Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya barabara za Newala Vijijini ambayo imetengewa fedha za kilometa 340 wakati zina mtandao wa barabara wa kilometa 960? (b) Je, Serikali inatoa msaada gani wa dharula kwenye matengenezo ya barabara za vijijini vinavyozungukwa na milima au mito kama vile Mkongi – Nanganga, Mikumbi – Mpanyani, Namdimba – Chiwata, Mkoma – Chimenena na Miyuyu – Ndanda?
Supplementary Question 1
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Wazir nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara Miyuyu - Ndanda kimekuwa kimetengewa fedha mara kwa mara za matengenezo ya kawaida, lakini fedha hizo hazitibu shida iliyoko kwenye mlima pale na barabara ile ni barabara ambayo inatumika kwa wagonjwa kutoka Wilaya za Newala na Tandahimba wanaopata rufaa kwenda Hospitali ya Ndanda. Hali ya pale ni mbaya, ni mlima kumbwa na korongo kubwa kiasi kwamba inahatarisha usalama kwa watumiaji wa barabara ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata kauli ya Serikali. Ni lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ile hasa kipande kile ili wananchi wanaotumia hospitali ya Ndanda kama hospitali ya Rufaa waweze kupata urahisi wa kufika hospitalini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo la Newala Vijijini, zimesababisha athari kubwa sana ya barabara kukatika magari hayapiti, hata pikipiki zinapita kwa shida, kwa mfano barabara kutoka Malatu Shuleni - Namkonda hadi Chitekete, barabara ya Maputi - Meta, barabara ya Likwaya Nambali, barabara ya Mtikwichini - Chikalule, barabara ya Mtikwichini - Lochino na Chikalule.
Mheshsimiwa Naibu Spika, upi mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa ajili ya dharura ya kutengeneza barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki? Ahsante.
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge aliuliza eneo korofi la Mlima Miyuyu mpaka Ndanda na amesema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha, lakini bahati mbaya tatizo hilo limekuwa halitatuliki, kwa hiyo, alikuwa anaiomba Serikali ni lini itajenga lami katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu peke ninachoweza kumuhakikishia ni kwamba kutokana na ombi alilolileta na sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutakwenda tufanye tathimini na baada ya hapo tutaleta majibu ya eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sehemu ya pili barabara ambazo amejaribu kuzitaja Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini anafanya kazi hii kwa nia njema ya kusaidia wananchi wake wa Jimbo la Newala, ameainisha maeneo mengi sana na kutaka mpango wa dharura na lenyewe nimuhakikishie kwamba Serikali tumesikia na kwa sababu katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha yakiwemo hayo maeneo ambayo ameyaainisha, lakini Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta vyanzo vingine.
Kwa hiyo kulingana na bajeti itakavyopatikana na sisi tutaakikisha kabisa kwamba tunatatua matatizo ya wananchi wa Newala na maeneo mengine ya Tanzania. Kwa hiyo, ahsante sana Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yako na nikupongeze kwa kazi nzuri kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved