Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Shabani Omari Shekilindi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Primary Question
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Jimbo la Lushoto lina Kituo kimoja cha Afya na sasa wananchi wameanza kujenga Vituo vya Afya viwili vya Gare na Ngwelo. Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo na ni lini itafanya hivyo?
Supplementary Question 1
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kituo cha Afya cha Mlola ndiyo kituo pekee kinachohudumia zaidi ya kata nane lakini kiuo kwa muda mrefu hakina gari la wagonjwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwapatia Kituo cha Afya Mlola gari la wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, vituo hivi vya Gare na Ngwelo ni vituo vilivyojengwa na nguvu za wananchi kwa muda mrefu sana. Vituo hivi nilianza kuviongelea tangu 2017, 2018, 2019, 2020 mpaka sasa hivi 2021 lakini hakuna majibu ya kuridhisha, majibu ni haya ya nadharia bila vitendo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari sasa kuongozana nami ili akaone kazi iliyofanywa na wananchi wale? Nadhani hapo ndipo atatupa fedha za kujenga vituo vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani O. Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Mlola kinahudumia wananchi wengi, kata nane katika Jimbo lile la Lushoto na ni kituo muhimu sana kuhakikisha kwamba kinapata gari la wagonjwa ili kiweze kufanikisha rufaa lakini pia na huduma dharura kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Lushoto. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Shekilindi kwamba Serikali inatambua kwamba kituo hicho kinahitaji kuwa na gari la wagonjwa na taratibu za kupata magari ya wagonjwa katika kituo hicho lakini pia katika Vituo vingine vya Afya zinaendelea kufanyika na tutaendelea kupelekea magari hayo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tumelichukua na tunalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na Vituo vya Afya vya Gare na Ngwelo kuanza kujengwa kwa nguvu za wananchi kwa muda mrefu, kwanza, Serikali inawapongeza sana wananchi wa Lushoto kwa kujitolea kuchangia kuanza ujenzi wa Vituo hivi vya Afya. Serikali inatambua sana mchango wa wananchi na itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika kukamilisha vituo hivi vya afya. Naomba nimhakikishie, pamoja na kwamba vituo hivi kwa muda mrefu vimekuwa vikiahidiwa kupatiwa fedha, jitihada zinaendelea kuendelea kutafuta fedha na mara zitakapopatikana Vituo hivi vya Afya vitapewa kipaumbele.
Name
Leah Jeremiah Komanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Meatu
Primary Question
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Jimbo la Lushoto lina Kituo kimoja cha Afya na sasa wananchi wameanza kujenga Vituo vya Afya viwili vya Gare na Ngwelo. Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo na ni lini itafanya hivyo?
Supplementary Question 2
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Changamoto zilizopo Jimbo la Lushoto zinafanana kabisa na zilizopo Jimbo la Meatu kwa kuwa ni Kituo cha Mwanhuzi pekee kilichoongezewa miundombinu ambacho pia kinatumika kama Hospitali ya Wilaya.
Je, Serikali haioni haja ya kuongeza miundombinu katika Kituo cha Afya Bukundi ili kukabiliana na wagonjwa ambao pia wanachangizwa na wagonjwa kutoka Wilaya ya Mkalama?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Bukundi katika Jimbo la Meatu ni muhimu sana na kwa bahati njema nakifahamu vizuri nikiwa nimefanya kazi huko kama Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Nafahamu kwamba tunahitaji kukiboresha na kukitanua kituo kile ili kiweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa sababu kipo pembezoni sana na eneo lile kuna umbali mkubwa sana kufika kwenye vituo vingine vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge Leah Komanya kwamba Serikali inatambua umuhimu huo na mipango inaendelea kufanywa kutafuta fedha. Mara fedha zikishapatikana tutahakikisha kituo hicho ni miongoni mwa vituo ambavyo majengo yake yatakwenda kupanuliwa ili kiweze kutoa huduma bora zaidi za afya.
Name
Kiswaga Boniventura Destery
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Primary Question
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Jimbo la Lushoto lina Kituo kimoja cha Afya na sasa wananchi wameanza kujenga Vituo vya Afya viwili vya Gare na Ngwelo. Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo na ni lini itafanya hivyo?
Supplementary Question 3
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala hili linafanana kabisa na Vituo vyangu vya Kisesa na Nyanguge, ni vituo vya siku nyingi ambavyo havitoi huduma inayostahili kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha hasa kufanya ukarabati na kuvipatia vifaa vya kutolea tiba katika Vituo vya Nyanguge na Kisesa? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kusema kwamba sisi sote Waheshimiwa Wabunge tunafahamu kazi kubwa sana ambayo imefanywa na ambayo inaendelea kufanywa na Serikali yetu katika kuhakikisha kwanza tunajenga vituo vya afya lakini tunakarabati vituo vya afya. Sisi sote ni mashahidi kwa kipindi hiki cha miaka mitano jumla vituo vya afya vipatavyo 487 vimeendelea kujengwa na kukarabatiwa na vimeanza kutoa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hatua moja inatupelekea kuendelea na hatua nyingine. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Kiswaga, kwanza kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kisesa na Nyanguge kwamba vinahitaji ukarabati, ni kweli na suala ambalo tunakwenda kulifanya ni kuanza kuweka taratibu za ukarabati na upanuzi wa vituo hivi kadri ya upatikanaji wa fedha. Tuna kata nyingi, tutakwenda kwa awamu, si rahisi kumaliza vituo vyote kwa pamoja lakini vituo hivi vyote ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na vifaatiba, naomba niwakumbushe watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, maelekezo yalikwishatolewa Serikali imekuwa ikigharamia ujenzi wa vituo hivyo, kuanzia hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati. Katika hospitali za Halmshauri tumetenga bajeti kwa ajili ya vifaa tiba lakini katika vituo vya afya, tumewaelekeza Wakurugenzi katika mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga fedha ili tuweze kununua vifaatiba.
Kwa hiyo, ni muhimu sana Mamlaka ya Halmashauri ya Magu wahakikishe wanatenga fedha katika mapato ya ndani na fedha zipatikanazo na malipo ya cost sharing ili kununua vifaatiba. Kwa ujumla, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha miundombinu hii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.