Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Primary Question
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: - Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
Supplementary Question 1
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na malalamiko mengi ya wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu lakini hawapati hiyo mikopo; na mimi ni shuhuda kwa kuwaleta wanafunzi wa jimbo langu, kwenda Bodi ya Mikopo lakini hawakuweza kufanikiwa kupata Bodi ya Mikopo, zaidi ya wanafunzi 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali je, serikali ni lini itahakikisha kwamba wanafunzi wenye sifa hakika wanapata mikopo badala sasa takwimu zinaonesha wanapata lakini uhalisia hawapati mikopo hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa wale waliofanikiwa kupata mikopo, kwa maana ya ukimaliza umeweka kanuni ama utaratibu kwamba mwanafunzi akimaliza chuo kikuu mara tu baada ya kumaliza aanze kurudisha huo mkopo na baada ya miezi 24, kwa maana ya miaka miwili, asipoanza kurudisha huo mkopo mmeweka kanuni kwamba atatozwa riba ya asilimia 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali, kwa wanafunzi ambao hawajapata ajira na sasa ajira ni changamoto, pengine miaka mitano, mingine kumi, wengine 20 na wengine hawapati kabisa; Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wanawawezesha kwanza hao wanafunzi kuwa-link na mashirika na taasisi ili fedha zilizokopwa na wanafunzi hawa zisipotee? Ahsante.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye swali langu la msingi,, kwamba Serikali imekuwa ikitoa mikopo hii kwa walengwa na wale ambao wamefikia sifa hizo. Kwa hiyo nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge; lakini Serikali inaendelea kuboresha bajeti yake ya mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo yetu imepanda kutoka bilioni 427 kwa 2017/2018 mpaka shilingi bilioni 464 2020/2021; na mwaka ujao wa fedha tunatarajia kutoa mikopo hii kwa jumla ya shilingi bilioni 500. Kwa hiyo tunaamini katika kuongeza wigo huu wa bajeti tunaweza tukawafikia walengwa wengi na changamoto hii ya vijana wetu kukosa mikopo inaweza ikatatulika. Hata hivyo tunarudi palepale, kwamba vigezo vya uhitaji ansifa zeke lazima viziingatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili eneo la pili la hizi asilimia; na hili naomba tulibebe kwasababu yamekuwa ni malalamiko ya wanufaika wengi na ni malalamiko ya muda mrefu, tuweze kwenda kuliangalia na kufanya review halafu tutaleta hoja hapa katika Bunge lako Tukufu kwamba namna gani tunaweza kwenda kuzishughulikia hizi tozo ambazo zimekuwa ni kero.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la hawa vijana sasa la kuwa-link kwenye taasisi na maeneo mengine ya ajira ni kwamba, jukumu la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kutoa taaluma kwa vijana, sio jukumu lake kutafuta ajira kwa vijana. Sasa hili tunaomba tulibebe kama serikali tuweze kuangalia vijana wetu wanapomaliza namna gani tunaweza kuwa-link na maeneo mengine ya kuweza kupata ajira ili fedha hizi ziweze kurudishwa kwa haraka ili na wanufaika waweze kuwa wengi zaidi. Ahsante.
Name
George Ranwell Mwenisongole
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbozi
Primary Question
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: - Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
Supplementary Question 2
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Mimi ningependa kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa nini Serikali isipunguze riba kwa hao wanaolipa deni lote kwa mkupuo kwa wakati mmoja ikatoka asilimia kumi au asilimia mbili au tatu au na vile vile kupunguza- retention fee ambayo ni kubwa na haipo kwenye mkataba wanaojaza wakati wa kukopa? Ahsante.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu yaliyopita, kwamba tunaenda kufanya review ya tozo hizi pamoja na riba na kuweza kuangalia namna gani tunaweza tukazipunguza au kuziondoa kulingana na uhitaji kutokana na malalamiko yaliyopo.
