Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa daraja hili linaunganisha Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro na hivyo ku-facilitate kusafirisha mifugo pamoja na mazao ya kilimo kwenda mikoa mbalimbali kutoka mikoa ya Kati kwenda Kaskazini. Kwa kuwa kuwepo kwa daraja hili kutafupisha safari ya kutoka Kilimajaro kwenda Dodoma kwa kilometa 172. Kwa kuwa fedha zinazotengwa TARURA ni ndogo sana na haziwezi zikatosheleza ujenzi wa daraja hili kwa haraka. Je, Serikali, Wizara ya TAMISEMI, haioni kwamba umefika wakati sasa wa kushirikiana na TANROADS au Wizara ya Ujenzi kwa sababu imekuwa inafanya hivyo katika projects mbalimbali ili kuweza kunusuru wananchi katika maeneo mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wakati huu ni wakati wa amani na kwa kuwa Jeshi letu la Wananchi limekuwa linafanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa miundombinu, je, katika madaraja haya ambayo yametajwa na Waheshimiwa Wabunge asubuhi ya leo pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni kwamba inaweza kushirikisha Jeshi ili liweze kusaidia kujenga madaraja haya ili wananchi waweze kupita kwa urahisi na shughuli za uchumi zikaendelea vizuri? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Daraja hilo la Mto Pangani ni muhimu sana kwa sababu linaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro. Ni kweli kwamba bajeti ya kawaida ya kuhudumia Halmashauri ya Same haiwezi kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kubwa; na hivyo katika utaratibu wa Serikali kuna ujenzi wa taratibu za kawaida lakini pia kuna ujenzi maalum kwa maana ya kutenga bajeti maalum kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu korofi kama ilivyo daraja hilo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mbinu hizi mbili za matengenezo ya muda wa kawaida kwa maana ya utaratibu wa kawaida na matengenezo maalum hutumika pale ambapo madaraja yanahitaji fedha kiasi kikubwa kuliko bajeti ya halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili TARURA tumeendelea kushirikiana kwa karibu sana na TANROADS kuona namna bora ya kushirikiana ili daraja hilo liweze kupata suluhu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ushirikiano huu unaendelea vizuri na tunaamini kwamba katika mwaka wa fedha ujao tutakuwa tumefikia hatua nzuri ya utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Jeshi kushiriki katika kujenga madaraja hayo, mara nyingi Serikali katika madaraja ambayo yanahitaji ujenzi wa dharura kutokana na maafa mbalimbali kama mafuriko, sote tumekuwa mashahidi kwamba majeshi yetu yamekuwa yanafika na kufanya matengenezo hayo kwa haraka na kwa wakati ili kurejesha huduma kwa wananchi. Jambo hili litaendelea kutekelezwa kadri ya matukio hayo hayavyojitokeza.

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo Same Magharibi zinafanana sana na changamoto zilizopo Jimbo la Busokelo. Kata ya Ntaba tuna Daraja ambalo linaitwa Mto Ngubwisya, liliondolewa na maji tangu tarehe 30 Aprili, 2019 na daraja hili linaunganisha Kata za Kisegese, Itete, Kambasegera pamoja na Luangwa.

Je, ni lini Serikali inakwenda kujenga daraja hili ili wananchi wangu wa Busokelo waunganishwe kama ilivyokuwa zamani? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fredy Makibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba daraja hilo muhimu ambalo linaunganisha kata na vijiji mbalimbali katika Jimbo la Busokelo lilivunjwa na maji mwaka 2019. Serikali inatambua sana umuhimu wa kwenda kulifanyia tathmini na usanifu daraja hilo ili liweze kutengewa fedha kadri ya upatikanaji wa fedha na kuweza kujengwa ili liweze kurejesha huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Busokelo na Mheshimiwa Mbunge ili kuweza kuona namna gani usanifu unafanyika na fedha zinatafutwa na kujenga daraja hilo kadri ya upatikanaji wa fedha.

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:- Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?

Supplementary Question 3

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kabla barabara hazijajengwa tunatengeneza bajeti, tukishaipitisha ndiyo inaanza kutekelezwa. Wakati mwingine kuna miradi ambayo inatokana na majanga, mfano barabara imekatika ghafla na yenyewe haikuwa imetengewa fedha, lakini kila ukiomba fedha inakuwa ni maneno tu wala hazipatikani.

Sasa nataka kufahamu, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba tunapopata majanga kama madaraja yanapokatika, wa kutoa fedha za dharura ili kuyajenga kuliko hivi ilivyo sasa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa barabara zetu unatekelezwa kwa mujibu wa bajeti za Serikali. Pia unatekelezwa kwa mujibu wa mapato yanayopatikana kutokana na makusanyo mbalimbali ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kutenga bajeti na kuandaa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo lakini pia utayari wa Serikali kuhudumia majanga pale yanapojitokeza na kukata mawasiliano ni jambo ambalo linapewa kipaumbele sana na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba ni kupata taarifa rasmi kutoka katika jimbo lake kwa hiyo barabara na daraja husika ili wataalam wa TARURA katika eneo husika na ngazi ya Wizara tuweze kuona namna ya kufanya thamini na usanifu na kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kufanya ujenzi na marekebisho ya daraja husika.