Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kiswaga Boniventura Destery
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Primary Question
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu?
Supplementary Question 1
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Kwa kuwa bajeti inayoendelea sasa tuko robo ya tatu na Serikali ilitenga shilingi milioni 750, ni lini Serikali itazileta hizi fedha za bajeti ya mwaka huu unaoendelea ili tuweze kuendelea na ujenzi wa jengo hilo la Halmashauri? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa jengo hili ni la muda mrefu na Serikali imewekeza fedha nyingi za kutosha na ili ufanisi wa shughuli za Halmashauri uweze kwenda vizuri, je, mwaka huu wa fedha Serikali itatenga fedha za utoshelevu ili kuhakikisha kwamba jengo hili linakamilika na majengo mengine ambayo yako kwenye nchi hii? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu kwenye swali la msingi kwamba Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 imekwishatenga shilingi milioni 750 kwa ajili ya kufanya shughuli za umaliziaji wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Magu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Magu kwamba fedha hizo ziko katika hatua za mwisho za kutolewa ili ziweze kufikishwa katika Halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza shughuli hizo zilizokadiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na jengo hili kuwa la muda mrefu ni kweli na Serikali inatambua kwamba jengo hili lina muda mrefu tangu limeanza kujengwa, na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba linakamilika mapema iwezekanavyo na ndiyo maana katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha Serikali itatenga kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia moja kwa ajili ya jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatenga fedha hizo na zitafikishwa ili ziweze kukamilisha jengo hilo kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wananchi.
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Primary Question
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu?
Supplementary Question 2
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mtama tulipokabidhiwa Halmashauri hii na Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba ujenzi wa mjengo yake utaanza mapema na hivi karibuni Waziri Mkuu alifanya ziara Jimboni Mtama na kutuahidi kwamba hizi fedha za ujenzi zitakuja.
Sasa je, Serikali iko tayari kuanza kuleta hizi fedha hata kama ni kwa awamu ili ujenzi huu na ahadi ya Mheshimiwa Rais ianze kutekelezwa?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imedhamiria kuhakikisha inakamilisha au inaanza ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri zile mpya ambazo miongoni mwao ni Halmashauri hii ya Mtama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 80.42 zimetengwa na zitaanza kutolewa wakati wowote kuanzia sasa na taratibu zinaendelea ili zile Halmashauri ambazo kwanza zilipata fedha za kuanza ujenzi zipate fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo lakini zile ambazo zinahitaji kuanza ujenzi ziweze kupata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya utawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili katika mwaka wa fedha ujao pia Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha shughuli hizo za ujenzi wa majengo ya utawala zinakamilika. Kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mbunge wa Mtama, Mheshimiwa Nape kwamba Serikali inatambua uhitaji wa kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Nape hiyo ya Mtama na tutahakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved