - (a) Je, ni lini Serikali itaipa Mlimba hadhi ya kuwa Wilaya hasa ikizingatiwa umbali mrefu wa takriban Km 200 ambao Wananchi wanatembea kufuata huduma Makao Makuu ya Wilaya? (b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Halmashauri na kuboresha miundombinu ya barabara?

Supplementary Question 2

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba na mimi niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Sengerema ina halmashauri mbili, Halmashauri ya Sengerema na Halmashauri ya Buchosa. Mimi ni Mbunge wa Buchosa, wakati wa kampeni nilimuomba Mheshimiwa Rais Halmashauri ya Buchosa nayo iwe Wilaya. Kwa hiyo, naomba kujua ni lini sasa Buchosa nao watakumbukwa kuwa Wilaya? Halmashauri hii ina mapato makubwa, ni halmashauri inayojitosheleza na inafaa kabisa kuwa wilaya ili huduma ziweze kuwasogelea wananchi. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Erick Shigongo, Mbunge wa Buchosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kusogeza huduma za jamii karibu zaidi na wananchi na kuanzisha maeneo mapya ya utalawa. Ni sehemu ya kusogeza huduma kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Buchosa ambayo Mheshimiwa Shigongo anaielezea, naomba nimshauri kwamba utaratibu wa kuomba maeneo mapya ya utawala unafahamika na Ofisi ya Rais, TAMISEMI bado haijapata taarifa rasmi kutoka Mkoa wa Mwanza, ukihitaji kuomba Halmashauri ya Buchosa kuwa Wilaya. Kwa hiyo, naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge, wafuate utaratibu huo na Serikali itaona namna gani ya kulifanyia kazi suala hili. (Makofi)