Name
Ndaisaba George Ruhoro
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Primary Question
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: - Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
Supplementary Question 3
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko kundi kubwa sana la wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wanakosa mkopo licha ya kuwa na sifa zote alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, na baada ya kukosa mkopo hupitisha bakuli maeneo mbalimbali wakichangisha fedha na wanabahatika kwenda vyuo vikuu lakini baadaye wanakatisha masomo yao kwa kushindwa kupata fedha za kuendelea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatambua wanafunzi hao ambao wame-drop out na kuweza kuwasaidia ili waweze kuhitimisha elimu yao na kufikia ndoto zao? Ahsante.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali kwamba Serikali tunaendelea na kuongeza wigo wa bajeti ili kuweza kuwafikia walengwa wengi zaidi. Kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, katika mwaka 2020/2021 waliojaza fomu ni zaidi ya 66,000 lakini tulioweza kuwapa mikopo ni 55,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, jawabu kwamba kuna zaidi ya wanafunzi 11,000 ambao walikidhi vile vigezo lakini hatukuweza kuwapa. Majawabu ya Wizara kupitia Serikali tunakwenda kuongeza wigo wa bajeti ili kuweza sasa kuwafikia walengwa wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza hapo mwanzoni kwamba bajeti yetu ya mwaka 2017/2018 ilikuwa ni bilioni
427. Bajeti ya 2020/2021 ilikuwa 464, lakini bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 inakwenda kuwa bilioni 500. Tunaamini kwa kadri tutakavyokuwa tunaongeza bajeti yetu itaweza kuwafikia walengwa wengi na vijana wetu wengi wataweza kunufaika na mikopo hii.
Name
Halima James Mdee
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: - Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
Supplementary Question 4
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikijinasibu kwamba mikopo hii inalenga kusaidia watoto wa familia maskini lakini kimsingi mikopo hii inakuwa ni mzigo kwa watoto wa familia maskini. Muuliza wa swali msingi amezungumzia asilima 15 ya makato kila mwezi, amezungumzia asilimia 10 ya interest rate kwa watu ambao ndani ya miezi 24 wameshindwa kulipa, kuna asilimia 6 ya interest kwa watu ambao wanalipa. Sasa matokeo yake ni kwamba badala ya kuwa ni mkopo wa kusaidia watoto unakuwa ni mkopo wa kibiashara.
Sasa ni lini Serikali italeta hapa Bungeni mabadiliko ya kisheria ili kile kinachosemwa kusaidia watoto maskini kithibitike kwa maneno na kwa vitendo na isiwe lugha za kisiasa?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, katika urejeshaji wa mikopo hii mnufaika anapaswa kukatwa asilimia 15 katika gross salary yake ambayo makato haya yalipitishwa katika Bunge lako hili Tukufu. Lakini vilevile kuna hizo alizozitaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hiyo asilimia 10 kwa wale watakaochelewa na asilimia sita.
Lakini kama nilivyojibu katika maswali ya nyongeza yaliyopita, kwamba tunakwenda kufanya review ya kanuni hizi na kuweza kuangalia namna gani tunaweza aidha kuondoa au kupunguza. Kwa hiyo, tunaomba tuachie ili jambo hili tukalifanyie kazi; na tuwe watulivu ili kuhakikisha mikopo hii haiendi kuwa kero kwa watumishi wetu maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza na mpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa maswali mengi ambayo yameelekezwa na ameyajibu kwa ufasaha. Jambo dogo tu nilikuwa nataka niweke kumbukumbu ili kwenye Hansard ikae vizuri.
Nilikuwa nataka tu kueleza kwamba, katika mkopo wa mwanafunzi analipa asilimia sita kama tozo ya kutunza thamani, lakini hakuna riba ya asilimia 10 kama ambavyo ilikuwa imeelekezwa, na hiyo asilimia 6 ndiyo hiyo ambayo tunaifanyika kazi. Nilikuwa ninaomba kumbukumbu zikae vizuri. Asilimia 15 ni makato ya mshahara kila mwezi, lakini ile riba iliyokuwa inatajwa ya asilimia 10 niombe niweke kumbukumbu vizuri hiyo haipo. Ahsante sana.