Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kenneth Ernest Nollo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Primary Question
MHE. KENNETH E. NOLLO Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa GoTHOMIS kwenye zahanati kama ilivyo kwenye vituo vya afya ili kuondoa mwanya wa upotevu wa mapato?
Supplementary Question 1
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, swali langu la msingi lilikuwa ni kwamba mfumo huu umeshafika kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kwenye zahanati 400, lakini tunajua nchi hii ina vijiji takribani 12,000, kwa maana hiyo na zahanati hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la msingi ni kwamba zahanati nyingi sasa hawawezi kukusanya kwa kutumia ule mfumo na kinachotokea ni kwamba kunakuwa na upotevu wa mapato. Sasa swali langu la msingi ni je, Serikali haioni kwamba tutumie mfumo wa kawaida wa makusanyo ya kawaida (POS) ili tutoke kwenye upotevu ambao unaendelea sasa hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa dawa, hasa kwa watu wanaotumia CHF, kichecheo kikubwa imekuwa fedha za papo kwa papo, na hiyo inatokana na hii ya kwamba kuna upotevu wa fedha ambazo sasa mtu anakuwa analipa lakini fedha hazionekani.
Kwa hiyo, swali langu liko hapo, kwamba ni namna gani Serikali sasa inakuja kwamba ikiwezekana sisi tutumie POS kwa ajili ya kukusanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili Mheshimiwa.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, connection kidogo, mfumo huu unatumia milioni 14 ku- install…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili ya nyongeza, na ndiyo yanayoruhusiwa.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa mapato, matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi lakini pia takwimu za huduma za afya katika vituo vyetu kwa kufunga mifumo ya GoTHOMIS. Na ni kweli kwamba bado kuna zahanati na vituo vya afya ambavyo bado havijafungwa mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Nollo kwamba kazi hii ya kufunga mifumo katika zahanati zetu ni endelevu. Kama ambavyo tunafahamu, hatujamaliza kujenga zahanati kwenye vijiji vyetu, na wala hatujamaliza kujenga vituo vya afya katika kata zetu lakini pia Hospitali za Halmashauri katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo automatically tutaendelea kutekeleza ufungaji wa mfumo huu katika vituo vipya ambavyo vinaendelea kujengwa lakini pia katika vile vituo ambavyo bado havijajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kutumia mfumo wa POS halitatuwezesha kuboresha huduma za afya, kwa sababu lengo la mfumo wa GOT-HOMIS ni kuwa na taarifa za uhakika za magonjwa, matumizi ya dawa, aina ya matibabu yanayotolewa katika vituo. Kwa utaratibu huo hatuwezi kupata taarifa hizo kwa kutumia mashine za POS. Kwa hiyo naomba nimuhakikishie kwamba kama nilivyotangulia kusema tumeshafunga katika vituo 921 nchini kote, na kila mwaka wa fedha tunaendelea kufunga mifumo hii na tutaendelea kufunga ili viendelee kutoa huduma bora zaidi za afya katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali pili, changamoto ya upatikanaji wa dawa kwa baadhi ya vituo. Ni kweli Serikali imeendelea sana kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyetu vya huduma. Ukilinganisha hali ya upatikanaji wa dawa mwaka 2015 na 2020/2021 tumepanda kutoka wastani wa asilimia 75 kwa dawa muhimu mpaka wastani wa asilimia 80 hadi asilimia 85 kwa dawa muhimu. Lengo la Serikali ni kufika angalau asilimia 95 kuelekea asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge; kwamba sisi ni sehemu ya Madiwani katika Halmashauri zetu, sisi ni wawakilishi wa wananchi katika Halmashauri zetu. Tuendelee kushirikiana na Serikali kusimamia ukusanyaji wa mapato ya uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu na kuhakikisha dawa zile kama ambavyo Serikali tunasimamia kwa karibu zinatumika na kuwafikia wananchi wote wakiwepo wanachama wa CHF. Kwa hiyo naomba nimuhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili litaendelea kuboreshwa.
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KENNETH E. NOLLO Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa GoTHOMIS kwenye zahanati kama ilivyo kwenye vituo vya afya ili kuondoa mwanya wa upotevu wa mapato?
Supplementary Question 2
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto ya upatikanaji wa dawa haiko kwenye zahanati na vituo vya afya peke yake bali hata katika Hospitali za Rufaa. Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa Hospitali ambazo zinachangamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa; na hii inatoka na…
NAIBU SPIKA: Swali, swali!
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA:…je? Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiwango cha dawa katika Hospitali ya Rufaa ili iweze kuwapatia wananchi wa Tabora huduma iliyobora ya dawa? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tunafahamu kwamba pamoja na uboreshaji wa upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu katika Hospitali za Halmashauri na Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora kwa maana ya Kitete bado tunachangamoto ya upungufu wa dawa baadhi ya vituo. Ndio maana Serikali imeendelea kwanza kuongeza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba kila mwaka. Kwa mfano kwa miaka mitano iliyopita tulikuwa na bilioni 30 sasa tuna bilioni takribani 270. Pili, tumeendelea kuboresha sana ukusanyaji wa mapato ya fedha za uchangiaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kwanza tunapunguza utegemezi wa vituo vyetu kwa bajeti ya Serikali Kuu kwa kuviwezesha kukusanya vizuri mapato ya uchangiaji lakini pia kununua dawa na vitendanishi vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Hawa kwamba jambo hili Serikali tunalichukua, na tumeweka mpango mkakati wa kwenda kuboresha upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu, zikiwezo Hospitali za Rufaa, ikiwepo Hospitali ya Kitete. Nimhakikishie kwamba tutahakikisha kadri ya bajeti na taratibu ambazo zimepangwa tunaboresha sana upatikanaji wa dawa kwa wananchi wa Tabora na katika Hospitali ya Kitete na nchini kote kwa ujumla.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved