Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza :- Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Uhamiaji na cha Polisi kuhudumia maeneo hayo ya mpakani?

Supplementary Question 1

MHE. DAIMU IDDI MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jimbo la Tunduru Kusini lina tarafa tatu, Tarafa ya Nalasi, Lukumbule na Sakata na zote zimepakana na Mto Ruvuma, kwa ng’ambo ni Msumbiji, lakini katika Jimbo hilo Kituo cha Polisi kiko kimoja tu kipo kwenye Tarafa ya Nalasi peke yake. Swali la kwanza, je, Serikali haioni ni muhimu sana kwa sasa kukamilisha Kituo cha Polisi Lukumbule ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa mipakani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Lukumbule ni sehemu ambayo watu wengi wanapitia kwenda na kutoka Msumbiji katika harakati za kufanya biashara. Wananchi wa Msumbiji wakija Tanzania hamna mahali popote wanapopita tunawapokea kiurafiki, lakini sisi Watanzania tukienda Msumbiji tunakamatwa wanapigwa, wananyanyaswa na kunyang’anywa mali zao. Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuharakisha mazungumzo ya kuanzisha Kituo cha Uhamiaji katika kijiji au Makao Makuu ya Tarafa ya Lukumbule?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduru Kusini kulikuwa kuna vituo vitatu, Kituo cha Nalasi, Masuguru na Lukumbile lakini kwa bahati mbaya hiki kituo kimoja kilikuja kikatiwa moto baada ya kutokea machafuko ya wananchi. Hata hivyo, baada ya Serikali kuona umuhimu sasa wa kuwepo kituo ili sasa kuimarisha hali ya ulinzi pale, Serikali ikashusha Waraka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili sasa watusaidie kujenga kile kituo hili eneo la Lukumbile. Hivi ninavyokwambia tayari kituo kimeshaanza kujengwa na kimeshafikia katika hatua ya lenta. Sasa kikubwa tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tunaenda kutengeneza mazingira sasa ya kuona namna na kupitia umuhimu wa kuwepo kituo hiki ili sasa tuweze kuweka kituo hiki ili wananchi waweze kuishi katika mazingira ya usalama zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, hakuna Serikali yoyote duniani ambayo inapenda wananchi wake wapate tabu; wanyanyaswe, wapigwe, wadhulumiwe. Sasa kitu ambacho nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, kutokana na umuhimu wa suala hili tunakwenda kuona namna ambavyo tutakapotengeneza bajeti yetu hii Wilaya ya Tunduru hasa katika hii sehemu ambayo wanahitaji Kituo hiki cha Uhamiaji tutaipa kipaumbele ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata kituo cha uhamiaji hapa ili wananchi waweze kuepukana na huo usumbufu. Ahsante.