Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Janejelly Ntate James
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JANEJELLY J. NTANTE Aliuliza:- Serikali inawahimiza watumishi kujiendeleza kielimu, lakini baada ya kuhitimu wanapoomba kubadilisha kada huteremshwa vyeo na mishahara:- Je, Serikali haioni ipo haja ya kuwaacha na mishahara yao ili kujiendeleza isiwe adhabu?
Supplementary Question 1
MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa kwa sasa hivi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuboresha maisha ya watumishi lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hivi Serikali haioni kumshusha mtumishi mshahara ni mojawapo ya adhabu apewazo anapokuwa na utovu wa nidhamu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali mtatoa tamko la kwamba hawa watumishi wanaofanyiwa recategorization mishahara yao ikiwa chini ya vyeo vile wanavyoenda kuanzia watabaki na mishahara yao?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nianze kusema siyo adhabu kumshusha mshahara mtumishi ambaye ametaka kubadilishiwa kada yaani recategorization kwa job satisfaction kwa sababu bila kufanya hivyo utakuta mwalimu tayari alikuwa ameshapanda daraja juu na sasa ameomba kuwa Afisa Sheria, natolea mfano, ni lazima aende kuwa Afisa Sheria Daraja la II, entry point ili kutengeneza seniority katika eneo la kazi. Bila ya kufanya hivyo, tunaweza tukawa tunawabadili kada watumishi anakwenda katika idara husika anakuta tayari kuna watumishi wengine waliotumikia kada hiyo miaka mingi yeye akaenda kuwa senior zaidi yao kwa sababu tu alishatumikia cheo kingine na kada nyingine. Kwa hiyo, kwa ajili ya kulinda hiyo seniority ni lazima aende katika entry point ya kazi ile aliyoiomba.
Mheshimiwa Spika, lakini akiwa ametumikia cheo kikubwa zaidi kwingine atahamia kule na mshahara binafsi ataombewa na mwajiri. Akiombewa mshahara binafsi atabaki nao kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba baada ya kufikia cheo sasa tuchukulie Afisa Sheria labda kafika kuwa Principal basi atalipwa mshahara ule wa Principal na ataacha mshahara wake wa mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, utumishi wa umma unaongozwa kwa sheria, taratibu na kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa. Kwa wale wote ambao wanastahili kufanyiwa recategorization ni wajibu wa waajiri kwanza kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya recategorization. Mbili, ni wajibu wa mwajiri kumfanyia recategorization huyo mtumishi na kumwacha na mshahara binafsi endapo kada yake ni ileile ambayo amejiendeleza nayo. Hili si ombi ni kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge kama kuna mifano maeneo mengine Waziri wangu pamoja na mimi mwenyewe tuko tayari kwenda kuweza kuwashughulikia hawa Maafisa Utumishi na waajiri ambao hawatekelezi sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nihitimishe kwa kusema hivyo, nashukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved