Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jesca Jonathani Msambatavangu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa kimkakakti wa machinjio Iringa Ngelewala ili kuwekezaji huo uanze kuleta tija kwa Taifa?
Supplementary Question 1
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, kwanza nawashukuru kwa namna ambavyo wameweza kulifanyia kazi suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza ni kwamba je, Wizara inajipanga vipi sasa kuandaa wataalam ili tarehe 1 Agosti tutakapokuwa tumekamilisha mradi huu uweze kuanza kazi mara moja, kwa kuwa mradi wenyewe ni wa muda mrefu; na kwa kuwa tumewekeza fedha nyingi pia, isije kukosa wataalam tukaacha tena, ikakaa muda mrefu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ina-coordinate vipi na Wizara nyingine, kwa sababu hali ya kwenda kule kwenye machinjio yetu, pamoja na miundombinu tuliyoiweka, bado kuna changamoto kubwa sana ya barabara. Tunaomba hilo pia Wizara watuhakikishie wata-coordinate vipi kwa kuwa ni mradi wa kimkakati? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunafahamu machinjio hii imekaa muda mrefu na ndiyo maana nimeeleza kwamba fedha ambazo zimetengwa zitakwenda kukamilisha ujenzi ifikapo mwezi Agosti, 2021. Hata hivyo, kipaumbele ambacho kimewekwa, moja ni kuhakikisha kwamba vifaa vinavyohitajika kuiwezesha machinjio ile kufanya kazi vizuri pamoja na watendaji kwa maana ya watumishi, wataalam wanaohitajika ni kipaumbele cha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utekelezaji wa mradi huu unakwenda sambamba na ukamilishaji wa majengo na mipango ya kuhakikisha kwamba tunapata vifaa kwa ajili ya kuhakikisha machinjio inafanya kazi vizuri na kuhakikisha kwamba watumishi wanapatikana ili huduma ziweze kuendelea. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mambo haya yote yako kwenye mipango yetu na tutahakikisha inapokamilika, inaanza kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na barabara, ni kweli ni lazima eneo lile lifikiwe vizuri na barabara kwa sababu tunafahamu machinjio ile ni ya kisasa na lengo letu ni kuboresha huduma katika jamii na kuwezesha Manispaa kupata mapato mazuri. Tutakwenda kuhakikisha tunashirikiana kwa karibu sana na TARURA ili kutenga bajeti ya kuhakikisha kwamba barabara ile inafikika. Barabara hii kama inahudumiwa na TANROADS pia tutawasiliana kwa karibu ili iweze kujengwa, ifike pale ili kuboresha huduma hizo.
Name
Stanslaus Shing'oma Mabula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa kimkakakti wa machinjio Iringa Ngelewala ili kuwekezaji huo uanze kuleta tija kwa Taifa?
Supplementary Question 2
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali inasisitiza Halmashauri zetu ziweze kujitegemea na kukusanya mapato kwa wingi; Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo kwa sasa haina machinjio ya uhakika, imetumia fedha za ndani kukarabati pamoja na wadau machinjio ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 200 peke yake na mahitaji ni takribani ng’ombe 800 kwa siku.
Je, Serikali iko tayari sasa kuipa Halmashauri ya Jiji la Mwanza fedha kwa ajili ya kununua mashine zitakazowekwa kwenye mashine mpya ili iweze kufanya kazi, kutoa ajira na kuzalisha mapato kwa wingi? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imewezesha ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Jimbo la Nyamagana kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma katika jamii na kuiwezesha Halmashauri kupata mapato ya kutosha ili iweze kugharamia shughuli za maendeleo katika Jimbo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pamoja na kukamilika kwa machinjio ile, bado haijaweza kutumika ipasavyo kuchinja ng’ombe kwa uwezo wake; na kwa sasa inachinja ng’ombe 200 kati ya mahitaji ya ng’ombe 800 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumelichukua. Naomba tukalifanyie kazi ili tuweze kuweka mpango wa kuiwezesha machinjio ile kupata vifaa vya kutosha ili iweze sasa kutoa huduma kwa uwezo unaostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tutalifanyia kazi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved