Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bonnah Ladislaus Kamoli
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI K.n.y. MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wa Chalinze waliopisha ujenzi wa miundombinu ya miradi ya kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi na Bwawa la Mwalimu Nyerere?
Supplementary Question 1
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nataka kujua ni lini Serikali italipa fedha hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu mradi huu umekaa sasa ni miaka minne, je, Serikali ipo tayari kuwapa kifuta jasho wananchi ambao wamesubiri kwa muda wote huo wakati wakisubiri malipo haya? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Bonnah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nieleze kidogo kwamba fidia inayotakiwa kufanyika katika maeneo haya ni fidia ambayo ni ya miradi ambayo tunaweza kuiita miradi ambatanishi. Kimsingi umeme unaozalishwa katika Bwawa letu la Mwalimu Nyerere megawatt 2,115 unatakiwa utoke Mwalimu Nyerere kuja kuingia katika Gridi ya Taifa na unaingilia kwenye Gridi ya Taifa pale Chalinze. Kwa hiyo, itajengwa hiyo njia ya kutoka Mwalimu Nyerere kuja Chalinze, lakini Chalinze kwenda Kinyerezi na Chalinze kuja Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuhusu exactly fidia italipwa lini ni tusema ni kabla ya kufika mwezi wa kumi mwaka huu, kwa sababu lazima kwanza tulipe fidia ndiyo tutaweza kujenga njia hiyo ya kupeleka umeme. Njia hiyo ya kupeleka umeme lazima ikamilike kabla ya tarehe 14 Juni, 2022 ili iweze kusafirisha ule umeme utakaozalishwa pale Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fidia itatolewa kwa wakati na haitochelewa kwa sababu kuchelewa kwa fidia hiyo kutasababisha mradi wa Mwalimu Nyerere usiweze kuingiza umeme wake kwenye grid.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili kama Serikali ipo tayari kuwapa kifuta jasho, niwahakikishie waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoendeshwa na Mama yetu Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni Serikali sikivu na isiyoonea mwananchi taratibu za fidia zipo na zinafahamika kwamba inalipwa kwa namna gani na ndani ya wakati gani. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa fidia stahiki italipwa kwa kila anayestahili kulipwa kwa mujibu wa viwango vya kisheria vilivyowekwa na muda uliowekwa kwa ajili ya hesabu hizo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved