Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo, lakini ujenzi wa stendi hii ulitakiwa uanze toka mwaka 2010/2011 ambapo Serikali iliweza kuzuia maeneo ya wananchi wa Kata za Moshono na Kata za Olasiti na maeneo hayo yaliwekwa mpaka kwenye master plan ya Jiji la Arusha. Sasa hivi Serikali imefanya maamuzi ya kwenda kujenga stendi kwenye eneo lingine la Bondeni City.

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu ya nyongeza, napenda kufahamu kwanza, je, sasa Serikali ina mpango gani na yale maeneo ya Olasiti na Moshono ambayo yalitengwa maalum kwa ajili ya kujenga stendi na yameishingia kwenye master plan? Je, Serikali sasa hivi inawaruhusu wananchi wale waende wakayaendeleze maeneo yao? Je, wako tayari kupabilisha master plan au Serikali inao mpango wa kulipa fidia?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku wananchi wale walitarajia kwamba Serikali ingeweka shughuli yoyote ya kiuchumi pale, hata kama sio stendi, pengine soko au shughuli yoyote, ingesaidia shughuli za kiuchumi za watu wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mrisho Gambo ushauliza maswali matatu tayari katika swali lako la kwanza la nyongeza na maswali yanayoruhusiwa ni mawili. Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunielewa.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa dhamira ile ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya vitega uchumi kwa maana ya miradi ya kimkakati katika Jiji la Arusha, ilitenga maeneo haya na mradi huu ulitarajiwa kuanza mwaka 2010/2011. Yale maeneo ambayo yalitengwa awali, ni yale ambayo wananchi waliahidiwa kwamba watafidiwa lakini pia ili kitega uchumi kiweze kujengwa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sababu kadhaa ambazo zilifanya Halmashauri ya Jiji la Arusha lakini na Serikali kuona ni vema sasa eneo la Bondeni City ambalo ni kubwa na linaweza likasaidia zaidi kwa maana ya geographical location yake kuwa na stendi ya kisasa ambayo itasaidia zaidi kuboresa mapato lakini pia huduma kwa wananchi wa Arusha. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mrisho Gambo kwamba nalichukua jambo hili twende tukalifanyie tathmini zaidi, tuweze kuona sababu ambazo zimetupelekea kuhamisha kwenda sehemu nyingine lakini tuweze kuona nini kitafanyika sasa katika lile eneo ambalo mara ya kwanza lilikuwa limedhamiriwa kujenga stendi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sehemu ya pili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mrisho Gambo, kama nilivyotangulia kusema Serikali inadhamiria kujenga miradi hii ya kimkakati yakiwemo haya masoko kisasa. Kwanza kuboresha huduma kwa wananchi, lakini pili kuwezesha halmshauri kupata mapato katika vyanzo vyake vya ndani. Baada ya tathmini hiyo na baada ya kumpata Mkandarasi Mshauri tutahakikisha kwamba tunakwenda kuanza ujenzi wa soko hilo la kisasa katika Jiji la Arusha.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi?

Supplementary Question 2

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali Arusha yanahusika kabisa na Mkoa mpya wa Songwe, yanafanana vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Mkoa wa Songwe, kuna eneo ambalo lilikuwa limetengwa la Mbimba TaCRI kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya Mkoa. Kwa kuwa michoro tayari ilishakamilika kwa muda mrefu karibu zaidi ya miaka sasa mitatu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba stendi kubwa ya Mkoa wa Songwe inaanza kujengwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Songwe tunahitaji kujenga Stendi ya Kisasa ya Mabasi. Katika majibu yangu ya msingi, nimeeleza kwamba tunatarajia kujenga stendi katika maeneo haya yote ambayo tayari yamekwishatambuliwa na sasa tunaendelea kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia ili kupata fedha kwa ajili ya kuwezesha sasa ujenzi wa maeneo haya ya miradi ya kimkakati kuanza. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Hasunga kwamba katika miradi hiyo inayokuja, mara mazungumzo yatakapokamilika na fedha hizo kupatikana basi tutaweka kipambele pia katika kuwezesha Kituo cha Mabasi cha Mkoa wa Songwe kuanza kujengwa.

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi?

Supplementary Question 3

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa changamoto za stendi katika Jimbo la Arusha Mjini, zinafana sana na changamoto za kukosekana stendi katika Jimbo la Busokelo. Je, ni lini Serikali itajenga stendi za Miji ya Ruangwa, Ruangwa Mjini pamoja na Kandete?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali inatambua uhitaji wa masoko ya kisasa katika Kata hizo ambazo Mheshimiwa Atupele Mwakibete amezitaja, lakini pia katika maeneo mengine kote Nchini. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira hiyo ya Serikali bado ipo na mipango ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa masoko hayo ya kisasa inaendelea. Mara fedha hizo zitakapopatikana tutahakikisha tunatoa vipaumbele katika maeneo hayo ambayo tayari yamekwishatambuliwa ili tuweze kuwekeza miradi hiyo ya kimkakati na kuwezesha huduma kuendelea. Kwa hiyo, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mwakibete kwamba maeneo hayo pia tutayapa kipaumbele mara fedha zikipatikana ili ujenzi wa masoko hayo uweze kuanza.