Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO Aliuliza:- Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Muleba inazidiwa na wingi wa wateja kutokana na miradi ya REA. Je, ni lini Wilaya hiyo itapewa hadhi ya Mkoa wa TANESCO ili iweze kutoa huduma kwa wakati?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara, ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wakati wananchi wa Muleba wakisubiria hizi hatua ambazo Wizara inazichukua, je, Serikali iko tayari kuiongezea nguvu Ofisi ya TANESCO iliyopo kwa sasa kwa kuiongezea wafanyakazi na vitendea kazi ili wakati tunaendelea kusubiria iendelee kutoa huduma stahiki kwa wananchi wa Wilaya ya Muleba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Muleba inavyo visiwa 39 na kati ya hivyo, visiwa 25 vinakaliwa na wavuvi ambao wanachangia pato la taifa. Je, Wizara na Serikali ni lini itavipelekea umeme wa uhakika na wa bei nafuu?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO imeendelea kutoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha kwamba huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini kwamba tutaendelea kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi na kuhakikisha kwamba ofisi ya TANESCO Muleba lakini na maeneo mengine yote nchini zinafanya kazi vizuri kabisa. Serikali tayari imeshaongeza nguvu kazi katika maeneo mbalimbali kwa kupeleka watumishi na vifaa mbalimbali ikiwemo vitendea kazi na magari. Tunaahidi kwamba tutaendelea kuboresha utendaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, kama nilivyokuwa nimetangulia kusema kwamba miradi inayopeleka umeme visiwani ni miradi inayoitwa off grid, maeneo ambapo Gridi ya Taifa haijafika na Muleba ni mojawapo ya maeneo ambayo ina visiwa vingi vinavyokaliwa na watu vinavyohitaji kupata huduma ya umeme. Tayari wako watu ambao walikuwa wanapeleka umeme huko ikiwemo kampuni ya JUMEME lakini gharama yake ilikuwa ni kubwa na Serikali ilitoa maelekezo kwamba gharama hiyo ya unit 1 kwa Sh.3,500 ishuke na kufikia shilingi
100. Maelekezo hayo tayari yameshaanza kutekelezwa. Kama bado kuna tatizo katika maeneo hayo basi tunaomba taarifa hiyo itolewa ofisini ili tuendelee kusimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali inao mpango wa kufikisha umeme wa TANESCO katika maeneo hayo kwa kadri bajeti itakavyoruhusu au kuweza kusimamia ile miradi ili iweze kutoa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu kwa wananchi wote wanaoishi visiwani.