Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Primary Question
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita? (b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
Supplementary Question 1
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba kumshukuru pia Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amekiri Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mahitaji halisi ya watumishi ni 469 na tulionao ni 162 na mwaka huu wakati Serikali imeajiri ilipeleka watumishi 20 wakati huo huo tunazo tayari zahanati 24 zimekamilika ambazo zimekuwa hazifanyi kazi. Sasa swali langu la msingi lilikuwa ni lini Serikali itahakikisha inapeleka watumishi wa kutosha ili zahanati hizo ambazo tayari zimekwishajengwa ziweze kufanya kazi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala ya TAMISEMI katika ziara tumethibitisha kwamba hospitali na zahanati ambazo zimefungwa mifumo ya ukusanyaji mapato zinapata pesa nyingi na zinafanya vizuri Zaidi. Kwa nini Serikali haioni jambo hili linaweza kuwa la kipaumbele ili maeneo ambayo yana network jambo hili likafanyika kwa haraka kuliko kuzungumzia zahanati zaidi ya 20 kutenga milioni 20?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Constantine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Geita na kama ambavyo nimetangulia kujibu kwenye swali la msingi kwamba Serikali inatambua upungufu huu na ndio maana kwenye ajira zilizopita moja ya halmashauri ambazo zilipata kipaumbele cha kuwa na watumishi wa kutosha ni Mji wa Geita. Lakini kwenye ajira zinazofata naomba nimhakiksihie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutoa kipaumbele cha kutosha kwa Mji wa Geita ili tuweze kupunguza pengo hili kubwa la watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Spika, pili ni kweli kwamba mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki ambao ni mfumo uliobuniwa na Serikali yetu wa GOT- HOMIS umeboresha sana mapato ya uchangiaji wa huduma za afya na mpango wa Serikali pamoja na kuelekeza halmashauri kuhakikisha zinatenga fedha za mapato ya ndani kufunga mifumo hii kwenye zahanati, vituo vya afya na ustawi za halmashauri tumeongea na wadau ili kuweka mkakati ambao utakuwa na muda maalum wa kuhakikisha tunashirikiana nao kufunga mifumo hii maeneo yote ambayo inaweza ikatumika na kuboresha mapato. Kwa hivyo suala hili tumelichukua kwa utaratibu huo pia wa kuweka mkakati maalum kabisa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kulitekeleza, nakushukuru sana.
Name
Halima James Mdee
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita? (b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
Supplementary Question 2
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, upungufu wa vifaa tiba ulioko Geita upo vilevile kwenye hospitali nyingi kama sio zote za wilaya, za mikoa, rufaa katika kukabiliana na janga la Covid - 19 hususan mitungi ya oxygen wananchi wengi wanakufa kwa kukosa mitungi ya oxygen. Sasa nilitaka Serikali iniambie wana mkakati gani wa dharura wa kuhakikisha hospitali hizi zinapata mitungi ya oxygen ili wananchi wenye uhitaji wa oxygen wasife kwa kukosa oxygen?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima James Mdee Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu wa baadhi ya vifaa tiba katika vituo vyetu na hospitali zetu za kutolea huduma za afya na Serikali katika mida tofauti na katika bajeti tofauti imeendelea kuweka mikakati ya kutosha kwanza kwa kuongeza sana bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba. Kwa mfano katika miaka mitano iliyopita mpaka sasa tumeongeza bajeti kwa zaidi ya mara tisa kutoka bilioni 30 mpaka bilioni 270.
Mheshimiwa Spika, lakini tunatambua kwamba kweli bado kuna changamoto ya vifaa tiba na hususan mitungi ya oxygen kama ulivyotamka na tumeweka mpango mkakati sasa wa kuhakikisha kwamba hospitali zetu za halmashauri zinakuwa na mitambo ya kusindika gesi ya oxygen pia kuhakikisha hospitali za rufaa za mikoa zote nchini zinasimika mitambo ya kuzalisha gesi ya oxygen ili tuweze kuondokana na changamoto ya upungufu wa mitungi hii pia kuhakikisha tunaboresha huduma za afya kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mpango huu utakwenda kutekelezwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanyia kazi hayo ili kuhakikisha tunaboresha huduma za afya, ahsante sana.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita? (b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ajira ya mwisho ya watumishi wa vituo vya afya na zahanati iliyotoka iliwachukua baadhi ya watabibu waliokuwa wanafanya kazi kwa mkataba na wengi walipoomba zile ajira walikuwa na nafasi ya kuomba kwamba wabaki wapi. Katika Wilaya yangu ya Longido kuna mmoja aliyekuwa anahudumia zahanati ya Kijiji cha Nondoto ambayo ndio inahudumia kata nzima hakuna nyingine alipoomba kubaki pale alipangiwa kwenda Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia zahanati hiyo mganga?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika ajira watumishi ambao wanaomba kuajiriwa na Serikali wanakuwa na option ya kuchagua vituo ambavyo wanakwenda kufanya kazi. Na katika mfumo wa ajira za hivi karibuni ambazo zimefanyika mwezi Mei mpaka Juni watumishi wote wamepangiwa kwenye vituo ambavyo waliomba kupitia mfumo wa kieletroniki wa ajira kwenda kufanya kazi katika vituo hivyo. Na watumishi wote wamepelekwa kwenye vituo ambavyo waliomba kwenda kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge inawezekana tulimwitaji sana mganga huyu katika kituo hicho lakini uchaguzi wake aliomba kituo kingine na ndio maana amepelekwa. Lakini jambo la msingi ni kupata mganga katika zahanati ile na mimi nimelichukua hili tutalifanyia kazi ili kuhakikisha tunapata mganga kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma katika zahanati ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaja, nakushukuru.