Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itasambaza umeme katika Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo?
Supplementary Question 1
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kunipatia niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kata hizi ilikuwa zipatiwe umeme REA awamu ya pili, lakini mpaka tunamaliza REA awamu ya pili kata hizo hazijapatiwa umeme. Je, Serikali inawahakikishiaje watanzania wa Wilaya ya Chemba kwenye kata hizi nilizozitaja, kwamba kwenye awamu hii ya REA awamu ya tatu iliyoanza Machi, 2021 kwamba vijiji hivi na kata zake hazitakwenda kukosa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ukatikaji wa umeme kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Chemba na kwenda kusababisha uharibifu wa mali za watumiaji wa umeme. Je, Serikali sasa haioni ni wakati wa kuanza kulipa fidia kutokana na tatizo la ukatikaji wa umeme bila taarifa? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe tamko la Serikali kwa niaba ya Serikali, kwamba tunawahakikishia wananchi wote wa Tanzania kwamba vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijapata umeme vilivyoko katika kata pamoja na hivyo alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge kwamba vitapelekewa umeme katika awamu ya pili ya mzunguko wa tatu wa REA, bila kuacha kijiji hata kimoja. Hiyo ni commitment ya Serikali na tayari mradi umeanza na vijiji vyote vilivyokuwa vimebakia takriban 1,900 vimechukuliwa katika mradi huu na vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa naibu Spika, timekuwepo changamoto kadhaa katika awamu zilizotangulia na zile baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yamebaki katika awamu hii ya tatu mzunguko wa pili hakuna hata kimoja kitakachobaki; na hiyo ni commitment ya Serikali. Kwa hiyo Mheshimiwa namuhakikishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chemba Mheshimiwa Monni amekuwa naye mstari wa mbele katika kufuatilia umeme wa wananchi wake; na sisi kama Wizara na Serikali tutahakikisha kwamba tunapeleka umeme katika mazingira hayo kwa kushirikiana na Wabunge wa maeneo yote. Ndio maana sasa swali lililoulizwa limejibiwa lakini pia na wengine wanaendelea kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali la pili alizungumiza kuhusu kukatika kwa umeme na nizungumzie katika eneo la Chemba. Yapo matatizo ambayo yanapelekea umeme kukatika; na kwa eneo la Dodoma tunalo tatizo moja kubwa sana. Udongo wa Mkoa wetu wa Dodoma ni udongo tepetepe inaponyesha mvua, kwa hiyo nguzo zimekuwa zikianguka na kulala panapokuwa panatokea hali ya hewa yenye mvua nyingi na udongo kuwa tepetepe. Na katika kulitatua hilo tumehakikisha basi tumeanza kuweka vitu vinavyoitwa concrete poles ambazo ni nguzo za zege zinaweza kwenda chini zaidi na zitahimili mzingo kwa sehemu kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa Jimbo la Chemba umeme unaokwenda Chemba unaenda katika sub-station yetu ya Babati unapita Kondoa, unakwenda Chemba, unakwenda Kiteto, unakwenda mpaka Kilindi, kwa hiyo ni parefu sana. Kwa Mkoa wa Dodoma imeamuriwa kwamba zijengwe sub-station nne zinazoitwa ring circuit ambazo zitakuwa zikiuzunguka mji wa Dodoma na zitapunguza mahitaji ya umeme kwenye msururu mrefu. Kwa mfano kutoka Kondoa kwenda Chemba kuna kilometa kama 30. Sasa ile Kiteto na Kilindi zitaondolewa kwenye mstari huu ili umeme unaokwenda Chemba uwe wa uhakika na uuhudimie wale wananchi walioko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekuwa tukiwaelekeza wenzetu waendelee kutoa taarifa kwa wananchi wao ili waweze kupata taarifa kwamba umeme utakatika na wajiandae kwa mazingira kama hayo.
Name
Mohamed Lujuo Monni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itasambaza umeme katika Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo?
Supplementary Question 2
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita Waziri wa Nishati alitembelea Kituo cha Afya cha Makorongo na kwa sababu ya umuhimu wa Kituo kile cha Afya alielekeza umeme uwekwe. Kituo kile kinahudumia Kata tano lakini mpaka leo hii kituo kile hakijapata umeme. Naomba sasa kujua, ni lini Wizara itatekeleza agizo lile la Waziri wa Nishati na Madini? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Waziri yalitakiwa yatekelezwe na kwa vyovyote vile yatakuwa katika hatua za utekelezaji kwa sababu uunganishaji wa umeme siyo jambo la siku moja. Naomba tulichukue na tukalifanyie kazi na kuhakikisha katika muda mfupi umeme unawashwa katika Kituo hicho cha Afya kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itasambaza umeme katika Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo?
Supplementary Question 3
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata 29 za Wilaya ya Mbozi, Kata tatu za Bara, Kilimpindi na Nyimbili bado hazijapelekewa umeme. Naomba kufahamu ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo? Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kuhusu kupeleka umeme katika kata alizozitaja katika Jimbo la Mbozi. Katika Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili wa REA iliyoanza Machi tutahakikisha tunapeleka umeme maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata umeme. Hivyo na yeye atakuwa mmojawapo kati ya wale watakaopata umeme katika awamu hii.
Name
Daimu Iddi Mpakate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itasambaza umeme katika Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo?
Supplementary Question 4
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tunduru Kusini lina matatizo makubwa sana ya umeme hasa vijiji vyake zaidi ya asilimia 70 bado havijapata umeme. Je, ni lini Mradi wa REA Awamu ya Tatu B utaanza katika Jimbo la Tunduru Kusini?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru kwa kusema ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili inazo jumla ya Lot 37 za kupelekeza umeme katika maeneo yetu ya vijiji. Katika hizo Lot 37, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tayari maeneo yote yaliyotakiwa kupelekewa umeme ambayo hayakuwa na umeme yamechukuliwa katika hizo Lot 37 na tayari tumeshazindua kuanzia Machi 15, pale Manonga na tunaendelea kuwatuma wakandarasi kuripoti katika maeneo yetu husika.
Mheshimiwa Natibu Spika, nikumbushie tu, agizo ambalo tumeshalitoa kwamba wakandarasi wote wanaenda kupeleka umeme katika maeneo hayo pamoja na maeneo mengine watakayopiga ripoti. Wapige ripoti kwa Waheshimiwa Wabunge ili kuwaonesha maeneo ambayo yanahitaji umeme kwa haraka na kwa ufasaha zaidi ili kuweza kushirikiana kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, itapunguza yale maswali ambayo tunaulizwa kwa sababu Waheshimiwa Wabunge watakuwa wamepata uhakika kwamba katika eneo lake mkandarasi anafika. Kwa hiyo, niwasisitize wakandarasi wafike katika maeneo ya Waheshimiwa Wabunge na kutoa taarifa ili Waheshimiwa Wabunge wapate hiyo taarifa na sasa kazi iweze kuendelea vizuri.