Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jerry William Silaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Primary Question

MHE. JERRY W. SILAA Aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya sasa ya kurejesha mfumo wa TANePS Hazina ili ukatekelezwe na kusimamiwa pamoja na GePG katika kuongeza ufanisi?

Supplementary Question 1

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakubaliana na Serikali kwamba kifungu cha 9 (1)(j) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kinaipa mamlaka PPRA kufanya kazi nyingine ikiwemo ya kuandaa mifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kwamba mfumo huu wa TANePS umeandaliwa na wataalam wa nje kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia; lakini atakubaliana na mimi, kwamba Serikali kupitia wataalam wa ndani kupitia Wizara ya Fedha imeandaa mifumo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ukiwepo huu wa GPG, MUSE na GSPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Juzi tumeona Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, ameonesha nia ya kuitaka serikali kuwa na mifumo michache ili kuongeza ufanisi.

(i) Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuwa na mifumo mingi kwenye taasisi nyingi itaendeleza urasimu badala ya ufanisi?

(ii) Kwa kuwa mfumo huu ukiuangalia na kwa language iliyoandikwa na wataalam hao wa nje haikuzingatia business concept ya nchi, yetu na mfumo huu umekuwa na matatizo mengi, hata siku mbili zilizopita mfumo huu ulikuwa chini na kuleta matatizo makubwa kwenye manunuzi.

Je, haoni kwamba ni wakati muafaka sasa kupitia kurugenzi yetu ya taarifa za mifumo ya fedha pale Hazina tutapunguza gharama kwa ku-integrate mfumo huu na mifumo ambayo nimeitaja hapo juu? (Makofi).

Name

Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Silaa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfumo wa TANePS tayari umeshaunganishwa na mifumo mingine ya GPS na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya serikali ikiwemo mifumo ya MUSE nakadhalika ili kupunguza gharama za uendeshaji Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Slaa, ni kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya juzi alipokuwa akipokea taarifa za CAG; kuhusu kuunganisha mifumo ya malipo yote ya Serikali ili kubaki na mifumo michache ili kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa hivyo, Mheshimiwa Rais amesema kwamba tuwe na mifumo michache ambayo inaweza kuendesha Serikali na kupunguza gharama za Serikali ili kuondoa usumbufu na upotevu wa fedha za Serikali. Ahsante. (Makofi)