Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:- Kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika Hifadhi ya Mbuga ya Selous na sasa tembo na nyati wanavamia mashamba pamoja na makazi ya wanavijiji na kuleta taharuki:- Je, Serikali inaweza kuwarudisha wanyama hao porini mbali zaidi na wananchi?
Supplementary Question 1
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa jambo hili ni la dharura kwani kwa sasa wakulima wamelima, wamepanda, wamepalilia na kutia mbolea katika mashamba yao kwa thamani kubwa lakini makundi ya tembo yameingia na kuvuruga mashamba hayo na wakulima wamepata taharuki hasa baada ya mkulima mmoja kuuwawa na tembo hao. Je, Serikali inaweza sasa kupeleka kikosi maalum kufanya operation ya kuwaondoa na kuwafukuza tembo hao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili linasababishwa pia na makundi ya ng’ombe waliondolewa katika maeneo ya Mkoa wa Morogoro na kuingia katika maeneo ya hifadhi ya tembo hawa na kuharibu ecology yake na kufanya tembo hawa kufika kwa wananchi. Je, Serikali kwa kutekeleza azma ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika hotuba yake ukurasa wa kumi na sita hapa Bungeni kwamba itaongeza maeneo ya hekta kufika milioni sita…
SPIKA: Fupisha swali Mheshimiwa.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, Serikali imejipangaje kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza maeneo ya wafugaji ili kuondoa mgongano huu?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge la Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza ambalo amesema kupeleka vikosi kazi kwa ajili ya kwenda kushughulikia uvamizi wa tembo; Serikali ipo tayari na hata leo anavyowasilisha tayari Serikali ilishafanya mchakato wa kuhamisha hao tembo na inaendelea kuwaondoa katika maeneo hayo ya mashamba na shughuli za kibinadamu. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Kawawa, kwenye hili suala la uvamizi wa tembo katika maeneo yanayozunguka au ya kandokando ya hifadhi kwamba, Serikali ina vikosi ambavyo viko katika Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kutumia Jeshiusu inaendelea kuwaondoa hawa tembo na wanyama wengine wakali ili kuwawezesha binadamu kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kundi la ng’ombe kwamba wanahamia kwenye maeneo ambayo yamepakana na hifadhi; naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Vita Kawawa kwamba Kamati ya Mawaziri iliundwa na Serikali kuangalia maeneo yote yenye migogoro ikiwemo migogoro inayozunguka mipaka yote ya hifadhi. Sasa hivi Kamati hii ilishamaliza kazi yake na utekelezaji wake unaenda kuanza baada ya Bunge hili Tukufu kumalizika. Hivyo maeneo yote ambayo yana migogoro kama ya namna hii Serikali inakwenda kuyamaliza na niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa kwamba wote ambao wana changamoto hii inakwenda kumalizwa na maamuzi ya Kamati ya Mawaziri. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved