Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali ila naomba yafanyike masahihisho. Ni Mji wa Mangaka, sio Banyaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo; la kwanza; kwa kuwa Mradi huu wa kuvuta maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Mji wa Mangaka unaanzia Kata ya Masuguru, unapita Nanyumbu, Chipuputa, Kilimanihewa hadi Sengenya ambapo matenki yatajengwa. Swali, je, vijiji vitakavyopitiwa na bomba hili vitanufaika vipi na mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunatambua kwamba mradi huu utachukua miaka miwili na wananchi wa Jimbo langu wana shida kubwa ya maji. Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwanusuru wananchi hawa wakati wanasubiri mradi kukamilika? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza, kwa sababu Mradi wa Ruvuma utapita kwenye hizi Kata tano alizozitaja, vijiji vitanufaikaje. Kama tunavyofahamu Sera ya Maji hairuhusu Kijiji cha B kianze kupata maji A kikarukwa. Nipende kusema kwamba vijiji vyote ambavyo mradi huu utavipitia, basi watapata maji kwa sababu lile bomba kuu litaruhusu michepuo kwa vijiji vile vinavyopitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ameongelea suala la muda mfupi. Mradi huu tunautarajia uchukue miezi 12 na tunatarajia uanze mwezi Mei mwaka huu. Mheshimiwa Mbunge hii kazi itafanyika kwa kasi kwa sababu tayari fedha zipo, hivyo itakuwa ni kazi ya muda mfupi na maji yataweza kuwafikia wananchi wetu kwa wakati. (Makofi)
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
Supplementary Question 2
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma, bado changamoto kubwa imebaki kuwa kukosekana kwa chanzo cha uhakika katika Mji wa Tunduma. Je, nini mkakati wa Serikali wa kutekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi ya kuvuta maji kutoka chanzo cha uhakika kilichopo katika Mji wa Ileje? Ahsante.
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha uhakika cha maji kwa Mji wa Tunduma kama alivyoongelea chanzo cha maji kutoka Ileje, feasibility study inaendelea kufanyika na mara itakapokamilika basi mradi ule utatengewa fedha kwa awamu na utekelezaji utaanza mara moja. Vile vile kwa nyongeza pale Tunduma nimeshafika na kuona namna gani bora ya kuweza kupatikana kwa maji kwa sababu miundombinu ya awali tayari ilikamilika Mheshimiwa Mbunge niseme tulishaweza kumpa maelekezo Meneja wa Maji Mkoa, RUWASA na yule Engineer ni Engineer ambaye tunamtegemea katika Wizara na anafanya kazi vizuri sana. Hivyo, nikuhakikishie shida ya maji katika Mji wa Tunduma inakwenda kuwa historia. (Makofi)
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
Supplementary Question 3
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Sisi Namtumbo kule tuna miradi ya maji yenye takriban miaka nane lakini bado haijakamilika na kuna changamoto ya ukamilifu wa miradi hiyo hasa vifaa na mabomba. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kuongozana nami kabla ya Bunge la Bajeti kwenda kuona miradi hiyo na changamoto yake na kuona ni jinsi gani atatuongezea nguvu ili kukamilisha miradi hiyo? (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa unataka kuongozana na Naibu Waziri au Waziri? Ni yupi uliyemwomba kati ya hao? (Makofi/Kicheko)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri. (Makofi/Kicheko)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyojibu maswali vizuri na nimpongeze na Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Kawawa kwa kazi kubwa anayoifanya Namtumbo. Kubwa mimi nipo tayari kuongozana naye. Mkoa wa Ruvuma pia ni moja ya mikoa ambayo tumeainisha hii changamoto ya maji na tumewapatia zaidi ya bilioni nane na katika wilaya yake tumeipa 1.3 billion katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Kwa hiyo, tunamtaka Mhandisi wa Maji, Namtumbo aache porojo, afanye kazi kuhakikisha wananchi hawa wanaweza kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
Supplementary Question 4
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri anajua Mradi wa Maji wa Bunda umetumia zaidi ya miaka 13, tayari maji yameshatoka Ziwa Victoria, kata saba za mjini wameanza kueneza mtandao wa maji na takriban milioni 300 zilienda. Ninachotaka kujua kama Mbunge senior wa eneo lile na kipenzi cha Wanabunda, ni lini Kata 14 zitapata maji safi na salama? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kuhusiana na Bunda mradi uliokaa kwa miaka 13 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji lengo letu ni kuona kwamba tunaleta mapinduzi makubwa sana kuona maji sasa yanakwenda kupatikana. Miradi hii ambayo miundombinu imekamilika bado maji hayatoshelezi, wataalam wanaendelea na kazi na tutahakikisha maji yanaenda kupatikana. Napenda kusema kwamba Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo alishafika kwangu mara kadhaa na suala hili tunakwenda kulitekeleza haraka. Ziara yangu baada ya hapa ni kuelekea ukanda huo, basi Bunda napo pia nitafika na maji yatapatikana. (Makofi)
Name
Anton Albert Mwantona
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rungwe
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
Supplementary Question 5
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kabla ya yote nipongeze sana Wizara ya Maji. Napongeza Wizara ya Maji, Naibu Waziri alikuja kwetu Rungwe Jimboni, ametembelea miradi, ameona matatizo ya maji kwa wananchi wa Rungwe. Naomba sasa niulize swali langu; je, ni lini mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Tukuyu utaanza kutekelezwa hasa baada ya Naibu Spika kutembelea na kutuahidi pale. Lakini pia upembuzi yakinifu ulishafanyika…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza swali.
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji mdogo wa Tukuyu tunafahamu kabisa miundombinu yake ni chakavu na idadi ya watu imeongezeka, tayari maelekezo yapo kwa Meneja wa Maji Mkoa wa Mbeya na ameshaanza manunuzi ya vifaa vya kazi na kufikia mwezi Machi kazi zitaanza kufanyika pale Tukuyu na upatikanaji wa maji unakwenda kuboreshwa. (Makofi)