Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Primary Question

MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?

Supplementary Question 1

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali japo siridhiki nayo kwa sababu maeneo ya kujenga Hospitali ya Wilaya katika Jimbo la Mbinga Vijijini yapo mengi katika maeneo tofauti tofauti, ni uamuzi tu wapi tujenge hospitali hiyo. Je, Serikali inawahakikishia nini wananchi wa Mbinga Vijijini katika bajeti ijayo ikiwa bajeti mbili tofauti zimepangwa na hizi fedha hazikupelekwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mbinga Vijijini kwa kuunga mkono juhudi za Serikali wamejenga na kukamilisha zahanati sita; zingine zina miaka miwili toka zikamilike. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wahudumu katika zahanati hizi ili zifunguliwe zianze kuwahudumia wananchi?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, kigezo muhimu cha kupeleka fedha katika Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ambacho Serikali iliweka ilikuwa ni Halmashauri husika kuainisha eneo na kuwasilisha taarifa ya uwepo wa eneo husika ndipo fedha ziweze kupelekwa kwenye Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mbinga Vijijini imekuwa na mivutano ya muda mrefu kuhusiana na wapi Makao Makuu ya Halmashauri iwepo. Januari hii wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipopita ndipo ilipata majibu ya kuwa na Makao Makuu ya Halmashauri yawepo. Kwa sababu hizo, hawakuwa na eneo rasmi ambalo liliwasilishwa Serikalini na ndiyo maana fedha haikupelekwa. Hata hivyo, kwa sasa, kama nilivyosema kwa sababu wamekwishawasilisha eneo ambalo limetengwa, katika shilingi bilioni 27 ambazo zimetengwa na Serikali, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba watapata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na zahanati sita ambazo zimekamilika na hazijaanza kutoa huduma kwa sababu ya upungufu wa watumishi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kapinga kwamba Serikali inathamini sana kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mbinga Vijijini. Kwa sababu zahanati hizi zimekamilika tutakwenda kuona utaratibu mzuri kwanza kwa kutumia watumishi waliopo ndani ya halmashauri kufanya internal redistribution ya watumishi hao angalau kuanza huduma za afya. Katika kibali cha ajira kinachokuja Halmashauri ya Mbinga Vijijini tutawapa kipaumbele ili watumishi hao waweze kwenda kutoa huduma katika zahanati hizo.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?

Supplementary Question 2

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Kwa kuwa na sisi watu wa Makete tuna changamoto ya hospitali ya wilaya toka mwaka 1982 kituo cha afya kilivyopandishwa hadhi kuwa hospitali ya wilaya, hadi sasa hatuna hospitali ya wilaya. Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Makete itaanza kujengwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/2021, kiasi cha shilingi bilioni 27 kimetengwa kwa ajili ya kujenga hospitali za halmashauri zile ambazo ni chakavu, tutajenga hospitali za halmashauri mpya na Halmashauri ya Makete ni miongoni mwa halmashauri ambazo tutakwenda kutenga fedha na kuhakikisha kwamba ujenzi wa hospitali ya halmashauri unaanza.

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?

Supplementary Question 3

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza dogo, kwamba Jimbo la Ndanda lenye kata 16 lina Kituo cha Afya kimoja tu cha Chiwale. Hata hivyo wananchi wa Ndanda, Lukuledi, Panyani, Mihima pamoja na Chilolo walijitahidi kwa kutumia nguvu zao pamoja na nguvu ya Ofisi ya Mbunge kujenga maboma kwa ajili ya zahanati na mengine kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali kuhusu kuwapokea wananchi mzigo huu wa kukamilisha maboma haya ili yaweze kutumika na kutoa huduma za afya?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Ndanda kwa kujitolea nguvu zao na kuanza ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na hiyo ni kauli ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaibua miradi na Serikali inaunga nguvu miradi hiyo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka huu wa Fedha 2020/2021, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 27.75 ambazo zitakwenda kufanya kazi ya kuchangia nguvu za wananchi katika kukamilisha ujenzi wa maboma 555 nchini kote. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwambe kwamba jimbo lake na vijiji na kata husika zipo katika mpango huu na Serikali itahakikisha inatoa mgao kwa ajili ya umaliziaji wa vituo hivyo ili viweze kutoa huduma kwa wananchi.

Name

Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Primary Question

MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?

Supplementary Question 4

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile swali la msingi linalohusu Mbinga Vijijini linafanana kwa kiasi kikubwa na tatizo la Madaba na kwa vile Madaba ilishatengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kwa vile kwa miaka miwili mfululizo fedha hiyo haijatoka. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha Madaba ili ujenzi wa hospitali ya wilaya uanze?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri.

Katika kipindi cha miaka mitano sote tumeona kazi kubwa iliyofanyika kwa kujenga hospitali za halmashauri zaidi ya 101 na katika mwaka huu wa fedha, kiasi cha shilingi bilioni 27 zimetengwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vituo na hospitali za halmashauri ambazo zitajengwa Jimbo lake la Madaba pia litapewa kipaumbele.