Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaoshindwa mitihani kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini?
Supplementary Question 1
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango mzuri wa kuwawezesha wanafunzi hao ambao wameshindwa kufaulu mitihani ya darasa la saba na kidato cha tano, lakini ikumbukwe kwamba wanafunzi tunaowazungumzia ni wale ambao wazazi wao wameshindwa kulipa ada ya 20,000 na kwa maana hiyo Serikali imewapa elimu bila malipo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mafunzo maalum ya bure kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili wanafunzi hao ambao wanashindwa mitihani na wanarudi nyumbani na kuwa tegemezi kwa taifa waweze kupata mafunzo hayo na hatimaye waweze kujiajiri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunayo Idara ya Elimu ya Watu Wazima lakini idara hii haijafanya vizuri kwa muda mrefu. Kutokana na wahitimu kuongezeka sababu ya mpango wa elimu bila malipo nchini wanafunzi wengi wanahitaji kupata elimu hii ya ziada. Je, Serikali sasa ipo tayari kutoa elimu ya watu wazima bure ili kuwawezesha wanafunzi ambao wanashindwa mitihani ya kidato cha nne na darasa la saba kupita kwenye mfumo huu ambao siyo mfumo rasmi wa elimu nchini? (Makofi)
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani maswali yote aliyouliza Mheshimiwa Husna ni mapendekezo ambapo anapendekeza kwa jinsi yeye anavyofikiri. Kwa hiyo, naomba maswali hayo yote mawili kwa pamoja tuyachukue na tuweze kwenda kuyaongeza kwenye mipango pamoja na Sera yetu ya Elimu na kuweza kuangalia namna gani ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nikirejea swali la Mheshimiwa Mbunge na hasa ushauri wake, kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikuwa anafikiri kwamba Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii vingeweza pia kutumika kuwafundisha na kuwasaidia vijana kukuza ujuzi katika skills ambazo zinatumika kwenye mazingira husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba program hizo zinaendelea na Serikali imekwisha kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tutaendelea kutenga hiyo bajeti lakini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tayari tunavyo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, ambavyo mwezi huu wa nne vitaanza kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana, kuwasaidia vijana kuweza kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali, lakini asilimia kubwa ya malipo ya ujuzi huo yatagharamiwa na Serikali. Tutakwenda kuangalia vyuo vyote ambavyo vinaweza kutoa mafunzo hayo, tutafanya tathmini yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, kuona vile ambavyo vina uwezo wa kufanya kazi hiyo tutaendelea kuvijumuisha kwenye mpango na vitaendelea kutoa mafunzo hayo na kuwafikia vijana wengi wa Tanzania kwenye programu hiyo maalum ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaoshindwa mitihani kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu ya vyuo vya kati na vya chini ni kiungo muhimu katika ujenzi wa uchumi na kupunguza umaskini nchini. Kwa kuwa watoto wengi wanaosoma katika hivi vyuo vya chini ni wa maskini. Je, Serikali ina mpango gani wa ku-extend ule Mfuko wa Mikopo wa Elimu ya Juu ili hawa watoto wa maskini wanaotaka elimu katika vyuo vya chini waweze kupata mikopo?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu lakini siyo hawa wa level ya elimu ya kati. Tukiangalia gharama za vyuo hivi kwa mwaka, Serikali inachangia au inagharamia kwa kiasi kikubwa sana. Kwa Vyuo vyetu vya FDC ada yake ni Sh.250,000/= kwa wanafunzi wale wanaokaa bweni na Sh.145,000/= kwa wanafunzi wa kutwa lakini kwa vyuo vyetu vya VETA, vina gharama ya Sh.120,000/= kwa wale wanafunzi wa boarding na Sh.60,000/= kwa wale wanafunzi ambao wako day. Hata hivyo, tunarudi pale pale kulingana na wigo na bajeti ilivyo, nadhani Serikali tutaangalia kitu gani cha kufanya lakini mpaka hivi sasa Serikali inatoa ruzuku ya kutosha kabisa kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinakwenda na kuwapunguzia mzigo wananchi wa kulipa gharama hizi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaoshindwa mitihani kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini?
Supplementary Question 3
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne, wanafunzi wachache ambao hawajabahatika kwenda kidato cha tano wanaenda vyuo vya ufundi. Vyuo vya ufundi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanalipia ada ya Sh.60,000/= na Sh.120,000/= kwa wale wa boarding. Je, Serikali haioni haja sasa kuondoa ada pia kwenye vyuo vya ufundi ili kuwawezesha watoto wengi kuweza kupata ujuzi? (Makofi)
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya mwanzo kwamba Serikali inatoa ruzuku ya kutosha. Kwa hiyo, hili alilolileta Mheshimiwa Sima ni pendekezo, tunaomba twende tukalifanyie kazi tuweze kuangalia namna gani aidha kwa kupunguza au kwa kuondoa wakati huo huo tukiangalia wigo wa bajeti ya Serikali unavyokuwa.