Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustino Manyanda Masele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:- Tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Mbogwe mwaka 2012 watumishi iliyokuwa Wilaya ya Bukombe walihamishiwa Wilayani Mbogwe lakini hawajalipwa stahiki zao za posho ya kujikimu pamoja na zile za usumbufu. Je, ni lini watumishi hao watalipwa stahiki zao?

Supplementary Question 1

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
(i) Naomba niiulize Serikali ni lini sasa madai ya hawa watumishi 65 waliosalia yatalipwa?
(ii) Kwa kuwa posho za kujikimu na posho ya usumbufu ni halali ya mtumishi, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuwa inawalipa watumishi inapowahamisha malipo hayo kwa wakati?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni lini fedha hizi zitalipwa, nimesema katika jibu langu la msingi, kwamba ni kweli pale kuna watumishi ambao wamehamia katika Halmashauri mpya. Katika kuliona hilo sasa tukaona ni vema sasa hii fedha itengwe katika bajeti ya mwaka wa fedha huu ili watumishi waweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndungu yangu Masele naomba uwe na subira tu, kwa sababu katika Bajeti yetu tulivyopitisha tulizungumza mchakato mkubwa katika suala zima la Halmashauri mpya kwa hiyo katika suala hili la ujenzi wa miundombinu lazima uende sambamba na malipo ya madeni ya watumishi mbalimbali. Kwa hiyo, jambo hili tutakwenda kulifanya kwa kadri iwezekanavyo ili watumishi wale wapate utulivu, wafanye kazi yao kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Spika, ni jinsi gani tutafanya Halmashauri zinapoanzishwa madai ya watumishi yaweze kulipwa kwanza, hili tutaliwekea maanani. Lakini Waheshimiwa Wabunge tukumbuke kwamba sasa hivi kuna Halmashauri mpya nyingi sana, ofisini kwangu mpaka sasa hivi nimeaandaa matrix form ya kuona Halmashauri ina Wilaya mpya ambazo Wabunge mbalimbali wameenda kupeleka maombi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuweza kuanzishwa. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa tutakuwanalo ni kuona ni jinsi gani haya matakwa ya wananchi katika maeneo husika yaweze kufikiwa, lakini hatuwezi kuzuia Halmashauri kuanzishwa kwa sababu posho bado hazijapatikana.
Mheshimiwa Spika, tukifanya hivyo tutakuwa tumezuia maendeleo ya wananchi katika maeneo husika, hata ninyi Wabunge hamtoridhika katika hilo. Kwa hiyo, tumechukua ushauri huo wote, lengo kubwa ni mipango yote iende sambamba, Halmashauri zinapoanzishwa na fedha ziweze kulipwa.