Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ghati Zephania Chomete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?

Supplementary Question 1

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na Sera ya Matibabu Bure kuendelea kutekelezeka, lakini bado kuna wazee wengi hawajapatiwa vitambulisho hivyo vya kuwawezesha kupata matibabu hayo:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wazee wote wenye sifa wanapata vitambulisho hivyo ili waweze kunufaika na Sera ya Matibabu Bure? (Makofi)

(b) Kuna malalamiko hata kwa wale wazee wachache wenye vitambulisho hivyo; wanapofika hospitalini wanaambiwa hakuna dawa: Je, ni lini Serikali itahakikisha ukosefu wa madawa huu unakwisha ili kuwaondolea wazee wetu kero hiyo? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Sera ya Wazee inatambua kwamba tunahitaji kuainisha wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo ili waweze kupata matibabu bila malipo. Serikali imeendelea kuweka utaratibu kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauti zetu kupita katika vijiji kwa kushirikiana na Watendaji katika Vijiji na Kata kuwatambua wazee hao wenye sifa, lakini pia kuhakikisha wanapata vitambulisho kwa ajili ya matibabu bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba bado hatujafikia asilimia 100 kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, lakini jiitihada za kuhakikisha tunafikia hapo zinaendea. Naomba nichukue nafasi hii kuwaelekeza Watendaji Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mitaa wote kote nchi kuhakikisha wanaweka mpango kazi wa kuwatambua wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, wasio na uwezo na kuweka mipango ya kuwapatia vitambulisho ili waweze kupata matibabu bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni endelevu, haliwezi kwisha kwa sababu kila siku kuna mtu anafikisha miaka 60. Kwa hiyo, hatuwezi kusema tumemaliza wazee wote, kwa sababu ni suala endelevu, kila mwaka kuna watu ambao wata-turn miaka 60 na Serikali itaendelea kuwatafutia vitambulisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika vituo vyetu kumekuwa kuna malalamiko kwa baadhi ya vituo na baadhi ya Halmashauri kwamba wazee wetu wakifika kwa ajili ya matibabu pamoja na vitambulisho vyao, wanakosa baadhi ya dawa muhimu. Kuna sababu mbili; sababu ya kwanza ni kwamba magonjwa mengi ambayo yanawapata wazee wa miaka 60 na kuendelea mara nyingi baadhi ya dawa zao hazipatikani katika ngazi ya vituo. Kwa hiyo, mara nyingine kunakuwa na changamoto ya magonjwa yale kwa ajili ya advanced cases, lakini wanahitaji kupata labda kwenye ngazi ya wilaya na ngazi ya rufaa, wakienda kwenye vituo vyetu mara nyingine hawapati zile dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka utaratibu wa kuendelea kwanza kuwaelimisha wananchi hao, lakini pia kuweka utaratibu wa kuona namna gani zile dawa muhimu katika maeneo husika zitapatikana ili kuwarahisishia wazee wetu kupata matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili ni ile ambayo nimeelezea kwa ujumla wake kwamba Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika vituo vyetu kote nchini ili kuhakikisha wazee wetu na wananchi kwa ujumla wanapata dawa kama ambavyo imekusudiwa.

Name

Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?

Supplementary Question 2

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo Mara ya wazee kutokutibiwa bure ipo kwenye Jimbo la Ngara ambapo hata wale wazee waliokuwa na vitambulisho walinyang’anywa walipofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya:-

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kufika kwenye Jimbo la Ngara kushuhudia namna ambavyo Sera ya Matibabu Bure haitekelezwi kwa hao wazee na kutoa muafaka wa namna nzuri ya hao wazee kupata huduma za matibabu bure? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Matibabu Bila Malipo kwa Eazee inahusika katika mamlaka zote nchini kote, ikiwepo Halmashauri ya Ngara. Kwa hiyo, naomba kwanza nipokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Jimbo la Ngara kuna baadhi ya wazee wenye vitambulisho walinyang’anywa. Suala hilo halikubaliki na wala siYo maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara na Mamlaka za Serikali za Mitaa za Ngara kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hili mapema. Serikali inaelekeza kutoa vitambulisho vya matibabu kwa wananchi, wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kunyang’anya vitambulisho vile kwa sababu ni kuwanyima haki wazee hao ambao sera inawatambua kwamba wanahitaji kupata vitambulisho hivyo kwa ajili ya matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kulitekeleza hilo, lakini kabla sijaenda, lazima Halmashauri ya Ngara itekeleze maelekezo haya ya Serikali kuhakikisha inaendelea kutoa vitambulisho kwa wazee na hakuna ruksa ya kumnyang’anya mzee yeyote kitambulisho kwa ajili ya matibabu. (Makofi)

Name

Minza Simon Mjika

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?

