Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 kwa kiwango cha lami ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi kati ya nchi yetu na Msumbiji?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama kwa namna ambavyo halali usiku na mchana anafuatilia kuona kwamba barabara hii inajengwa ili kuweza kuchochea uchumi wa wananchi wa maeneo husika Mkoa wa Ruvuma na Nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Ruvuma ni mkoa ambao umeshika nafasi ya kwanza mara tano mfululizo kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka. Wananchi wa maeneo hayo wanajishughulisha na kilimo, uzalishaji wa makaa ya mawe, soko la mazao la Kimataifa, lakini pia kuna shamba la miwa.
Mheshimiwa Naibu Spika…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najenga hoja. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kuwa kuchelewesha ujenzi wa barabara hii ni kuendelea kufanya udumavu wa maendeleo kwenye maeneo husika hasa kwa Mkoa wa Ruvuma na Jimbo la Peramiho na kwa nchi yetu kwa ujumla? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nafahamu kwamba Kamati ya Bajeti imetenga fedha shilingi milioni 110 kwa ajili ya kufanya usanifu wa ujenzi wa daraja, daraja ambalo limekwishajengwa, daraja la Mkenda. Je, ni kwa nini Serikali sasa isihamishe fedha hii shilingi milioni 110 ikaanze ujenzi wa barabara mara moja ili kuweza kuchochea uchumi wa maeneo husika? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii na kwa kutambua umuhimu wa uzalishaji ambao uko katika Mkoa wa Ruvuma lakini pia na makaa ya mawe; katika jibu langu la msingi tumesema barabara hiyo pia ni muhimu sana kwa ulinzi wa nchi yetu na pia ni moja ya vipaumbele vya nchi kuunganisha nchi na nchi na hii ni trunk road wala sio regional road. Ndiyo maana tayari barabara hii imeanza kutengewa fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Mbunge amenisikiliza vizuri, kulifanyika usanifu wa awali ambao wakati huo barabara haikuwa na matumizi ambayo inayo sasa hivi na ndiyo maana kukafanyika redesign yaani usanifu mpya kwa sababu tayari sasa kule kuna makaa ya mawe na mgari yaliyokuwa yanapita wakati ule wakati barabara inafanyiwa usanifu siyo ambayo sasa yanapitika. Kwa hiyo lazima lile daraja lifanyiwe usanifu mpya ili liweze kumudu shughuli ambazo sasa zitaweza kufanyika kwa maana ya kuwa na uwezo wa kuhimili magari ambayo yatapita na uzito wake hasa baada ya kugundua makaa ya mawe na kuongezeka kwa traffic kwenye hiyo njia. Ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Primary Question
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 kwa kiwango cha lami ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi kati ya nchi yetu na Msumbiji?
Supplementary Question 2
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, lakini pia swali hilo linafanana na hali ya kule Mufindi. Kwa kuwa Mufindi ni kitovu cha viwanda nchini na zaidi ya viwanda tisa viko pale na miundombinu imekuwa ni mibovu sana; na kwa kuwa barabara ya Nyololo - Mtwango na Mafinga - Mgololo zimeahidiwa kuanzia wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja na Rais Magufuli, zimeahidiwa na Mawaziri Wakuu, Mzee Pinda na Mzee Kassim Majaliwa, zimetajwa kwenye Ilani ya CCM karibu mara tatu…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuingiza kwenye bajeti barabara hizo? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara zote alizozitaja zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa sana ambao yanachangia fedha nyingi sana kwenye Mfuko wa Serikali na kama alivyosema barabara hizo zimeahidiwa na viongozi wengi wa Kitaifa, lakini pia barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizo kwa sababu ya umuhimu wake, kuanzia bajeti inayokuja zitaanza kutengewa fedha ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved