Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- (a) Je, ni nini sababu ya kuweka tozo ya ada ya tathmini ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambapo asilimia 50 inalipwa kabla ya kuanza kufanya tathmini na asilimia 50 inalipwa baada ya mkopo kuidhinishwa? (b) Je, ni kigezo gani kilisababisha tozo kuwa asilimia 1 na si vinginevyo? (c) Je, mkopo usipoidhinishwa hiyo asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa inarudishwa ama la?

Supplementary Question 1

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Sekta ta kilimo ni sekta ambayo inaajiri kati ya asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania, hii ni robo tatu ya Watanzania wanategemea hii sekta moja kwa moja, directly ama indirectly. Lakini sasa ukiangalia mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi kwa mwaka huu uliopita eneo la kilimo ambalo linategemewa na asilimia 65 mpaka 70 ya Watanzania limepata asilimia 8.7 tu ya mikopo yote iliyotolewa kwa sekta binafsi. Sasa na hii inajumuisha Benki ya Kilimo yenyewe pamoja na hizi benki nyingine. Sasa hiki ni kiashiria kwamba, mazingira ya kibenki sio rafiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, kwa kuzingatia haya, Serikali ina mikakati gani, mosi kuiongezea mtaji benki ya kilimo, lakini pili kuzungumza sasa na mabenki haya mengine ya biashara ili kuwe kuna riba rafiki ili wakulima waweze kukopa mikopo? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, Benki ya Kilimo ni miongoni mwa benki ambayo ina mikopo chechefu sana, na taarifa ya CAG iliyopita imeonesha kwamba, kati ya mikopo chechefu ya shilingi bilioni 129 iliyorekodiwa ni mikopo chechefu ya shilingi bilioni 2.1 tu iliyoweza kukusanywa. Sasa Serikali ina mkakati gani basi, kuhakikisha kwamba, hii mikopo inakusanywa ili kutoa nafasi kwa wakulima wengine kuweza kukopa na benki kuendelea kama kwaida? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali maswali aliyoyasema. Na kipengele cha pili cha swali lake ndio kinatoa majibu ya kipengele cha kwanza kwamba, ni kwa nini inaonekana mikopo inayokwenda kwenye sekta hiyo ni kidogo:-

Mheshimiwa Spika, sababu yake ni hiyo ambayo umeweza kuona kwamba, hata Mdhibiti, CAG, aliweza kuonesha kwamba, sekta hiyo inaongoza kwa mikopo chechefu.

Mheshimiwa Spika, na sababu kubwa na ameuliza mkakati ni nini wa Serikali:-

Mheshimiwa Spika, utasikiliza mara kwa mara Waziri wa Kilimo amelisemea ni kuibadilisha sekta nzima, ili itoke kwenye ubahatinasibu kwenda kwenye uhakika. Na sehemu ya kwanza ambayo Mheshimiwa Waziri wa kilimo ameweka mkazo, kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameelekeza nguvu ielekezwe, ni kuanzia na mbegu bora zenyewe. Kwamba, mtu anapokopa halafu akaenda kuwekeza kwenye kilimo, halafu akatumia mbegu bora ana uhakika wa kupata kutokana na kile kilichowekezwa. Kwa maana hiyo sekta nzima ikibadilishwa ikawa sekta ya uhakika, mbegu bora, kilimo cha umwagiliaji, matumizi bora ya zana za kilimo pamoja na uhifadhi pamoja na masoko, ukiukamilisha ule mnyumburisho wote maana yake unamfanya yule aliyekopa akawekeza kwenye kilimo awe na uhakika wa kurejesha.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo utaratibu ule utakapokuwa umekamilika kwa kuanzia na hilo la mbegu bora pamoja na vingine ambavyo viko kwenye mpango wa sekta ya kilimo vitawezesha sekta hiyo iwe ya kutabirika na ya uhakika na hivyo, itawezesha mtu aweze kukopa. Na ikishakuwa ya uhakika hata benki zitakuwa na uhakika wa kukusanya kutokana na hiyo kwa hiyo, riba zitakuwa rafiki.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali kuiwezesha, kuiwekea nguvu; tutaendelea kuliangalia kwa sababu ni moja ya kipaumbele ambacho tunalenga ili kuweza kuwezesha uchumi wa viwanda, lakini pia kukuza kipato cha kila Mtanzania, ili tuweze kusonga mbele kiuchumi.

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- (a) Je, ni nini sababu ya kuweka tozo ya ada ya tathmini ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambapo asilimia 50 inalipwa kabla ya kuanza kufanya tathmini na asilimia 50 inalipwa baada ya mkopo kuidhinishwa? (b) Je, ni kigezo gani kilisababisha tozo kuwa asilimia 1 na si vinginevyo? (c) Je, mkopo usipoidhinishwa hiyo asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa inarudishwa ama la?

Supplementary Question 2

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, iliyokuwa benki ya FDME, sasa ni zaidi ya miaka minne tangu BOT waifunge. Wananchi wa Arusha na sehemu mbalimbali waliokuwa na akaunti katika benki hiyo hadi leo hawajui hatima ya pesa zao. Nini kauli ya Serikali?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri. Na mara zote amekuwa kinara wa kuwatetea wananchi wa Tanzania, hasa wa Arusha, nadhani ndio maana huwa wanamchagua mara kwa mara:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwepo na zoezi hilo la kuichukua iliyokuwa benki ya FDME na kilichochelewesha ni ule utaratibu ambao ni wa kawaida unapoikabiodhi kwa mufilisi kwa hatua zile. Kwamba, unatoa kile cha kwanza ambacho kiko kisheria kwa wale ambao walikuwa na akiba zisizozidi kiwango kilichowekwa kisheria, lakini kwa wale ambao viwango vyao vilikuwa zaidi ya kiwango kinachogawanywa kwa awamu ya kwanza huwa ni lazima zoezi la mufilisi likamilike kwanza.

Mheshimiwa Spika, na zoezi hilo linahusu uhakiki wa mali zote zilizopo zikusanywe, ziuzwe, halafu zikishauzwa zikageuzwa kuwa fedha ndio watu wale waweze kugawanywa, wale ambao akiba zao zilikuwa zinazidi kiwango cha kwanza ambacho kilikuwa kimegawanywa. Sasa kwa kuwa zoezi hilo kukamilika linachukua muda, kuhakiki mali uzipate zote, lakini pia uzibadilishe ziwe fedha linachukua muda, hicho ndicho ambacho kimechelewesha.

Mheshimiwa Spika, sasa ni lini itakamilika?

Mheshimiwa Spika, nakumbuka utaratibu huu ulikuwa bado unaendelea na ulikuwa hatuia nzuri. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge tutakapokuwa tumemaliza zoezi lako la hapa Bungeni nitapata taarifa ambapo imeshafikia hatua gani ili niweze kujua ni lini watakuwa wameshakamilisha kwasababu, zoezi lilikuwa linaendelea.