Supplementary Question 3

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu tuna machine ya X-Ray tuliletewa toka mwaka 2002. Swali langu ni hili, katika hospitali hiyo hatuna mtaalam wa X-Ray:-

Je, ni lini Serikali italeta mtaalam wa X-Ray katika Wilaya hiyo? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu wana mashine ya X-Ray ambayo kwa kipindi kirefu imekosa mtumishi kwa maana ya mtalaam wa X-Ray. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeendelea kuwasiliana kwa karibu na Wizara ya Afya, lakini pia na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuona namna gani tunapata watumishi hawa ili tuweze kupata mtumishi mmoja na kumhamishia katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu. Wataalam hawa bado ni wachache lakini jitihada za Serikali ni kuendelea kuwasomesha ili tuweze kupata wataalam wengi ili waendane na kasi ya ujenzi wa vituo vya afya ambavyo kimsingi vitahitaji kupata watalaam hawa wa X-Ray.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshalifanyia kazi na tulishaainisha mtumishi kwa ajili ya kumpeleka Meatu na wakati wowote atakwenda kuanza kutoa huduma ya X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu. (Makofi)

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Pamoja na nia njema ya Serikali yetu kutoa tiba bure kwa wazee wetu, lakini zoezi zima limegubikwa na ukiritimba wa kutoa tiba kwa wazee wetu.

Je, Serikali haioni busara kuoanisha vitambulisho hivi vinavyotolewa kwa wazee na Bima ya Afya ili wazee wetu wapate tiba stahiki? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme, Serikali imeendelea kuhakikisha inapunguza changamoto ambazo Mheshimiwa anaziita ukiritimba wa Matibabu kwa Wazee Bila Malipo na ndiyo maana tumeainisha utaratibu wa kuainisha, kuwatambua wazee wetu na kuwapa vitambulisho. Hiyo ni sehemu ya jitihada ya Serikali kuhakikisha ule ukiritimba unapungua na kuwawezesha wazee wetu kupata matibabu bila malipo na bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea wazo lake la kuunganisha vitambulisho pamoja na sehemu ya matibabu kwa wazee ili Serikali iweze kulifanyia tathmini na kuona uwezekano wa kufanya hivyo au uwezekano wa kuendelea kuboresha utaratibu uliopo ili tuweze kuboresha huduma.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nilitaka kuongeza kwenye swali la Dkt. Kikoyo kwenye suala la ku-link huduma za matibabu kwa wazee na Bima ya Afya. Jambo moja ambalo lilituchelewesha labda kuleta kwenye Bunge lako Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ilikuwa ni kuweka utaratibu kama huo ambao ukishafanya Bima ya Afya ni compulsory, maana yake lazima Serikali ije na utaratibu wa kuona ni jinsi gani Bima za Afya zitapatikana kwa watu hao kama wazee, akina mama wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali la Dkt. Kikoyo ni zuri. Pale ambapo Serikali italeta Muswaada wa Bima ya Afya, pia itaweka sasa utaratibu ambao utaondoa hizi changamoto za matibabu bure kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kwamba tukimaliza, nadhani tutakuwa tumepata mwarobaini wa tatizo hili. (Makofi)

Name

Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Primary Question

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?

Supplementary Question 5

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunatambua kwamba Serikali ina vituo takribani 16 nchi nzima vya kulelea wazee wetu, lakini huduma za afya zinazopatikana ndani ya vituo vile kwa kweli ni kama huduma ya kwanza tu:-

Je, Serikai haioni kuna haja ya kuweka huduma bora ndani ya vituo vya kulelea wazee wetu? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, majengo au nyumba za kulelea wazee wetu zilizopo kote nchini zinaendelea kupewa huduma za muhimu kwa kutumia taasisi mbalimbali ikiwepo Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuwezesha wazee wetu kuishi katika mazingira bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la huduma za afya katika maeneo hayo, kumekuwa na utaratibu wa karibu wa uratibu kati ya Maafisa Ustawi wa Jamii na Watoa Huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kufika katika maeneo hayo, lakini pia kuweza kuchunguza afya za wazee wetu na kuwapatia matibabu pale inapobidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu tutaendelea kuuimarisha kuona namna gani wataalam katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa wanaweka utaratibu wa mara kwa mara wa kuwatembeala wazee wetu katika maeneo hayo wanayoishi na kutambua wale wenye dalili za kuhitaji matibabu waweze kupata matibabu kwa urahisi zaidi. (Makofi)